- Mahakama yatunga kanuni kuruhusu polisi kuchukua maelezo kwa njia ya sauti, video
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania imetunga kanuni inayoruhusu Jeshi la Polisi kuchukua maelezo ya mshitakiwa kwa njia ya sauti na video, hatua ambayo itasaidia kuongeza uwazi na uharakishaji wa usikilizaji wa mashauri.
Hayo yamebainishwa tarehe 31 Oktoba, 2024 na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari kwenye mkutano wa kila mwezi na vyombo vya habari.
Katika Mkutano huo uliofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro, Mhe. Kamugisha alizungumzia mchango wa maboresho ya kanuni za Mahakama katika upatikanaji wa haki kwa wakati.
Kabla ya kutungwa kwa kanuni hiyo, Tangazo la Serikali No. 792/2023, Jeshi la Polisi limekuwa likichukua maelezo ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai kwa njia ya kuandika kwa mkono, ambayo yamekuwa yakikataliwa mara kwa mara wakati wa kuwasilishwa mahakamani, hivyo kuchangia ucheleweshaji.
“Sisi wote ni mashahidi, kuna vilio vingi vya wananchi. Wanasema haya maelezo siyo ya kwangu, nilipigwa na polisi, nililazimishwa kuyatoa. Kwa hiyo, kanuni hii itasaidia kuondoa malalamiko kama haya,” amesema
Mhe. Kamugisha amebainisha pia kuwa kitendo cha mshitakiwa kukana maelezo aliyoandika akiwa kwenye kituo cha polisi kumekuwa kukichangia ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri husika.
“Mtuhumiwa akishasema kuwa maelezo aliyoyatoa polisi siyo yake, inabidi Mahakama iache shauri mama na kuanza kusikiliza shauri dogo ili kujiridhisha kama kweli mshitakiwa alitoa maelezo kwa ridhaa yake…
…Muda mwingi umekuwa ukipotea, mfano ukiwa na kesi moja yenye washitakiwa 10, halafu kila mmoja anakana maelezo yake, hii inasababisha shauri kuchukua muda mrefu zaidi kusikilizwa,” amesema.
Mhe. Kamugisha ameeleza kuwa kanuni za uchukuaji wa maelezo ya mtuhumiwa kwa njia ya video na sauti zitaongeza uwazi na kupunguza mapingamizi dhidi ya kupokelewa kwa maelezo ya mshtakiwa kwa sababu ya kuchuliwa kwa vitisho au mateso.
Mkurugenzi huyo amewatoa wasiwasi wananchi kwamba tahadhari kubwa imechukuliwa kikanuni ili kusiwepo na udanganyifu wa aina yoyote, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba wa kuunganisha matukio yanayoleta taswila tofauti na uhalisia.
“Kanuni zinabainisha taratibu za kuanza kuchukua maelezo, zinaeleza chumba kiwe namna gani, mpangilio wa chumba uweje na uonekano wa mshitakiwa au yule anayehojiwa uwe wa namna gani. Wakati wa kunukuu maelezo, lazima awepo shahidi huru ambaye atashuhudia zoezi hilo,” amebainisha.
Hivi karibuni, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema Mahakama ya Tanzania inakusudia kujenga Studio Maalum zitakazotumika kuchukua maelezo na picha za washitakiwa baada ya kutuhumiwa kutenda makosa ya kijinai.
Akizungumza wakati anafunga Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, Mhe. Prof. Juma alibainisha kuwa hatua hiyo itapunguza malalamiko ya ya kubambikiwa kesi au mtu kusema alilazimishwa kutoa maelezo hayo na Polisi.
Jaji Mkuu alieleza kuwa matarajiao ya ujenzi wa Studio hizo unafuata baada ya Kamati ya Kanuni ya Mahakama ya Tanzania inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye kutunga kanuni inayoitwa, “Audio and Video Recording of Police Interview of Suspects.”
Alieleza kuwa Kanuni hiyo inaainisha kuwa badala ya Polisi kuwahoji na kuandika maelezo ya Watuhumiwa kwenye vituo vya Polisi, kuwe na Studio Maalum ambazo zitatumika kuchukua yale yanayotokea na kuchukua picha.
“Hatua hii itapunguza malalamiko ya wananchi ya kubambikiwa kesi au kusema maelezo yangu nililazimishwa kuyatoa,” Mhe. Prof. Juma alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni