Na Innocent Kansha - Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Mkoa wa Dar es Salaam na
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam,
Mhe. David Patrick Ngunyale amewaasa watumishi kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma bora kwa wananchi wanaofika mahakamani kupata huduma mbalimbali ili
kuendelea kujenga imani ya wananchi katika huduma zitolewazo na Mahakama kwani
ndiyo walengwa wa huduma hizo.
Akifungua mafunzo kwa watumishi wote wa Mahakama wa kada
mbalimbali wa Mahakama ya Wilaya Ilala na Mahakama zake za Mwanzo yaliyofanyika
Mahakama hapo hivi karibuni, Mhe. Ngunyale aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa,
huduma na maadili bora huanzia ngazi ya familia, iwapo upendo na amani
vitajengwa kutoka ngazi ya familia ni rahisi kuhudumia wateja kwa upendo wawapo
eneo la kazi.
Aidha, Mhe. Ngunyale aliwambia washiriki mafunzo hayo ya
ndani yana lengo la kuwajengea uwezo katika kuboresha ufanisi wa kazi na kutoa
huduma bora zinazoridhisha wateja ili kuendelea kuimarisha imani ya wananchi
kwa huduma zinazotolewa na Mahakama.
“Ni rai yangu kwenu washiriki wote wa mafunzo haya
tutakayojengewa uwezo kuyaishi mafunzo haya katika kuboresha huduma zaidi kwa
wateja na maisha yao binafsi. Vilevile niwashauri kutenga muda wenu kuhudumia familia
na kushirikiana na jamii inayowazunguka kwani hamuishi kisiwani,” aliongeza
Mhe. Ngunyale
Naye, Afisa TEHAMA kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dar
es salaam Bw. Tumaini Malima akitoa mada juu ya matumizi sahihi ya mifumo ya kuratibu
mashauri alisisitiza kwamba, watumiaji wote wa mifumo hiyo wakiwemo Mahakimu na
Watunza Kumbukumbu waendelee kuitumia na kuendelea kujifunza ili kuifahamu
zaidi inavyofanya kazi.
“Mtaendelea kupokea maboresho mbalimbali yanayohusu
mifumo hii ya kuratibu shughuli mbalimbali za kimahakama ili kila mmoja wetu aweze
kutoa huduma stahiki na kufikia malengo na matokeo tarajiwa,” alisema Afisa
huyo.
Mada zilizowasilishwa katika mafunzo ni pamoja na
Huduma kwa Wateja, Maadili ya Watumishi, Afya ya Akili na Matumizi ya Mifumo Mbalimbli
ya Mahakama ikiwemo mifumo ya kuratibu mashauri (e-Case Management System) pamoja na Mfumo wa tathmin wa taarifa za
watumishi (Ess).
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo walipongeza juhudi
za Mahakama na kutoa maoni mbalimbali wakifurahishwa na mafunzo hayo wakisema
yamewaongezea uelewa kimaisha kuanzia ngazi ya familia na utoaji huduma bora
maeneo ya kazi. Wakaomba mafunzo ya aina hiyo yaendelee kutolewa mara kwa mara
ili kuzidi kuboresha utendaji kazi wao.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya
Ilala Mhe. Janeth Boaz Kinyage aliwashukuru wawezeshaji wote kwa kuonyesha
upendo na kutenga muda wao kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo ambayo yataleta
mwamko chanya katika utoaji huduma za kimahakama na mahusiano ya kijamii ndani
na nje ya Mahakama.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha watumishi wa ngazi
mabalimbali wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala na Mahakama zake tano (5) za Mwanzo
ikiwa ni pamoja na Kariakoo, Ilala, Buguruni, Ukonga na Chanika, na watumishi
wa kada mbalimbali wakiwemo Mahakimu, Wahasibu, Wasaidizi wa Kumbukumbu,
Waandishi Waendesha Ofisi, Wahudumu wa ofisi na Walinzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Mkoa wa Dar es Salaam na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Patrick Ngunyale (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Wilaya ya Ilala na Mahakama zake za Mwanzo mara baada ya kufungua mafunzo kwa watumishi hao. Wengine walioketi ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala Mhe. Janeth Boaz Kinyage (kulia) na kushoto ni Hakimu Mkazi Mhe. Rehema Lyana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo Mkoa wa Dar es Salaam na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Patrick Ngunyale (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala na Mahakama zake za Mwanzo mara baada ya kufungua mafunzo kwa watumishi hao. Wengine walioketi ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ilala Mhe. Janeth Boaz Kinyage (kulia) na kushoto ni Hakimu Mkazi Mhe. Rehema Lyana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni