Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Arusha
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel tarehe 31 Desemba, 2024 alitembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha lengo likiwa ni kujua maendeleo ya ujenzi huo.
Akizungumza na Mwangalizi wa eneo la Mradi huo, Bw. Elirehema Simbo, Mtendaji Mkuu alisema kuwa, amefika katika eneo la Mradi ili kuona hatua ya ujenzi iliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kujua changamoto wanazokumbana nazo katika ujenzi wa Mradi huo.
“Nimekuja kuona hali halisi ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai na kusikia kutoka kwenu juu ya changamoto mnazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yenu ya ujenzi, ikiwa ni pamoja na kujua mikakati mliyojiwekea katika kuhakikisha kasi ya umalizaji wa Mradi huu inaongezeka na hatimaye uweze kukamilika kwa wakati,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Akizungumzia hali ya Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai, Bw. Elirehema Simbo alisema kuwa, ujenzi umefikia hatua ya kuweka paa (roofing) na kwamba wamefanikiwa pia kuunganisha huduma za maji na umeme katika eneo la Mradi huo.
“Mara tu kazi ya upauaji itakapokamilika, kazi za ndani ya jengo sambamba na zile za nje zitaendelea, tunachoomba ni fedha kutolewa kwa wakati ili kuendana na kasi ya ujenzi. Vifaa vya ujenzi vipo katika eneo la mradi na kazi zinaendelea kama mnavyoona,” alisema Bw. Simbo.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu huyo aliwatembelea pia watumishi wa Mahakama hiyo na kuwasalimia pamoja kukagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai na kutoa maelekezo ya kupima na kujua mipaka ya eneo la Mahakama hiyo kwa lengo la kujua idadi ya miti inayotakiwa kupandwa katika mipaka ya eneo hilo.
Akizungumzia hali ya mashauri katika Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Walter Mwijage alisema kuwa hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2024 jumla ya mashauri 1,398 yalisajiliwa na kati ya hayo 1,385 yalikuwa tayari yamesikilizwa na kuamuliwa.
Baada ya kupata taarifa hiyo fupi Mtendaji Mkuu aliwapongeza watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai kwa kufanya kazi kwa bidii, ikizingatiwa kuwa idadi ya Mahakimu ni watatu pekee lakini wameweza kumaliza idadi kubwa ya mashauri.
Katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu aliambatana na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bi. Aisha Ally.
Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai ni moja kati ya Mahakama za Mwanzo zilizo chini ya Mahakama ya Wilaya Arumeru mkoani Arusha na ndio Mahakama yenye mashauri mengi kuliko Mahakama zingine katika Wilaya hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai akiwa pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Maji ya Chai alipotembelea mahakamani hapo tarehe 31 Desemba, 2024. Wa tatu kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Bi. Aisha Ally.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni