Jumamosi, 28 Septemba 2024

MAHAKIMU KANDA YA TABORA WAPIGWA MSASA

Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora

Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Tabora wamepatiwa mafunzo ya siku mbili  yaliyosheheni mada mbalimbali lengo likiwa ni kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kisheria na kuboresha utendaji kazi.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo tarehe 25 Septemba, 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Jaji Dkt. Mwajuma Juma Kadilu alisema, “Mafunzo ni sehemu muhimu katika ukuaji wa taaluma yoyote.”

Mhe. Dkt. Kadilu alisema Mafunzo hayo na mada zitakazofundishwa yataongeza uelewa wa masuala mbalimbali sambamba na kurahisisha utekelezaji wa majukumu.

Mada zilizofundishwa kwenye mafunzo hayo yaliyomalizika tarehe 26 Septemba, 2024 ni pamoja na vitendo na hatua za usikilizaji wa Mashauri katika Mahakama za Mwanzo, changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika usikilizaji wa mashauri, mirathi, uandishi wa hukumu, uendeshaji binafsi wa mashtaka na uwepo wa Mawakili katika Mahakama za Mwanzo.

Nyingine ni Afya ya Akili na udhibiti wa msongo wa Mawazo, uwasilishaji wa ushahidi wa kielektroniki mahakamani: Sheria, Kanuni zinazoongoza ushahidi wa Mtoto Mdogo: Mazoezi na Utaratibu.

Watoa mada katika mafunzo hayo walikuwa ni Kaimu Jaji Mfawidhi pamoja na Majaji wengine wa Kanda hiyo akiwemo Mhe.Dkt. Zainabu Mango, Mhe. Dkt Mwajuma Kadilu.

Watoa mada wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Simon Swai, Bw. Kelvin Kayaga na Bw. Roghat Robert.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt Jaji Mwajuma Kadilu akifungua mafunzo ya Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Tabora.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe.Dkt. Zainabu Diwa Mango akitoa mada wakati wa mafunzo kwa Mahakimu wa Kanda hiyo.
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia moja ya mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Pamela Mazengo akiwasilisha mada katika mafunzo kwa Mahakimu wa Kanda hiyo.


Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu wa Mahakama Kanda ya Tabora walioshiriki kwenye mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni