Jumamosi, 7 Septemba 2024

WANAFUNZI WA SEKONDARI MWAKIJOMBE WATEMBELEA MAHAKAMA KUU TANGA

Na MUSSA MWINJUMA- MahakamaTanga

wanafunzi wapatao 138 wa Shule ya Sekondari Mwakijombe iliyopo wilayani Mkinga Kijiji cha Mwakijombe Mkoani Tanga jana tarehe 6 Septemba, 2024v walitembelea Mahakama Kuu Tanga ilikujifunza shughuli za Mahakama. 

Wanafunzi hao wa vidato mbalimbali wakiongozwa na Mwalimu wao, Bw. Deodatus Kapulima walipokelewa na Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Tanga, Bi.Veronica George.

Baada ya kutembezwa katika idara mbalimbali za kiutawala na mashauri, wanafunzi hao walikusanyika katika ukumbi wa wazi, tayari kwa kupata maelezo kadhaa yanayohusu Mahakama kutoka kwa wawezeshaji.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Charles Matiko aliongoza kikao hicho kwa kuanza kuwapitisha wageni katika muundo wa Mahakama kwa mtindo wa maswali. Wanafunzi hao walionesha kuelewa muundo wa Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani kwa mtiririko unaostahili. 

Aidha, Mhe. Matiko alitoa maelezo ya kina kuhusu kesi za madai na kesi za jinai. Akielezea kesi za jinai, Mhe. Matiko alisema ,“Kesi za jinai zinazohusisha Jamhuri dhidi ya mtuhumiwa, ambapo kesi hizo zinapofika mahakamani, ushahidi unaanza na yule anayelalamika ambae ni Jamhuri na ikitokea ushahidi unaotolewa hauna uhusiano na kosa lililotendeka kesi hiyo itafutwa,” alieleza.

Pia Mhe. Matiko aliwaeleza wanafunzi hao kwamba zipo Mahakama zilizoanzishwa kwa ajili ya kusikiliza mashauri maalumu ambazo zinaitwa Divisheni ndani ya Mahakama Kuu.

“Zipo Mahakama zilizoanzishwa kwa ajili ya kusikiliza mashauri maalumu, kwa mfano Divisheni ya Uhujumu Uchumi, maarufu kwa jina la Mahakama ya Mafisadi, Divisheni ya kazi, Ardhi na Biashara, hizi Mahakama zinasikiliza kesi maalum kama zilivyo kwa majina yake na huwezi kupeleka kesi ya ndoa kwenye Mahakama ya Biashara,” alisema

Naye Afisa TEHAMA wa Mahakama hiyo, Bw. Mussa Mwinjuma aliwapitisha wanafunzi hao katika mfumo wa TEHAMA wa usikilizaji wa mashauri kwa njia ya runinga unaoitwa kwa lugha ya kiingereza Virtual Court.

 Akitolea maelezo ya mfumo huo, Bw. Mussa alisema, “Mfumo wa virtual court umerahisisha usikilizwaji wa mashauri na kuokoa gharama .” Akitolea mfano wa shahidi aliyeko Mwanza na kesi ipo Mahakama Kuu Tanga, hatohitajika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kutoa ushahidi na badala yake ataunganishwa kieletroniki na atatoa ushahidi wake kule alipo.

Katika Mkutano huo wa wanafunzi ambao pia ulihudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Kanda ya Tanga, Mhe. Messe Chaba ambaye alizungumzia athari za udhalilishaji wa kijinsia na masula ya ubakaji.

Akizungumzia suala hili, Mhe. Chaba alisema, “Hata mimi nina watoto kama nyinyi na huwa ninaongea nao kwa uwazi, na kizazi cha sasa mnajua mambo mengi kuliko hata wazazi wenu, hivyo nimefurahi sana kuwaona hapa kwa kuwa mtajifunza namna nzuri ya kutoa taarifa pale tatizo la ubakaji au ulawiti linapotokea.”

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe.Katarina Revocati Mteule alifunga mkutano huo wa wanafunzi kwa kuwapa nasaha kadhaa. Jaji mfawidhi aliwaambia wanafunzi hao, “Mlinzi wa afya yako ni wewe mwenyewe, ujitunze, epuka vishawishi na kutochangamana na watu usio wajua kwa kuwa unajiweka hatarini bila kujua.

Mhe. aliwashukuru waalimu kwa kuwaleta vijana hao kujua namna gani Mahakama inafanya kazi zake na kupata uelewa wa ujumla wa shughuli za kimahakama.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe Katarina Revocati Mteule (mwenye nyeusi katikati) akipata picha ya pamoja na wanafunzi waliotembelea mahakamani hapo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Messe Chaba akiendelea na utoaji elimu kwa wanafunzi waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya kujifunza shughuli za Mahakama.

Afisa Tehama, Bw. Mussa Mwinjuma akitoa elimu juu ya mifumo mbalimbali inayotumika na Mahakama katika kuendesha mashauri.

Mwezeshaji, Mhe. Charles Matiko ambaye ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, akiendelea na utoaji wa elimu juu ya shughuli za Mahakama ya Tanzania.

Waalimu na wanafunzi wakiwa katika ukumbi wa wazi wa Mahakama Kuu Tanga wakiendelea na kikao cha kujifunza shughuli mbalimbali za Mahakama.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni