- Studio maalum za kuchulia maelezo ya watuhumiwa kujengwa
- Hatua hiyo mwarobaini wa malalamiko watu kubambikiwa kesi
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama ya Tanzania, kupitia Kitengo cha Maboresho, inakusudia kujenga Studio Maalum zitakazotumika kuchukua maelezo na picha za washitakiwa baada ya kutuhumiwa kutenda makosa ya kijinai.
Akizungumza wakati anafunga Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania leo tarehe 11 Oktoba, 2024 katika Hoteli ya Mount Meru jijini hapa, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa hatua hiyo itapunguza malalamiko ya ya kubambikiwa kesi au mtu kusema alilazimishwa kutoa maelezo hayo na Polisi.
“Sasa, ili kuwasaidia Polisi kwenye hili, Kitengo cha Maboresho kinafikiria kutayarisha baadhi ya Studio Maalum zitakazokuwa sehemu ambazo maelezo ya washitakiwa yatachukuliwa pamoja na picha zao badala ya kutegemea yale maelezo yaandikwa kwa mkono wa Polisi,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa matarajiao ya ujenzi wa Studio hizo unafuata baada ya Kamati ya Kanuni ya Mahakama ya Tanzania inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye kutunga kanuni inayoitwa, “Audio and Video Recording of Police Interview of Suspects.”
Ameeleza kuwa Kanuni hiyo inaainisha kuwa badala ya Polisi kuwahoji na kuandika maelezo ya Watuhumiwa kwenye vituo vya Polisi, kuwe na Studio Maalum ambazo zitatumika kuchukua yale yanayotokea na kuchukua picha.
“Hatua hii itapunguza malalamiko ya wananchi ya kubambikiwa kesi au kusema maelezo yangu nililazimishwa kuyatoa. Haya ni baadhi ya maeneo ya maboresho ambayo yanaonesha ni kwa kiasi gani Kamati ya Kanuni imesaidia,” Mhe. Prof. Juma amesema.
Jaji Mkuu amefafanua kuwa baada ya kutayarisha Mpango Mkakati wa Mahakama Awamu ya Kwanza, Mahakama ya Tanzania ilijenga hoja kwa Serikali itafute fedha za kuutekeleza na kuwezesha kufanyika kwa maboresho mbalimbali.
“Moja ya eneo ambalo lilionekana kuhitaji maboresho ni la Sheria na Kanuni ambazo zilioneka kuwa zimepitwa na mabadiliko ya Dunia na haziwezi kubeba maboresho ya kuweka mazingira ya utawala bora, utawala wa sheria, mazingira bora ya biashara na mazingira ya uwekezaji,” amesema.
Mathalan, amesema, ili ijilinganishe na Mahakama zilizokuwa zikipendwa na wafanyabiashara na wawekezaji, kwa mfano Singapore, Mahakama ya Tanzania ilitakiwa kupunguza hatua nyingi ambazo mashauri hupitia, ili kuleta urahisi wa kufanya biashara.
Jaji Mkuu wa Tanzania, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo, amebainisha kuwa maboresho ya sheria yalipewa uzito na kutengewa fedha za mradi kwa malengo ya kuiwezesha Kamati kutekeleza wajibu wake.
“Katika kipindi cha Programu za Maboresho, jumla ya Kanuni zilizotayarishwa na kupendekezwa kwa Jaji Mkuu na Kamati ya Kanuni ni kati ya 60 hadi 70, hii ni kuanzia mwaka 2013,” amesema.
Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa Kamati ya Kanuni ni jicho la Mahakama kama mtumiaji na mtekekezaji sheria.
Amesema kwamba, katika shughuli zake za kila siku, Mahakama inapokutana na Sheria ya Bunge ambayo ni kikwazo kwa maboresho, Kamati ya Kanuni hutayarisha Andiko lenye hoja na mapendekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aifikishe kwenye Wizara husika itayarishe Rasimu ya Mswada wa kutunga Sheria Mpya au kubadili Sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni