Jumatano, 21 Mei 2025

WANAFUNZI CHUO CHA MWEKA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO MAHAKAMA KUU MANYARA

Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara

Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro wamefanya ziara ya kujifunza shughuli na taratibu mbalimbali za kimahakama, Mahakama Kuu Manyara.

Ziara hiyo, iliyofanyika leo tarehe 21 Mei, 2025 jumla ya wanafunzi Hamsini na tatu (53) kutoka Chuo hicho waliambatana na walimu wao watatu (3) kwa lengo la kujifunza taratibu na masuala mbalimbali yanayotendeka mahakamani kwa njia ya vitendo ili kuwasaidia katika elimu wanayojifunza chuoni.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Karimu Mushi, amewafundisha wanafunzi hao juu ya taratibu mbalimbali za usikilizwaji wa mashauri yanayohusu Wanyamapori kuanzia hatua ya kwanza yanapofunguliwa, kusikilizwa na hata hatua ya mwisho ya utoaji wa Hukumu.

Aidha, Mhe. Mushi aliwasisitiza wanafunzi hao, kujitahidi kuhudhuria mahakamani mara kwa mara kwa sababu kujifunza kwa vitendo kuna tija zaidi kuliko kujifunza kwa nadharia pekee.

“Chuoni mnasoma zaidi kwa nadharia, nawapongeza kwa kuja leo na kushuhudia namna ya mashauri haya yanayohusu wanyamapori yanavyoendeshwa mahakamani. Mafunzo haya yataongeza tija na uelewa wenu zaidi katika hayo mnayojifunza chuoni,” alisema Mhe. Mushi.

Naye, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu, Manyara Mhe. Thobias John alitumia nafasi hiyo kuwafundisha wanafunzi hao juu ya Muundo wa Mahakama ya Tanzania ulivyo.

“Mahakama zetu hapa nchini, kuanzia Mahakama ya Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu Pamoja na Mahakama ya Rufaani zina taratibu zake za usikilizaji wa mashauri kulingana na uzito wa mashauri husika hivyo ni vema mkafahamu kuwa hata haya mashauri ya Wanyamapori mathalani hayawezi kusikilizwa katika ngazi za Mahakama za Mwanzo,” amesema Mhe. Thobias John.

Mwendesha Mashtaka wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Bw. Rusticus Mahundi, aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuchagua Mahakama Kuu Manyara kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu taratibu za kimahakama.

“Mmefanya jambo sahihi kuichagua Mahakama hii kwa sababu mashauri mengi yanayohusu wanyamapori yanashughulikiwa hapa kutokana na sababu za uwepo wa Mbuga za Wanyama na Mapori mengi ya akiba ambapo makosa mengi yanayohusu wanyamapori yanafanyika,” alisema Bw. Mahundi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Walimu waliombatana na wanafunzi hao Dkt. Emanuel Martin baada ya mafunzo hayo aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Manyara kwa kuwapokea vema na kuwapa Elimu waliyokuwa wakiihitaji.

“Tunashukuru sana Uongozi wa Mahakama Kuu Manyara kwa kutupokea na kwa ushirikiano mliotupa, tuaamini kuwa elimu hii itatusaidia sana na tutaendelea kuja hapa kwa ajili ya mafunzo mengine” alisema Dkt. Martin.

Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara imeendelea na utaratibu wa  kutoa elimu kwa kwa wananchi wanaofika mahakamani kila wakati lakini pia kwa kupitia vyombo vya Habari vilivyopo hapa mkoani kwa lengo la kuendeleza mahusiano bora kati ya Mahakama na wadau wanaosaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama.

Wanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa wakiwa nasikiliza kwa makini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu mbalimbali katika ziara yao ya Mafunzo Mahakama Kuu Manyara iliyofanyika leo tarehe 21 Mei, 2025.

Wanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa wakiwa nasikiliza kwa makini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu mbalimbali katika ziara yao ya Mafunzo Mahakama Kuu Manyara iliyofanyika leo tarehe 21 Mei, 2025.

Wanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa wakiwa nasikiliza kwa makini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu mbalimbali katika ziara yao ya Mafunzo Mahakama Kuu Manyara iliyofanyika leo tarehe 21 Mei, 2025.

Wanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka wakiwa wakiwa nasikiliza kwa makini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu mbalimbali katika ziara yao ya Mafunzo Mahakama Kuu Manyara iliyofanyika leo tarehe 21 Mei, 2025.

Hakimu Mkazi wa Mahakama Kuu Manyara ambaye pia ni Katibu wa Sheria wa Jaji Mhe Thobias.K.John akitoa Mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka ( hawapo pichani) waliofika Mahakama Kuu Manyara kwa ajili ya ziara ya Mafunzo.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Mhe. Karimu Mushi akitoa Mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka (hawapo pichani) waliofika Mahakama Kuu Kanda ya Manyara kwa ajili ya ziara ya Mafunzo leo tarehe 21 Mei, 2025.

Mwendesha Mashtaka wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Bw. Rusticus Mahundi akizungumza na wanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka (hawapo pichani) waliofika Mahakama Kuu Manyara kwa ajili ya ziara ya Mafunzo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni