- Mahakama ya Tanzania yawapeleka wajumbe mkutano wa kimataifa kujionea utajiri Tanzania
- Wao wasema huu ni ukarimu uliopitiliza
Na
FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha
Wajumbe
takribani 380 wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Chama cha Mahakimu na Majaji
kutoka Afrika Mashariki (EAMJA) leo tarehe 6 Desemba, 2024 wametemelea Hifadhi
ya Ngorongoro mkoani Arusha, kujionea maajabu ya dunia na utajiri ambao
Tanzania inajivunia.
Ziara hiyo iliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kama sehemu ya Mkutano huo imekonga nyoyo za wajumbe mbalimbali wa Mahakama kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar na Burundi ambao wameahidi kurudi tena Tanzania kama watalii binafsi ili kujionea maajabu zaidi.
"Haya yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania ni ukarimu uliopitiliza. Tumefurahishwa sana na ziara hii ya kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro. Tumefurahiya sana, kila kitu kilikuwa kizuri. Ni kweli tumejionea maajabu. Tulikuwa tunatamani tuendelee kuwepo Arusha, lakini hatuna namna lazima tuondoke," amesema Mhe. Cobrand Ob Oroya, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Mahakama ya Uganda.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya, Divisheni ya Kazi, Mhe. Jemimah Keli ameeleza kuwa wamefirahia ukarimu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, wamejifunza mengi wakati wa Mkutano, wametengeneza marafiki na wamefurahishwa na ziara ya kwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro na wangependa kurudi tena Arusha kwa safari zao binafsi kujionea utajiri uliopo.
Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania, ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. John Kahyoza amesema wageni wa Mkutano huo wameelezea kufurahishwa na matayarisho na mapokezi waliyoyapata na kila kitu kilienda vizuri tangu siku ya kwanza.
Safari kuelelea katika Hifadhi hiyo ilianza mapema asubuhi saa 12.30 katika Viwanja vya Magereza Kisongo na msafara wa wajumbe hao ulipokelewa na Viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi katika lango kuu la kuingilia hifadhini.
Wakiwa katika Hifadhi hiyo, Mahakimu na Majaji kutoka nchi hizo pamoja na wageni wengine mbalimbali wamejionea utajiri wa wanyama pori na misitu ya kupendeza.
Wajumbe hao wamefanikiwa kuwaona baadhi ya wanyama maarufu duniani wanaofahamika kama Big-5 wanaopatikana kwa urahisi katika Hifadhi hiyo kama Tembo, Simba, Nyati na Faru. Chui, ambaye ni miongoni mwa Wanyama hao maarufu hakuweza kuonekana. Kwa kawaida, Twiga hapatikani katika Hifadhi hiyo kutokana na umbo lake.
Kadhalika, Mahakimu na Majaji hao pamoja na wageni wengine wamefanikiwa kuwaona wanyama wengine kama swala, pundamilia, mbuni, nyani, fisi, Kiboko na ndege wa aina mablimbali wakiwemo Filamingo na Korongo.
Viongozi hao wameonesha kufurahishwa na utalii huo na wamefarijika kujionea kwa macho wanyama wanaowaona kwa picha kwenye vitabu na runinga. Wameahidi kuja tena Tanzania kwa ajili ya kufanya shughuli za utalii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni