Alhamisi, 15 Agosti 2024

RAIS SAMIA AMWAPISHA DKT. FELESHI KUWA JAJI MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 15 Agosti, 2024 amemwapisha Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Uapisho huo umefanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama, akiwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Zungu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Katika hafla hiyo, kulikuwepo pia na uapisho wa Viongozi wa Serikali, wakiwemo Mawaziri, Katibu Tawala wa Mkoa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Wakuu wa Taasisi.

Akizungumza baada ya uapisho wa Viongozi hao aliowateua jana tarehe 14 Agosti, 2024, Rais Samia alisema kuwa mabadiliko aliyoyafanya ni ya kawaida katika kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao.

“Tunachotarajia kwenu ni kwenda kuongeza ufanisi kwenye maeneo yenu. Nendeni mkaishi viapo mlivyoapa na kufuata maadili ya kikazi yanayotakiwa,” alisema.

Mhe. Dkt. Samia aliwakumbusha wateule hao kuwa wakati wa kufanya kazi kuna utaalam waliousomea na kujiongeza kwa kutumia akili ya kawaida, hivyo akawasihi pale wanapoona inafaa wafanye hivyo katika kuwatumikia wananchi.  

Naye Makamu wa Rais, akiongea katika hafla hiyo, aliwaeleza Viongozi hao kuwa viapo walivyoapa mbele ya Rais na umma kwa ujumla ni vizito, hivyo akawasihi kuviishi katika nafasi zao.

“Matumaini ya Rais aliyewapa dhamana hiyo na Watanzania ni kwamba watapata huduma bora katika nafasi zenu mbalimbali. Kila mmoja aende akafanye kazi kwa bidii, mkashirikiane na Viongozi wengine ambao mtawakuta katika nafasi zenu ili kwa ujumla kama Taifa tuweze kwenda haraka zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahimiza Viongozi hao kurejesha imani waliyoaminiwa na Rais kwa kuwajibika kwake na Taifa kwa ujumla. Aliwaeleza kuwa dhamana walizopewa ni kubwa, zinahitaji kujiamini, nidhamu na weledi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimwapisha Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania katika hafla iliyofanyika  leo tarehe 15 Agosti, 2024 Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam. Picha chini, Mhe. Dkt. Feleshi akisaini kiapo chake.


Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eliezer Mbuki Feleshi akitoa ishara ya shukrani mbele ya Rais Samia (hayupo kwenye picha) baada ya kuapishwa.

Viongozi mbalimbali walioapishwa katika hafla hiyo wakila kiapo cha maadili.

Viongozi Wakuu waliohudhuria hafla ya uapisho huo. Kutoka kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Zungu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango akizungumza katika hafla ya uapisho huo.


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Hassan Zungu akizungumza katika hafla hiyo.

Viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakimpongeza Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi baada ya kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania. Picha chini akipongezwa na Majaji wenzake wa Mahakama ya Rufani pamoja na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kulia).




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni