Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Umoja wa Wanasheria Wanawake Shinyanga (Shinyanga Women Lawyers) wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ,Mhe. Ruth Massam, walitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kutoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi za kitanzania Milioni nne kwa ajili ya kuwafariji na kuwasaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) pamoja na wakina mama.
Timu hiyo inayojumuisha Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu, Wanasheria wa Serikali na wa Kujitegemea walifika katika Hospitali hiyo jana 11 Desemba, 2024 kwa kutambua mazingira wanaozaliwa na kukulia watoto hao wanaozaliwa kabla ya wakati.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Ruth Massam alisema, “tumetembelea Hospitali yetu ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuwasaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) pamoja na kuangalia maendeleo ya ukuaji wao baada ya kuzaliwa katika hali hiyo.’’
Mhe. Massam alisema kuwa wametoa msaada wa vifaa hivyo kwa lengo pia la kumshukuru Mwenyezi Mungu kuelekea kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025.
Aidha, Jaji Massam, amewaomba wadau mbalimbali yakiwemo Mashirika, Taasisi za Kiserikali pamoja na watu binafsi kuendelea kujitoa kuwatembelea, kuwasaidia na kuwafariji Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Akipokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Lizila John alitoa shukrani za dhati pamoja na kuwapongeza Wanasheria hao Wanawake wa Mkoa huo kwa kufika katika hospitali hiyo na kutoa vifaa vitakavyowasaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na akina mama.
Dkt. John aliwaomba kuendelea kuwa na moyo huo wa kipekee kwa kuwakumbuka na kuwasaidia Watoto wanaozaliwa katika hali hiyo.
Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa na Wanasheria hao ni pamoja na mashine za kusaidia kupumua, khanga, shuka pamoja na vifaa vingine vitakavyowasaidia katika maendeleo ya ukuaji wao.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Ruth Massam (kulia) akimkabidhi Dkt. Luzila John mashine ya kusaidia kupumua watoto njiti wanaozaliwa katika Hospitali hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni