Alhamisi, 22 Mei 2025

WANAFUNZI WAVUTIWA NA TAALUMA YA SHERIA: WATAMANI KUWA MAHAKIMU NA MAJAJI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jumla ya wanafunzi wa darasa la saba 116 wa Shule ya Msingi Bangwe iliyopo mkoani Kigoma hivi karibuni walitembelea  Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kuonesha nia ya kusomea taaluma ya sheria siku za mbeleni kufuatia kuvutiwa na kufurahishwa elimu waliyopata wakiwa katika Mahakama hiyo.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akitoa elimu kuhusu Muundo wa Mahakama kwa wanafunzi hao ili wafahamu uwezo wa Mahakama husika, mamlaka zake na jinsi zinavyofanya kazi, wanafunzi hao walionesha kuhamasika kujifunza kuhusu huduma za Mahakama na shughuli zake za kila siku. 

Mhe. Msola aliwaeleza kuwa, Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ndio Mahakama inayopokea mashauri yote ya rufaa kutoka Mahakama za chini pamoja na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba (DLHT) na Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa Mkoa huo.

Aidha, aliongeza kuwa, katika jengo hilo, ipo Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani ambayo inashughulikia rufaa zote kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Pamoja na hayo, wanafunzi hao waliuliza ni hatua gani huchukuliwa iwapo mtoto akikutwa na hatia katika makosa ya jinai. Akijibu swali hilo, Mhe. Msola aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, Mahakama zinapomkuta mtoto na hatia kwa makosa ya jinai huadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya watoto lakini pia kwa kuupa kipaumbele ustawi wa mtoto huyo.

Kwa upande wake, Mwalimu wa darasa hilo, Bw.Alexander Toy aliushukuru uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kwa ukaribisho na kuwawezesha kupata elimu ya sheria na huduma za Mahakama.

 Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Darasa la saba wa Shule ya Msingi Bangwe mkoani Kigoma aliyeketi kulia kwa Mhe. Msola ni Mwalimu wa darasa hilo, Bw.Alexander  Toy na kushoto kwa Mhe. Msola ni Kiongozi wa wanafunzi hao, Bi. Noela Tabagi. Wanafunzi hao walitembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wa darasa la saba  Shule ya Msingi Bangwe waliotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akifafanua jambo wakati anafundisha wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Bangwe walipotembelea Mahakama hiyo.

Mwanafunzi Bi. Nurrat Adamu, alienyoosha mkono akiuliza swali la kutaka kujua ni hatua gani huchukuliwa iwapo mtoto atakutwa na hatia katika makosa ya jinai.

Wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Bangwe wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni