Jumatano, 4 Septemba 2024

JAJI MKUU ATETA NA VIONGOZI WA MAHAKAMA WALIOAPISHWA NA KUPEWA NYENZO ZA KAZI

Na Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi kutambua kuwa wao ni Viongozi wa Mahakama watakaowakilisha Uongozi wa Mahakama na watumishi wa ngazi mbalimbali katika majukumu yao mapya watakayoyatekeleza maeneo mbalimbali waliyopangiwa hapa nchini.

Akizungumza katika hafla fupi mara baada ya kuwakabidhi nyenzo za kufanyia kazi Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi watano leo tarehe 04 Septemba, 2024 jijini Dar es salaam, Mhe. Prof. Juma amewambia Viongozi hao kuwa wao kazi yao ni nyepesi iliyotajwa katika Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosisitiza utoaji wa haki.

“Hatuna kazi kubwa sana zaidi ya utoaji wa haki katika ngazi mbalimbali za kimahakama na kwa bahati nzuri kuna maelekezo mengi ya namna hiyo, haki inatolewa kwa namna gani. Mathalani kutoa haki kwa kuzingatia sheria ninaimani wote tunafahamu…

"...vilevile kufuata kanuni za kutenda haki bila kujali hali ya mtu na bila upendeleo kulingana na viapo vyetu, kutochelewesha haki, kujaribu kutoa fidia pale panapo stahili na pia kutofungwa na masharti ya kiufundi na kuzingatia maadili,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu akawahimiza Viongozi hao kuwa, wakiweza kusimama katika misingi hiyo kila jambo watakaloshughulika nalo litakwenda vizuri. Hivyo akawatakia mema na fanaka katika kazi zao za kila siku.

Kwa upande mwingine, Mhe. Prof. Juma akawakumbusha Viongozi hao kwenda kusimamia Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na Programu ya Maboresho ya huduma za kimahakama yanayoendelea. 

Akawasisitiza Mahakimu Wakazi Wafawidhi hao waliokabidhiwa nyenzo za kutendea kazi na Naibu Wasajili walioapishwa kuwa wana kazi kubwa ya kuwa mawakala wa maboresho kwa kuyasemea na kusimamia.

“Unajua wananchi wanapozungumzia maboresho wanajua ni majengo tu, kumbe sisi mtaji wetu mkubwa ni yale mambo yanayotokana na majengo, yanayotokana na mabadiliko ya sheria, ndiyo yana faida kubwa zaidi katika maboresho kuliko yale mambo yanayoonekana kuwa mawakala wa maboresho ni pamoja na kwenda kutenda haki,” ameongeza Jaji Mkuu,.

Vile vile, Jaji Mkuu amewahimiza Viongozi hao kutathimini mwelekeo wa shughuli za Mahakama hasa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwa mabalozi wazuri katika matumizi ya mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri (e-Case Management System) ambao umeshaanza kufanya kazi kwa mafanikio makubwa na programu ya kudijiti nyaraka na kumbukumbu ili kuachana na matumizi ya karatasi, huo ndiyo mtihani mkubwa ambao Mahakama inaendelea nao.

"Tayari kuna mifano ya mafanikio kwa baadhi ya Mahakama mfano, Mahakama ya Wilaya Kigamboni wamepiga hatua kubwa sana katika kuhama kutoka kwenye matumizi ya kutumia karatasi (Paperless Court) katika shughuli za huduma za utoaji haki na pia Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita vile vile hawatumii karatasi. Tukiweza kutoka kwenye matumizi ya karatasi nadhani thamani ya haki tunayotoa itakuwa kubwa zaidi, tutakuwa wawazi zaidi, tutakuwa na ufanisi zaidi na tutakuwa na ubora zaidi,” ameongeza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine Jaji Mkuu amewataka viongozi hao kupenda kujisomea na kujiendeleza hata kwa kujifunza kutoa kwa viongozi wenzao kujua wanafanya nini katika maeneo yao kila siku wanapotimiza majukumu yao. Wanakabiliana vipi na changamoto zinazojitokeza za kimahakama hususani kwenye vyombo vya habari na namna ya kuzitatua.

“Kazi yetu ni kazi ya umma kwa hiyo tukubali kukosolewa, tunaweza kukosolewa kwa haki na vilevile tunaweza kukosolewa kwa kuonewa na siku zote huwa hatupigi kelele. Kwa sababu mtu anayekukosoa anaweza kuwa anakukosoa kwa kutokuelewa kwa hiyo ni jukumu lako kumelimisha na kuna wengine wanakukosoa kwa makusudi tu wakiwa wanafahamu ukweli uko wapi ila anakukosoa tu, huyo unamsamehe lakini lengo letu ni kuhakikisha tunawafikia wananchi wa kawaida,” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiteta na Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi (hawapo pichani) walioteuliwa na kuapishwa na kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi leo tarehe 04 Septemba, 2024 ofisini kwake jijini Dar es salaam.

Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Ally Abdallah Mkama akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)


Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Francis Mweiga Kishenyi akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto).

Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Veronica Lucas Mugendi akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)
Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Aristida Veterian Tarimo akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)

Hahakimu Makazi Mafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Mhe. Mwanaheri Kassim Rashid akikabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto)






Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) mara baada ya kukabidhiwa nyenzo za kufanyia kazi.

Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) mara baada ya kuapishwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mohamed Mustapher Siyani ofisini kwake jijini Dar es salaam.


Wananchama wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa kwenye picha ya pamoja Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) mara baada ya hafla hizo mbili.


Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki hafla ya kuwaapisha Manaibu wasajili na kuwakabidhi nyenzo za kufanyia kazi Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) mara baada ya hafla hizo mbili.

Picha na Innocent Kansha- Mahakama

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni