Alhamisi, 29 Agosti 2024

MTENDAJI MKUU MAHAKAMA YA TANZANIA AWATAKA WATUMISHI KATAVI KUTIMIZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO

Na. JAMES KAPELE –Mahakama, Katavi

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi kutimiza majukumu yao ipasavyo ili malengo yaliyowekwa na Taasisi, ikiwemo kutoa haki kwa wakati kwa wananchi yaweze kutimia.

Prof. Ole Gabriel alitoa wito huo jana tarehe 28 Agosti, 2024 alipopata fursa ya kuwasalimia watumishi katika Mahakama hiyo na kuzungumza nao akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Katavi unaotekelezwa na Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd chini ya Mkandarasi Mshauri Kiongozi M/s Crystal Consultants.

Aliwatia shime kufanya kazi kwa bidii ili malengo ambayo Mahakama imejiwekea katika mkakati wake unaoendelea kutekelezwa sasa yatimie bila kikwazo chochote.

“Nimefurahi sana kuwakuta katika ari nzuri ya uchapaji kazi, tena mkiwa nadhifu sana. Niwatake mfanye kazi zenu vizuri na kila mtu atimize majukumu yake ipasavyo ili malengo tunayojiwekea wenyewe kama ilivyo kwenye mpango mkakati tunaoutekeleza sasa yanatimia bila kikwazo chochote kwa lengo la kuwahudumia wananchi wetu,” alisema.

Aidha amempongeza Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Katavi, Bw. Allan Mwella kwa kuendelea kuyatunza majengo mapya ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi na Mahakama ya Wilaya Mpanda.

Mahakama hizo zilizinduliwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani tarehe 18 Januari, 2024.

“Nikupongeze sana Mtendaji wa Mahakama kwa kuyatunza majengo haya katika kiwango kizuri, yanaonekana katika kiwango kizuri mno, ni kama tumezindua jana tu. Hongereni sana kwa utunzaji wa miundombinu,” alisema. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitia saini katika kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama Katavi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na watumishi katika eneo la wazi la Mahakama hiyo.

Pichani ya pamoja ya watumishi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel baada ya kumaliza kikao chake.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni