Jumatatu, 2 Septemba 2024

JENGO LA MAHAKAMA YA MWANZO KABANGA LAZINDULIWA

Na AHMED MBILINYI – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi hivi karibuni alizindua jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Kabanga kwa ajili ya utoaji wa huduma za kimahakama.

Mahakama hiyo ipo katika Tarafa ya Kanazi, Kata ya Kabanga, Kitongoji cha Mundimanga, Kijiji cha Murukukumbo, Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Banzi alionyesha furaha isiyo ya kifani kwa Mhimili wa Mahakama, wananchi wa Kabanga na Wilaya ya Ngara na majirani zake kwa kupata jengo zuri na la kisasa. 

“Ikubukwe kwamba kabla ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kabanga Wilaya ya Ngara, wananchi walilazimika kusafiri umbali wa kilometa 17 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Kanazi na umbali wa Kilometa 20 kupata huduma katika Mahakama ya Mwanzo Mabawe...

“Umbali wa hapo awali wa kufuata huduma katika Mahakama za Mwanzo Kanazi na Mabawe ulikuwa mrefu na wananchi waliathirika kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta huduma za Mahakama, muda ambao wangeutumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii,” alisema.

Jaji Mfawidhi alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kutumia Mhimili wa Mahakama kupata haki zao badala ya kwenda kwenye Mahakama zisizo rasmi kwani, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 107A, Mahakama ndio Taasisi pekee iliyopewa jukumu la kutoa haki.

Awali, Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Ngara, Bw. Sauweli Urio, kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba, alitoa taarifa ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kabanga.

“Mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kabanga ulianza tarehe 19 Machi, 2021 na Mkandarasi alikuwa ni Kampuni ya Silva Investments Limited na Mshauri Elekezi wa mradi alikuwa Wakala wa Majengo Tanzania kupita Meneja wake Kagera,” Bw. Urio alisema.

Alibanisha kuwa mradi ulikamilika mwezi wa sita 2024 na tayari jengo lilmeshaanza kutumika tangu mwezi wa saba 2024. Bw. Urio alieleza kuwa kuanza kutumika kwa jengo hilo kumeboresha utoaji huduma za kimahakama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi akisoma hotuba ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya mwanzo Kabanga.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Afisa Tarafa, Bw. Jawadu Yusuph akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Ngara.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ngara, Mhe.Terrysophia Tesha akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo.

Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Ngara, Bw. Sauweli Urio akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kabanga.

Viongozi wa Dini, wadau wa haki jinai wa Wilaya ya Ngara na wananchi wa Kabanga wakisikiliza hotuba ya uzinduzi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya TanzaniaKanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (hayupo pichani).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama, wafanyakazi wa Mahakama ya Wilaya Ngara pamoja na wadau wa haki jinai wa Wilaya ya Ngara wakati wa uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Kabanga. 
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni