Alhamisi, 28 Agosti 2025

MAJAJI NA MAHAKIMU TUNA WAJIBU WA KUDUMISHA AMANI YA TAIFA KUPITIA KAZI ZETU: JAJI MKUU

·       Awakumbusha Majaji na Mahakimu kushughulikia mashauri ya uchaguzi kwa haki

·       Awakumbusha Majaji na Mahakimu kuzingatia viapo walivyokula wakati wa uapisho wao

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Mahakama ya Tanzania ina nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa, nchi inakuwa katika hali ya amani na utulivu kwa kusimamia ipasavyo jukumu la utoaji haki kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.

Hayo yameelezwa leo tarehe 28 Agosti, 2025 na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yanayotolewa kwa Majaji wa Mahakama Kuu.

“Katika kutekeleza jukumu hili, Mahakama inapaswa kuzingatia masharti ya Ibara ya 107A (a) - (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yanaweka misingi ya utoaji haki, pamoja na Ibara ya 107B inayoelekeza kuwa, katika kutekeleza jukumu hilo la utoaji haki Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia masharti tu ya Katiba na yale ya sheria za nchi,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu amewataka Majaji na Mahakimu kutekeleza jukumu la utoaji haki inavyotakiwa kwani ni kazi ambayo wamekasimiwa na Mungu na inatambulika hata kwenye Vitabu Vitakatifu vya Mungu ikiwemo Biblia na Quran, na kuwasihi kusoma Biblia kwenye vitabu vya ‘Kumbukumbu la Torati 4:2, 6, Kutoka 18:21-22 na 2 Mambo ya Nyakati 19: 6-7.

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 na umuhimu wa mafunzo hayo, Mhe. Masaju amesema kuwa, kila Jaji au Hakimu anapaswa kufahamu kwamba, mashauri ya uchaguzi ni mashauri yenye mvuto wa kipekee na yanapaswa kushughulikiwa kwa umakini na mapema ipasavyo.

 Vilevile, amesema ni muhimu kukumbuka kuwa Uchaguzi Mkuu unabeba mustakabali wa taifa kwa kuingiza kazini Serikali ambayo kimsingi inapata mamlaka kupitia wananchi, na kwa vile Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba inatokana na Wananchi ndio maana hata kiwango cha kuthibitisha madai kuwa uchaguzi ni batili ni kile cha kwenye mashauri ya jinai, yaani pasipo kuacha shaka.

“Tunao uwezo mkubwa wa kutekeleza wajibu wetu, umuhimu wa mafunzo haya ni kubadilishana uzoefu kuhusu mashauri ya uchaguzi, zingatieni kujiamini katika usikilizaji wa mashauri hayo, jiridhisheni pasipo na shaka kabla ya kutoa uamuzi,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, amewasihi Majaji hao kusoma Sheria mbalimbali zinazosimamia masuala ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ikiwemo Sheria Na.1 ya mwaka 2024, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 250 Toleo la 2023, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, Sheria Na. 2 ya Mwaka 2024, Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura 322 Toleo la 2023, ili kuwa na ufahamu kuwa ni makosa gani yanaweza kubatilisha uchaguzi na ni mazingira gani yanaweza kusababisha uchaguzi ukahairishwa.

Kadhalika, Mhe. Masaju ametoa rai kwa kila Taasisi inayohusika katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 kuhakikisha kuwa, inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Jaji Mkuu amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, na Jeshi la Polisi. Hivyo, ni muhimu kwa taasisi hizo kukumbuka kuwa, sheria zinaendelea kufanya kazi kipindi hicho chote cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha uwezo wa Maofisa Mahakama, yaani Majaji na Mahakimu katika namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi ili kuwaweka tayari kushughulikia kwa weledi na mapema ipasavyo mashauri hayo pale ambapo wadaawa watakuwa wamegonga milango ya Mahakama kutafuta haki.

Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa, Kundi la kwanza la Mafunzo hayo limejumuisha jumla ya Majaji Wafawidhi na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu 49 na yamepangwa kutolewa kwa awamu kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto.

  
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akifungua Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yanayotolewa kwa Majaji wa Mahakama Kuu leo tarehe 28 Agosti, 2025  kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



Picha mbalimbali za Washiriki wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi ambao ni Majaji Wafawidhi na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha).

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa neno wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa
Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu wanaoshiriki katika 
Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.
Meza Kuu ikiongozwa na 
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa mafunzo hayo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wanaoshiriki katika Mafunzo hayo.

Meza Kuu katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya Maandalizi ya Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)


















 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni