Alhamisi, 12 Desemba 2024

JAJI NDUNGURU AWATAKA WAJUMBE WA KAMATI ZA MAADILI KUZINGATIA VIAPO VYAO

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Iringa

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Ndunguru amewataka wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Iringa kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao ya kusimamia nidhamu na maadili ya Mahakimu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Iringa leo tarehe 11 Disemba, 2024 mjini humo, Jaji Ndunguru amewataka wajumbe hao kukumbuka viapo vyao kila wanapotekeleza majukumu yao ya kamati.

”Kiapo kiendane na utendaji wenu wa kazi, tekelezeni viapo vyenu mlivyoapa leo. Pale unapopewa dhamana katika kazi ya jamii ni lazima kuapa ili kila unapotekeleza jukumu ulilopewa ukumbuke kiapo na kukizingatia”, alisema.  

Wajumbe wa Kamati walioapishwa leo ni pamoja na Mkuu wa wilaya ya Iringa Bw.  Kheri James (Mwenyekiti), Katibu Tawala wa wilaya ya Iringa-DAS Bw. Michael Semindu (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa na wajumbe wengine wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya.

Aliwataka wajumbe hao kumtanguliza Mungu, kuwa makini na kuzingatia maadili  wanapotekeleza majukumu yao kwa kuwa Kamati hizo hushughulikia mashauri ya nidhamu ambayo yanagusa maisha ya Watumishi hususan Mahakimu.

Jaji Mfawidhi pia alitoa wito kwa wajumbe wa Kamati kuhakikisha wanafanya kazi pasipo kumuonea wala kumpendelea Mtumishi yoyote. Aidha aliwashauri kuwalea Mahakimu, kujenga utamaduni wa kuwapongeza wanapofanya vizuri na  kuwaonya wanapoenda kinyume.

”Kamati za Maadili zina umuhimu kwa kuwa zinasaidia Mahakimu kufanya kazi kwa uadilifu, zinafanya kazi ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa zimekasimiwa jukumu hilo kisheria na Tume”, alisema Jaji Ndunguru.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Kheri James akizungumza mara baada ya kuapishwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliahidi ushirikiano katika kutimiza majukumu ya kamati ili haki itendeke.

Alisema Wilaya ya Iringa inaongozwa na mambo matano ambayo ni Utawala bora, haki, usawa, maendeleo na umoja na mshikamano. Alisema mambo haya yakizingatiwa Kamati itatekeleza vema wajibu wake.

”Tutaendelea kuwa wa mfano katika kufanya vikao vilivyowekwa kisheria ili Mahakama na watumishi wake waone kuwa kamati hii iko kwa ajili ya kuisadia Mahakama kutimiza malengo yake”, alisema.  

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

 

Mkuu wa wilaya ya Iringa Bw.  Kheri James akiapa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Ndunguru kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Iringa leo tarehe 11 Disemba, 2024 mjini humo. 

Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Iringa wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa leo tarehe 11 Disemba, 2024 mjini humo.  
Katibu Tawala wa wilaya ya Iringa (DAS) Bw. Michael Semindu akiapa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Ndunguru kuwa Katibu wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Iringa leo tarehe 11 Disemba, 2024 mjini humo.  


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa Mhe. Ritha Protas Ruta akiapa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Dunstan Ndunguru kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Iringa leo tarehe 11 Disemba, 2024 mjini humo.  

Sehemu ya Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye hafla ya kuapisha Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Iringa. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni