Kikao kazi cha siku tano kilicholenga kupitia na kuboresha Mwongozo wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mahakama wa mwaka 2019, ili kujumuisha ukaguzi wa Mahakama za Watoto, kimehitimishwa.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho kilichokuwa kinafanyika katika Ukumbi wa Mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba, aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua ya kuanzisha mchakato wa maboresho ya mwongozo huo kwa lengo la kuzijumuisha Mahakama za Watoto.
Jaji Mwaseba, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, alieleza kuwa kwa muda mrefu eneo la ukaguzi wa Mahakama za Watoto halikuwa na mwongozo rasmi wa ukaguzi, hali iliyosababisha ukaguzi kutofanyika kwa ufanisi na kutokuwepo kwa taarifa rasmi za kila robo mwaka, tofauti na Mahakama nyingine.
“Daima nimekuwa nikitamani kuona Mahakama za Watoto zikikaguliwa kwa weledi ili kubaini mapungufu yaliyopo kwa kuwa zina upekee wake katika uendeshaji wa mashauri. Mapitio haya ya Mwongozo wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mahakama, 2019 kwa lengo la kujumuisha ukaguzi wa Mahakama za Watoto, Shule za Maadilisho (approved schools) na Mahabusi za Watoto (retention homes), yataboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa haki kwa Watoto na kulinda ustawi wao,” alisisitiza Jaji Mwaseba.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Naibu Msajili na Mratibu wa Dawati la Watoto Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mhe. Mwajabu Mvungi kwa uratibu madhubuti wa kikao kazi hicho ambacho kitakuwa chachu ya kuimarisha usimamizi wa haki za Mtoto. Aidha, aliishukuru timu ya maofisa waliopitia na kuboresha mwongozo huo kwa umahiri wao uliochangia kufanikisha kazi hiyo kwa kiwango cha juu.
Kadhalika, Mhe. Mwaseba alilipongeza Shirika la UNICEF na Bi. Victoria Mgonela, Mtaalam wa Ulinzi na Haki za Mtoto katika Ofisi ya Mwakilishi wa UNICEF anzania, kwa ushirikiano mzuri na juhudi thabiti zilizochangia katika kuboresha mifumo ya utoaji haki kwa Watoto nchini.
Katika kipindi chote cha kikao kazi hicho, washiriki walijadili na kupitia kwa kina vipengele muhimu vinavyohusu usimamizi na ukaguzi wa Mahakama za Watoto. Majadiliano yalihusisha pia mwongozo wa usimamizi na ukaguzi wa mahakama mwaka 2019, fomu za ukaguzi wa Mahakama na Magereza, Sheria, kanuni, waraka, taratibu za mazoea, pamoja na mfumo wa e-CMS ili kuhakikisha mwongozo mpya unazingatia mazingira halisi ya utoaji haki kwa Watoto.
Kwa upande wake, Mhe. Mwajabu aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuratibu na kuwezesha kikao kazi hicho na kueleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, kikao hicho pia kilibaini changamoto mbalimbali. Mojawapo ni ukosefu wa mfumo wa mawasiliano na ushirikiano wa pamoja kati ya Mahakama na Wadau wengine muhimu wa haki za Watoto, jambo ambalo limekuwa kikwazo katika kushughulikia ipasavyo masuala ya Watoto wanaokinzana na kukutana na Sheria.
Alieleza kuwa anaamini kuwa mapendekezo yaliyotolewa na maboresho yaliyopendekezwa yatakapoanza kufanyiwa kazi yataleta suluhu ya changamoto hizo kwa manufaa ya haki za Watoto nchini Tanzania.
Maofisa wa kikao kazi wakiwa wanajadili masuala
mbalimbali ya kikao kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni