Jumanne, 6 Agosti 2024

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KUANZISHA MFUMO WA KURATIBU AJIRA, MAADILI NA NIDHAMU

 Na Lydia Churi na Evelyne Odemba- Morogoro

Tume ya Utumishi wa Mahakama inakusudia kuanzisha mfumo wa kielekitroniki utakaoratibu masuala ya Ajira, Maadili na nidhamu kwa watumishi wa Mahakama.

Katika mchakato wa kuanzishwa kwa Mfumo huo, leo Agosti 6, 2024 Tume imekutana na wadau wake muhimu katika kikao kazi kilichoanza mjini Morogoro kwa lengo la kupokea maoni na mapendekezo kwa lengo la kuanzisha mfumo huo utakaorahisisha utendaji kazi na kuleta uwazi zaidi.

Akifungua rasmi kikao kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor alisema kuanzishwa kwa mfumo wa Kielekitroniki wa Ajira, Maadili na nidhamu ndani ya Tume ya Utumishi wa Mahakama  ni muendelezo wa safari mageuzi ya mfumo ya Mahakama ya Tanzania ili kuboresha shughuli za utoaji haki nchini.

”Katika dunia ya sasa teknolojia inakua kwa kasi na shughuli nyingi za Serikali inafanywa kwa mfumo huo, kwa kutambua hili, Tume imeona ni vema kuwa na mfumo wa kielekitroniki utakaoratibu masuala ya Ajira, Maadili na Nidhamu kwa watumishi wa Mahakama”, alisema.

Aidha, Jaji Mansoor alitoa rai kwa wadau kutoa michango ya mawazo itakayozaa matunda yatakayowezesha kujengwa kwa mfumo bora zaidi wa ajira ambao utafungamanishwa na mfumo wa kielekitroniki wa uendeshajiwa Kamati za maadili ambazo Wenyeviti wake ni wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.

Awali akitoia neno la utangulizi, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama  ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kupata maoni ya wadau kuhusu uanzishwaji wa mfumo ambao utaleta mabadiliko ya Utendaji kazi wa Tume.

“Nia yetu ni kuona kwamba Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania inaenda kuwa kitovu cha mageuzi ndani ya Afrika na duniani kote katika matumizi ya TEHAMA”, alisema.

Alitaja baadhi ya mada zilizowasilishwa katika kikao kazi hicho kuwa ni pamoja na rasimu ya mafunzo kuhusu mfumo huo, rasimu ya masuala ya ajira, kushirikishana uzoefu wa masuala ya TEHAMA na kujadiliana namna ya kuboresha mfumo huo ulioanza kujengwa.  

Alisema kuwa ujio wa mfumo huo utasaidia katika kusimamia rasilimali watu, ajira, maadili na nidhamu na utakuwa na manufaa kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama na watanzania kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bw. Jocktan Bikombo alisema kuwa Tume imedhamiria kuanzisha kuanzisha Mfumo ambao utasaidia kupanua wigo wa kiutendaji kazi wake.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor akifungua kikao kazi maalum kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfumo wa kuratibu Ajira, Maadili na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 6 Agosti, 2024 mjini Morogoro.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzaniua Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa Kikao Kazi Maalum kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfumo wa kuratibu Ajira, Maadili na Nidhamu wa Tume leo tarehe 6 Agosti, 2024 mjini Morogoro.
Sehemu ya Viongozi wa Tume, Mahakama pamoja na Wadau wakiwa kwenye kikao kazi maalum kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfumo wa kuratibu Ajira, Maadili na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 6 Agosti, 2024 mjini Morogoro. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya.
Sehemu ya Watumishi wa Tume, Mahakama pamoja na Wadau wakiwa kwenye kikao kazi hicho. Wa pili Kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa Bi. Souz Ngate.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau wakiwa kwenye kikao kazi hicho. Katikati ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimawatu wa Mahakama ya Tanzania Bi. Beatrice Patrick
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Latifa Mansoor (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Tume, Mahakama pamoja na wadau mara baada ya kufungua kikao kazi maalum kwa ajili ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mfumo wa kuratibu Ajira, Maadili na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 6 Agosti, 2024 mjini Morogoro.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni