Alhamisi, 19 Septemba 2024

USIKILIZWAJI WA MASHAURI YA MAUAJI MBEYA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAHABUSU GEREZENI

 

Na DANIEL  SICHULA-Mahakama Kuu, Mbeya

 

Jumla ya mashauri 30 yanatarajiwa kumalizika katika kikao cha kusikiliza mashauri ya mauaji Mahakama Kuu  ya Tanzania Kanda ya Mbeya  mwishoni Novemba ,2024 na kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani.

 

Hayo yalisemwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, katika kikao kilichofanyika hivi karibuni, mbele ya Mhe. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe.Joachim Tiganga ambaye pia aliongozana na Mhe. Jaji Musa Pomo.

 

“Katika vikao hivyo vitatu tumepanga jumla ya mashauri 30 (thelathini). Kati ya hayo mashauri ishirini na tisa (29) ni ya mauaji na shauri moja la dawa za kulevya. Mashauri yote haya  yanatarajiwa kushughulikiwa ndani ya miezi miwili kuanzia tarehe 23, Septemba mpaka tarehe 27, Novemba 2024, ambapo mashauri yote haya ni ya mlundikano na yale yanaelekea kuwa mlundikano ifikapo Desemba 2024,” alisema Mhe. Temu.  

 

Aidha katika kikao hicho cha awali kujadili mashauri hayo ya mauaji, kimehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, na Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), na washiriki wote wamehaidi kutoa ushirikiano mzuri ili mashauri yasikilizwe na kumalizika kwa muda uliopangwa. 

 

Kwa upande wake Mhe.  Tiganga, aliwaomba wadau wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa weledi ili kuongeza ufanisi wa usikilizwaji wa mashauri yote yaliyopangwa kusikilizwa ndani ya kipindi hicho.   Alihimiza mawakili na wadau wote kuhakikisha wanafika gereazani mapema na kuongea na mahabusu wenye kesi hizo na kubaini mapema endapo kutahitahika wakalimani.

 

“Mnapaswa kuandaa wakalimani kwa mashahidi na mahabusu ambao hawana ujuzi wa kuelewa na kuzungumza lugha mama ya Taifa (Kiswahili) ili kurahisisha usikilizwaji wa mashauri (kesi) na kuenda na muda uliopangwa kwani inaelekea kuna baadhi ya mahabusu kukosa uelewa wa kuzungumza Kiswahili” alisema Mhe. Jaji Tiganga.

 

Pia, Jaji Mfawidhi alisisitiza kutumia vizuri muda uliopangwa kusikiliza mashauri hayo na amewataka mawakili wote kuwa wa wazi wakati wa usikilizwaji wa mashauri kwa kukumbushana masuala ya uelewa wa pamoja wa sheria kwenye hoja mbalimbali kwa kutumia lugha za staha.

 

“Ni nia yetu sote kuona mashauri yote yaliyopangwa yanasikilizwa na kutolewa maamuzi kwa wakati. Tunapaswa kuwa wawazi wakati wote wa usikilizji wa mashauri kwa kukumbushana mambo mbalimbali ya kisheria kwa kutumia lugha za staha mahakamani. Hili litatusaidia sana kufikia malengo tuliyojiwekea,”alisisitiza.

 

Naye mwakilishi wa Gereza Kuu Ruanda lililopo hapa Mbeya, aliipongeza Mahakama na wadau kwa jitihada wanazoedelea kuweka na kuhakikisha msongamano wa mahabusu gerezani umepungua kwa kiasi kikubwa ndani ya muda mfupi. 

 

Sambamba na hayo yote, wadau wamesisitizwa pia kutoa ushirikiano na kujiandaa kufanya mahojiano na mashahidi wanaotoka nje ya Kanda ya Mbeya kwa njia ya mtandao (video Conference) ili kuwapunguzia gharama za usafiri na kuokoa muda utakaowasaidia kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, (aliyesimama) akisoma taarifa kuhusu mashauri hayo.




Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe.Joachim Tiganga(katikati) akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.

 


    Wadau wa   Mahakama wakiwa katika kikao hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni