Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo tarehe 03 Desemba, 2024 amefungua Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) uliowaleta pamoja zaidi ya washiriki 380 ili kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma ya utoaji haki katika Ukanda huo.
Mhe. Majaliwa amefungua Mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Shamrashamra za hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo zilianza kuanzia saa 2 asubuhi kwa burudani ya ngoma ya asili, washiriki na wageni mbalimbali wa Mkutano huo walianza kuwasili katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Gran Melia` ambapo mkutano huo unafanyikia.
Mgeni Rasmi aliwasili katika viwanja vya Hoteli hiyo majira ya saa 4 asubuhi na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Viongozi wengine waliompokea Waziri Mkuu ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ignas Kitusi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.
Mara baada ya kuwasili, Mgeni rasmi alipokelewa na kupumzika kwa muda mfupi chumba cha wageni maalum katika Hoteli ya Gran Melia` na baadaye kuingia ukumbini kwa ajili ya kutekeleza jukumu la kufungungua rasmi Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA).
Hotuba mbalimbali zilitolewa katika hafla hiyo, ambapo hotuba ya kwanza ilitolewa na Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA), Mhe. John Eudes Keitirima akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda.
Baadaye, Waziri wa Katiba na Sheria alipanda jukwaani kuzungumza kwenye hafla hiyo na baadaye kufuatiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye, baada ya kutoa hotuba yake, alimkaribisha Waziri Mkuu kufungua rasmi Mkutano huo.
Katika hafla hiyo ufunguzi, Waziri Mkuu alikabidhiwa zawadi maalum na Jaji Mkuu kama shukrani kwa kukubali kumuwakilisha Rais kufungua Mkutano huo.
Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar, Burundi na Sudani ya Kusini na mada mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa zikilenga kuboresha huduma ya utoaji haki katika nchi za Ukanda huo.
Kaulimbiu ya Mkutano huo inasema; ‘Uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa ajili ya kuimarisha utengamano na Ukuzaji Uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.’
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akishuka kwenye gari alipowasili katika hoteli ya Gran Melia`jijini Arusha kwa ajili ya kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) leo tarehe 03 Desemba, 2024.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (mwenye suti ya bluu) akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) alipowasili katika Hoteli ya Gran Melia` kwa ajili ya kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama na Serikali wakielekea ukumbini kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) leo tarehe 03 Desemba, 2024 katika hoteli ya Gran Melia` jijini Arusha.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo leo tarehe 03 Desemba, 2024 katika Hoteli ya Gran Melia` jijini Arusha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni