Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma.
Maadhimisho
ya Wiki ya Sheria kitaifa yanayofanyika jijini Dodoma yaingia siku ya tatu
tangu kuzinduliwa rasmi tarehe 25 Januari, 2025 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yameshika
kasi baada ya Mahakama ya Tanzania kuzindua rasmi programu maalum ya kutoa
Elimu ya Sheria na kujibu hoja za wananchi kwenye maeneo mbalimbali yenye
mkusanyiko wa Umma kwa vitendo.
Katika
kuhakikisha Mahakama inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia programu hiyo
maalum ya utoaji elimu mtaani leo tarehe 27 January, 2024 Maafisa Mahakama
walishiriki kutoa elimu kwa njia ya gari maalum katika maeneo kadhaa ya jiji la
Dodoma ikiwemo Mnada Mpya na Soko la Machinga Complex.
Mada
mbalimbali zilizowasilishwa na Maafisa hao zilikuwa ni pamoja na matumizi ya
TEHAMA katika kuongeza ufanisi wa utoaji haki nchini, Nafasi ya Kituo cha
Huduma kwa Mteja katika kuboresha huduma za Mahakama na kuongeza imani kwa
Umma, Wosia na umuhimu wake katika kujenga jamii yenye Amani na maendeleo ya Taifa,
Warithi na haki za warithi, Taratibu za malipo ya mirathi na pia taratibu za
uendeshaji mashauri ya mirathi, ndoa, talaka na kuasili.
Aidha,
Maafisa hao wa Mahakama ya Tanzania walijimwaga mtaani kwa wananchi kwa kutoa
mada za Mchango wa Maboresho ya Mahakama katika kukuza ustawi wa haki madai na
uchumi wa Taifa, Mchango wa Mahakama katika kuboresha na kurekebisha sheria na
kanuni ili kurahisisha upatikanaji wa haki madai kwa wakati vilevile,
utekelezaji wa amri na tuzo za Mahakama nafasi ya Mahakama katika kuhakikisha
haki inafikiwa.
Akitoa
elimu kwa umma kuhusu masuala ya mirathi, ndoa na talaka Mhe. Sifa Jacob
amesema, msimamizi wa mirathi huteuliwa na Mahakama kulingana na majadiliano na
mapendekezo ya ukoo husika wa marehemu na akasisitiza kuwa jamii inatakiwa
kutambua kuwa msimamizi wa mirathi siyo mmiliki wa mali za marehemu kwani msimamizi
anawajibu wa kukusanya mali za marehemu, kugawa mali halali za marehemu kwa
warithi na kulipa madeni kama yapo kwa mujibu wa utaratibu na pia anaweza
kushitakiwa ama kushitaki kama italazimu kufanya hivyo.
“Napenda
niwahakikishie ndugu wananchi msimamizi wa mirathi siyo mmiliki wa mali za marehemu
kazi zake za msingi akishateuliwa na Mahakama anawajibu wa kuhakikisha
wanufaika wa mirathi wanapata mgao unaostahiki kutokana na mali alizoziacha
marehemu aidha iwe ni kwa wosia ama bila wosia kadri busara itakavyo iongoza
familia husika,” amesema Mhe. Jacob.
Wakati
huo huo akitoa elimu kuhusu Matumizi ya TEHAMA mahakamani yanavyorahisisha
utoaji wa haki kwa wananchi na kwa wakati Afisa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania
Bw. Witness Ndenza amesema, mifumo ya TEHAMA imekuwa msaada mkubwa katika
kuharakisha shughuli za utoaji haki kwa kupitia mfumo wa kuratibu mashauri (e-
CMS) mathalani upatikanaji wa nakala za hukumu kwa njia ya mtandao, kusajili
mashauri, utoaji wa ushahidi wa mashauri mahakamai, malipo ya ada za Mahakama,
utambuzi wa mawakili halali na wasio na sifa, kushughulikia taarifa za
kiutumishi, mfumo wa kutambua Mahakama mahali zilipotolea huduma, kuongeza
uwazi na uwajibikaji wa shughuli za Mahakama na kusaidia kusomana kwa taarifa
mbalimbali wakati zinapohitajika kupitia mifumo ya kielektroniki.
“Ni
wajibu wa kila mwananchi kujielimisha kutumia mifumo hii ya kimtandao ili
kuweza kupunguza gharama za kuendesha mashauri na kuokoa muda ili kupata muda
wa kutosha kufanya shughuli za kiuchumi ili kuweza kujiingizia kipatao kwa maakama
mifumo imerahisisha shughuli za uendeshaji wa mashauri na kupunguza adha kwa
wananchi kufika mahakamani pasipo kuwa na ulazima wa kufanya hivyo,” ameongeza
Afisa TEHAMA huyo.
Naye,
Afisa Uchumi Idara ya Mipango na Uratibu kutoka Mahakama ya Tanzania Bw.
Kisingi Mhando akitoa mada ya Programu ya maboresho ya Mahakama amesema,
Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za kimahakama
hususani ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ya haki.
“Ujenzi
wa majengo ya kisasa kuanzia ngazi za Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya
Rufani, ukarabati mkubwa wa majengo ya zamani ili kusogeza huduma za utoaji
haki karibu zaidi na wananchi, uboreshaji wa mifumo ya kuendeshea mashauri kama
ilivyotajwa awali na kuweka mipango mathubuti ya kupunguza na kama siyo kuondoa
kabisa mlundikano wa mashauri kwa kushirikiana na wadau wa mnyororo wa haki
nchini ili mwananchi aweze kupata haki kwa wakati na pia kuongozwa na Mpango
Mkakati ili kufikia malengo na vilevile kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo,” amesema Bw. Mhando.
Kwa
upande wake, Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Denice Mlashani amesema, Kituo hicho kimeanzishwa ili kuwasaidi wananchi
kutoa mrejesho wa huduma wanazopata kutoka mahakamani kwa kuwasilisha maoni,
pongezi, malalamiko ya namna huduma za Mahakama zinavyotolewa kwa wananchi.
Kituo kinafanya kazi masaa 24 siku saba za wiki kupokea na kuchakata maoni ya wananchi
juu ya huduma za Mahakama na hatua stahiki huchukuliwa kurekebisha dosari na
kasoro zilizobainishwa na mteja kwa wakati.
“Hii
inasaidia zaidi wananchi watapata fursa ya kutoa mrejesho wa huduma wanazopokea
kupitia maoni yao. Maoni yatakayotolewa yatatumika kama mtaji wa kuboresha
utoaji haki nchini,” ametanabaisha Mhe Mlashani.
Kwa
upande Mwingine, akitoa mada ya Mchango wa Mahakama katika kuboresha na
kurekebisha sheria na kanuni ili kurahisisha upatikanaji wa haki madai kwa
wakati Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Maktaba
ya Mahakama ya Tanzania Mhe. Kifungu Mrisho Kariho amesema, Mahakama ya
Tanzania kupitia Kamati ya Jaji Mkuu ya mapitio ya kanuni imefanya kazi nyingi
za kumshauri Jaji Mkuu na kurekebisha baadhi ya kanuni za uendeshaji wa
mashauri ya madai mathalani kupitia mchako huo Mahakama imeweza kupunguza hatua
za uendeshaji wa mashauri ya madai kutoka hatua 38 za awali hadi hatua 21 ili
kuharakisha utoaji haki kwa wananchi.
“Na
pia kuna kanuni za uendeshaji wa mashauri ya madai madogo zilizoanza kufanya
kazi mwaka 2023, kwa sababu zinaenda tofauti na zile kanuni za madai ya kawaida
yanayoendeshwa na Mahakama, unaweza kuwa unamdai mtu milioni mia tano au mia
tatu ukatumia kanuni hizi ambapo kesi yako ikasikilizwa ndani ya miezi mitano
au mwezi mmoja na ukapata haki yako,” ameongeza Mhe. Kariho.
Mhe.
Kariho amesema kwa kutumia kanuni hizo mdaawa anatakiwa kufungua madai yake
ndani ya siku saba na anayekujibu atafanya hivyo ndani ya siku saba lakini
baada ya kusikilizwa madai hayo Hakimu hatakiwi kukaa zaidi ya siku 30 kabla
hajatoa uamuzi wa madai hayo. Na pia Kanuni hizo zinaruhu maombi ya mdomo
kusikilizwa hapo hapo wakati yamewasilishwa na mleta maombi. Vilevile, Kanuni
hizo zimeondoa mbinu za kiufundi wakati wa uendeshaji wa mashauri madogo ya
madai. Kanuni hizo zinalenga mashauri ya kuanzia milioni mia moja kushuka chini
au kupanda juu hasa kwa masahuri ya madai madogo.
“Ukifungua
shauri la madai kwa njia hiyo utakuwa unaepuka zile taratibu za kawaida za
madai zinazoongozwa na sheria Madai Sura namba 33 ambazo zimefanyiwa marekebisho mwaka 2022 tunawashauri
wananchi kuzitumia Kanuni hizi ambazo zimerahisisha uendeshaji wa mashauri ya
madai,” amesema Mhe. Kariho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni