Alhamisi, 5 Desemba 2024

MTENDAJI MKUU MAHAKAMA ATEMBELEA MAHAKAMA ZA MWANZO PAHI NA BUSI


Na ARAPHA RUSHEKE - Mahakama Kondoa 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.Elisante Ole Gabriel  ametembelea Mahakama za Mwanzo Pahi na Busi zilizopo Wilaya ya Kondoa jijini Dodoma, ikiwa  ni lengo  la kuona hali halisi ya mazingira na kazi lakini pamoja na kutambua mafanikio na changamoto zinazo kabili Mahakama hizo.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama hizo tarehe 4 Desemba, 2024, Prof.Ole Gabriel alisema kuwa amezitembelea ili kufahamu nini kinaendelea katika Mahakama za Mwanzo  hizo ukizingatia asilimia kubwa ya mashauri ambayo yapo mahakamani  katika Nchi yetu yanaanzia katika Mahakama za Mwanzo.

Aidha alisema amefika mahakama hizo ili kuwaona na kuwapongeza watumishi waliopo  kwani licha yakuwa mazingira wanayofanyia kazi kuwa na changamoto lakini hawakuacha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa  sana.

“Leo tarehe 4 Desemba, 2024 nimefurahi sana kufika katika Mahakama hizi Pahi na Busi nachukua fursa hii kumshukuru Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania        Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, ambaye nilimpomtembelea ofisini kwake wiki mbili zilizopita alinihihamasisha kwamba kuna mahakama mbili muhimu nifike kuzitembelea  ambazo ni Pahi ambayo ina miaka 78 na Busi  yenye miaka 92 kwa hiyo nifaraja kubwa sana kwangu leo kwanza nimeweza kufika katika majengo haya  muhimu ya kihistoria,” alisema Prof. Ole Gabriel.

Aliwashukuru watumishi wanayoyatunza  majengo hayo, huku akitaka   utamaduni wa kutembelea Mahakama za Mwanzo mara kwamara ambazo zipo pembezoni ambazo zinadhaniwa zimesahaulika uendelee ili kupata picha halisi. 

“Nadhani tukiwa tunakuja mara kwa mara tutapata picha halisi, leo nimejionea barabara ambayo inapita katikati ya mto maana yake ni kwamba watumishi hawa wakati wa mafuruko wao wanakuwa wamefungiwa hawawezi kutoka, lakini wanendelea na kazi na hii inanifanya nithamini na niguswe zaidi na maneno aliyosema Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.Ibrahim Hamis Juma mnamo tarehe 30 Novemba, 2024 tulipokuwa katika Chuo cha   Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto…

“Aliposema kwamba hakika anawapongeza na Majaji kwa kufanya kazi iliyotukuka kwa kuwatumikia wananchi kwa mazingira yeyote na ndio maana sio vyema kubeza au kuzalilisha kazi hii inayofanywa kwa sababu wapo watu wanaoishi katika mazingira kama haya magumu kabisa lakini bado wanachapa kazi,” alisisitiza Prof .Ole Gabriel.

Prof. Ole Gabriel aliwaomba  watumishi  wa mahakama hizo wapokee salaam nyingi  za dhati kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma vivyohivyo Jaji Kiongozi  wa Mahakama         Kuu ya Tanzania, Mhe, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani naye anawasalimia.

Aidha  aliwaahidi kwamba Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, itaendelea kushiriakiana na nyinyi kwa kuwa wanajivunia  kuwa na nanyi sababu Mahakama za Mwanzo ndio msingi wa nyumba. Hivyo  wanathamini kazi zenu pia watambue kwamba hatutakumbukwa kwa sababu ya vyeo vyetu  tutakumbukwa na jamii kwa mchango yetu mizuri tuliyoifanya katika jamii.

  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.Elisante  Ole Gabriel (wa kwanza kushoto ) akisalimiana na mtumishi Maulidi Ally Mwiru (Mlinzi Mkuu wa Mahakama Mwanzo  Pahi) mara baada ya kuwasili katika Mahakama hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel  akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Pahi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Pahi.

  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel  akisaini kitabu cha wageni katika Mahakama ya Mwanzo Busi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na Diwani wa Kata ya  Busi Bi. Madina Athumani.

 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel akiwa anakagua jengo la zamani la Mahakama ya Mwanzo Busi ambalo lilijengwa miaka 92 iliyopita kipindi cha ukoloni.

     Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.Elisante Ole Gabriel  katikati)akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama (kulia kwake) ni Mhe .Upendo Ngitiri Naibu Msajili Mahakama Kuu Dodoma anayefuatia ni Afisa Tawala Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya Kondoa,  Bi,Edna Dushi  (wa pili kutoka kushoto)  ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Pahi, Mhe.Shungu Selemani Shungu alipombelea Mahakama ya Mwanzo Busi anayefuatia ni Mlinzi Mkuu Mahakama ya Mwanzo Busi, Bw.Chundu Hassan Chundu.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni