Jumapili, 13 Oktoba 2024

JAJI MKWIZU: UKARIMU WA HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI WA KIMATAIFA

Na MAGRETH KINABO- Mahakama

 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam maarufu kwa jina la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu amesema Mahakama hiyo imefurahishwa na huduma za kiwango cha kimataifa zitolewazo na viongozi, wakiwemo watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,huku akiahidi kuendeleza ushirikiano uliopo.

 

Hayo yamesemwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, jana tarehe 12 Septemba, 2024 wakati wa ziara ya siku mbili ya kutembelea hifadhi hiyo, iliyoko Mkoa wa Morogoro.

 

“Tumefurahishwa na hadhi mliyotupa wana Mahakama, tangu tulipowasili kuanzia mapokezi na huduma mlizotupatia, tumesikia kupendwa tutawatangaza kuwa ninyi ni wahifadhi wa wanyama na watu.Hifadhi hii ni ya mfano na ukarimu wenu ni Kiafrika wa kiwango cha kimataifa…

 

“Sisi tutaendelea kuwa mabalozi wa hifadhi hii na tutawaeleza wenzetu wana familia wa Mahakama kuwa wana wajibu wa kutembelea Hifadhi za Taifa mfano ya Mikumi ili kuweza kuona vivutio mbalimbali,” amesema          Mhe.Jaji Mkwizu.

 

Aidha Mhe. Jaji Mkwizu ameongeza majaji na watumishi wa Mahakama hiyo, wamefurahishwa na  Huduma kwa Mteja itolewayo hifadhini humo ambayo imeanzia kwa viongozi, wahifadhi, wahudumu na hata kwa wanyama, ambapo ameushukuru uongozi na watumishi wote wa Kanda ya Mashariki, wakiwemo wa Hifadhi ya  Taifa ya Mikumi kwa kitendo hicho.

 

Hata hivyo Kaimu Jaji Mfawidhi huyo, ameongeza kwamba Mahakama hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na uongozi wa hifadhi hiyo, huku akiwakaribisha kutembelea Mahakama ya Tanzania ili waweze kufahamu shughuli za Mahakama.

 

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki John Nyamhanga, Kanda hiyo inayohusisha hifadhi za Udzungwa, Mwl., Nyerere, Saadani na Mikumi, amesema wamefarijika kutembelewa na Majaji, viongozi na watumishi wa Mahakama hiyo, kwa kuwa wameweza kubadilishana mawazo na kuongeza kuwa kuna hifadhi 21, lakini Mahakama hiyo imechagua Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

 

“Tunashukuru kwa kutenga muda wenu kwa ajili ya kutembelea hifadhi hii, pia tunashukuru  kuwa majaji wote kuanzia sasa wamekubali kuwa wahifadhi, na mimi niwaongezee cheo sio wahifadhi waandamizi ni wahifadhi wakuu, hivyo mtaiwasilisha nchi yetu kuisemea kwenye shughuli za uhifadhi na utalii na mali asili zetu, kwani uhifadhi sasa umetapakaa kwenye mhimili wa Mahakama, mhimili huu muhimu wa haki, mtauwambia umma kuwa tumerithishwa tuwarithishe,” amesema Kamshina huyo.

 

Naye Mhifadhi Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki, Apaikunda Mungure akitoa neno kwa niaba ya Menejimenti ya Kanda na Mikumi ameiomba Mahakama kuendelea kutembelea hifadhi nyingine kwa kuwa kila hifadhi ina upekee wake.

 

Amesema kuwa vivutio vingine kama vile mali kale, makumbusho ya Mwalimu Nyerere, utalii wa kupanda milima, makumbusho ya utumwa na utalii wa bahari.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam wakipata kifungua kinywa kabla ya kuanza shughuli za kitalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, iliyoko Mkoa wa Morogoro.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, viongozi na watumishi wengine wakiwa katika picha ya pamoja kabla kuingia kwenye magari maalumu kwa ajili ya shughuli za kitalii.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es  Salaam, Mhe.Elizabeth Mkwizu(aliyevaa kofia na kilemba) akiwa tayari kwenye gari maalumu la kitalii kwa ajili ya kuwaongoza majaji wenzake, wakiwemo watumishi wa Mahakama hiyo kutalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Majaji wakiwa kwenye gari maalumu.
Watumishi wa Mahakama hiyo wakiwa katika sare ya kutalii hifadhi hiyo.

Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu(aliyenyoosha mkono) akifurahia jambo mara baada ya kutalii kwenye hifadhi hiyo.

Tembo wakiwa wanakunywa maji katika bwawa lilipo katika hifadhi hiyo. 

         Swala wakiwa katika hifadhi hiyo.

Pundamilia  wakiwa hifadhini.

Twiga wakiwa hifadhini.

Mamba wakiwa katika bwawa.

 Viboko wakiwa katika bwawa.

 Dereva wa gari maalumu la kitalii, Bw. Method Mrema(aliyevaa shati na kofia) akiwaelezea majaji kuhusu tabia za viboko na mamba.

Watumishi wakiwaangalia wanyama hao.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu(wa kwanza ) akiwaongoza majaji wenzake huku akifurahia kupata chakula cha mchana kijulikanacho kwa jina la ‘bush lunch’ kwenye kivuli cha moja ya mti ulipo katika hifadhi hiyo.
Majaji na watumishi wa Mahakama hiyo wakipata chakula.


Majaji wakila chakula kwenye kivuli cha mti mojawapo uliopo hifadhini humo.

 

Watumishi wakila chakula kwenye kivuli cha mti huo.


Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki John Nyamhanga, Kanda hiyo inayohusisha hifadhi za Udzungwa, Mwl.Nyerere, Saadani na Mikumi, akizungumza jambo wakati wa ziara hiyo.

Mhifadhi Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki, Apaikunda Mungure akitoa neno kwa niaba ya Menejimenti ya Kanda na Mikumi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Elizabeth Mkwizu akitoa neno la shukurani.

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni