Jumatano, 4 Desemba 2024

MKURUGENZI MTENDAJI CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA ASHAURI UOANISHAJI SHERIA ZA KAZI, AJIRA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania, Bi.  Suzanne Ndomba-Doran ameziomba nchi za Afrika Mashariki kuangalia uwezekano wa kuoanisha sheria zinazohusu sekta ya ajira na kazi ili kuwa na uelewa wa pamoja katika utatuzi wa migogoro ya kazi katika ukanda huo.

Bi. Ndomba-Doran ametoa wito huo leo tarehe 4 Desemba, 2024 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Uoanishaji Sheria za Kazi Afrika Mashariki ili Kuboresha Utatuzi wa Migogoro kwenye siku ya nne ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki unaofanyika jijini hapa.

“Kama nchi zote tunajadiliana suala zima la Umoja wa Afrika Mashariki na maeneo mengine machache ambayo tayari yanajadiliwa, nafikiri hata hili linawezekana. Jinsi gani litafanyika ni suala la majadiliano zaidi namna ya kuangalia. Tunaweza tusikubaliane katika maeneo yote kwa sababu nchi hizi zinatofautiana, lakini pia kuna maeneo ambayo tunaweza kukubaliana,” amesema.

Amebainisha kuwa ukiangalia katika sheria za kazi zilizopo unaweza kuona kuna maeneo ambayo hakuna utofauti kubwa, mfano vipengele vinavyohusu likizo za uzazi na hiyo inatokana na nchi hizo kuridhia mikataba fulani ya Shilika la Kazi Duniani.

“Zoezi hili la uoanishaji wa sheria za kazi lina faida. Kama tunazungumzia ulinganifu na kama watu wanatoka sehemu moja kwenda nyingine, mfano suala la uhamishaji wa mafao, kila nchi ina utaratibu wake wa kulipa mafao. Sheria za Tanzania zinaruhusu raia wa nje akimaliza muda wake anaweza kutoa yale mafao…

“Lakini labda tunaweza kuwa na mikataba ambayo inaruhusu kwamba yale mafao yake yanaweza kusomeka katika nchi yake, lakini sheria za nchi zote lazima ziangalie jinsi gani mafao yale yanaweza kusomeka ili kuhakikisha ule mustakabali mzima wa pensheni uweze kuwa na uhalisia,” Mkurugenzi huyo amesema.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Majaji tayari wameshaanza kuangalia sheria za nchi zingine zinafanyaje na wamezitumia katikakuamua mashauri. Ametoa mfano wa mashauri kadhaa yaliyoshughulikiwa na Mahakama ya Rufani Tanzania, ikiwemo ya CCBRT Hospital dhidi ya Daniel Celestine Kivumbi na ile ya Standard Chartered Bank Ltd dhidi ya Justin Teneishemo.

Kadhalika, Bi. Ndomba-Doran amemnukuu Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Kenya, Mhe. Mhe. Dkt. Priscah Wamucii Nyotah, ambaye alizungumzia kuhusu umri wa mtoto wa kufanya kazi. “Kwenye hili kulioanisha ni ngumu? Kwa sababu kuoanisha inaweza ikawa siyo kuwa na sheria moja, lakini mkakubaliana kwenye kifungu kinachohusiana na masuala hayo,” amesema.

Kabla ya kuhitimisha mada yake, aliwaeleza washiriki namna utendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi inavyosaidia na pia jukwaa la utatu linalofanywa na Mahakama kuwaalika waajiri na wafanyakazi kwa pamoja kujadili masuala mbalimbali, changamoto na kuangalia maeneo ya kuboresha zaidi.

Baada ya uwasilishaji wa mada hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kenya, Mhe. Jemimah Keli aliongoza mjadala uliochangiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Linda Lilian Tumusiime Mugisha na Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Kenya, Mhe. Dkt. Priscah Wamucii Nyotah kabla ya kuruhusu washiriki wa Mkutano huo kuuliza maswali.

Mkutano huo unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 380 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar, Burundi na Sudani ya Kusini na mada mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa zikilenga kuboresha huduma ya utoaji haki katika nchi za Ukanda huo.

Kaulimbiu ya Mkutano huo inasema; ‘Uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa ajili ya kuimarisha utengamano na Ukuzaji Uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.’ 

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania, Bi.  Suzanne Ndomba-Doran (juu na chini) akiwasilisha mada kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki unaofanyika jijini Arusha.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa na Viongozi wengine wakifuatilia uwasilishaji wa mada hiyo. 

Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki (juu na chini) wakifuatilia uwasilishaji wa mada hiyo.


Sehemu nyingine ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki (juu na picha mbili chini) wakifuatilia uwasilishaji wa mada hiyo.



Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania, Bi.  Suzanne Ndomba-Doran (kulia) akiwa kwenye Mkutano huo baada ya kuwasilisha mada yake. Picha chini akipokea zawadi kutoka kwa Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu kutoka Nchi za Afrika Mashariki, Mhe. John EudesKeitirima.



 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni