Jumatano, 10 Septemba 2025

JAJI MKUU ATAKA MIKAKATI THABITI KUSIMAMIA SHERIA YA UHIFADHI WA WANYAMAPORI

  • Ataka kila Mdau wa Uhifadhi kuwajibika ipasavyo kwenye eneo lake

Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha

Wadau wa uhifadhi wa Wanyamapori nchini wametakiwa kuweka mikakati thabiti itakayowawezesha kuwajibika na kusimamia ipasavyo Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Uhifadhi wa maliasilia ikiwemo Mazingira na Wanyamapori.

Akizungumza jana tarehe 09 Septemba, 2025 jijini Arusha wakati akifungua Mafunzo baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wadau wa Haki Jinai, Mgeni Rasmi ambaye ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju alisema licha ya kuwepo kwa sheria hiyo bado kumekuwa na changamoto kadhaa katika eneo la uhifadhi wa maliasili.

Mhe. Masaju alisema pamoja na kusimamia Sheria kuna miongozo mingine ya kusimamia uhifadhi ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sera ya Uhifadhi, Matamko ya Wakuu wa Taifa ikiwa ni pamoja na Tamko la Hayati Mwalimu Nyerere la mwaka 1961 kuhusu uhifadhi ambapo alinukuu tamko hilo kuwa, “uhai wa wanyamapori (Wanyama na Mimea) ni jambo linalotuhusu sana sote katika Afrika, viumbe hawa wa porini wakiwa katika mapori wanamoishi sio muhimu tu kwa ajili ya kuwavutia ni sehemu ya mustakabali wa maisha yetu ya baadaye, kwa kukubali dhamana ya wanyamapori wetu tunatamka kwa dhati kwamba tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba wajukuu wa watoto wetu wataweza kufurahia urithi huu mkubwa na wa thamani adimu.......”

Kadhalika, Jaji Mkuu aliwataka Wadau hao wa uhifadhi kusoma na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo ukurasa wa 41 wa Dira hiyo unasisitiza juu ya uhifadhi wa mazingira kuwa ni muhimu katika kufikia malengo...., vilevile amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki na wajibu huku akinukuu Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema kwamba kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yoyote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine, vilevile watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa Taifa kwa umakini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao......

Mhe. Masaju aliongeza pia kwa kurejea Ibara ya 25 (i) a-b ya Katiba ambayo inasema kila mmoja anatakiwa kuwajibika na kwamba kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na kila mtu anao wajibu wa kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali na kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.

“Tujiulize, nidhamu ya kazi yetu ni nini sisi tuliopo kwenye Vyombo vya utoaji maamuzi,  tuliopo mahakamani nidhamu yetu ya kazi ni nini, waliopo kwenye uhifadhi nidhamu yao ya kazi ni ipi na malengo yao yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria. Haya mambo lazima tuyazingatie,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Alisema kwamba, Kipaumbele cha tatu cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni Uwajibikaji kwa watumishi wa umma, huku akisisitiza uwajibikaji wa kila Mdau wa uhifadhi ambapo alishauri kuwa, kuna haja ya kutungwa kwa Sheria ya Uwajibikaji ili suala la uwajibikaji liweze kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee na kusimamiwa ipasavyo.

“Sisi hapa hatung’ang’anii huu uhifadhi kwa sababu ya kudumisha uhai wetu tu kwa maana ya ‘ecology’ lakini pia ni kwa sababu ya manufaa ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni,” alisisitiza Mhe. Masaju.

Mhe. Masaju alisema kuwa, kumekuwa na changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ujangili na biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu ambapo matukio ya ujangili wa wanyamapori na biashara haramu ya meno ya tembo yamekuwa yakiongezeka,” alieleza Jaji Mkuu.

 

Aliongeza kuwa, changamoto nyingine ni kuongezeka kwa matumizi ya silaha za kivita kwenye matukio ya ujangili, kutokuwepo kwa vikao kazi vya kitaaluma kati ya Majaji, Mahakimu, Mawakili wa Serikali na Wadau wengine wa Uhifadhi ikiwa ni pamoja na TANAPA na Idara ya Misitu, jambo ambalo linafifisha mahusiano baina wadau wote.

 

“Changamoto nyingine ni kutozingatia umuhimu wa urithi wa Taifa kwenye Uchumi wa nchi wakati wa kushughulikia migogoro ya maliasili, ugumu wa kupata Shahidi binafsi unaotokana na mazingira ya maeneo ambayo ujangili unatokea, kuongezeka kwa uingizaji mifugo katika maeneo ya Hifadhi kunakosababisha wanyamapori watoke na kuingia katika maeneo ya jamii na kusababisha uharibifu wa mazao pamoja na kujeruhi ama kusababisha maafa kwa jamii,” alisema Jaji Mkuu.

 

Mhe. Masaju aliongeza kuwa, kumekuwa na migogoro kati ya wanyamapori na binadamu ambayo inatokana na Uingizaji mifugo katika maeneo ya hifadhi na kufungwa kwa mapito ya wanyamapori.


Mhe. Masaju aliwasihi wadau hao kila mmoja katika nafasi yake kuwajibika ipasavyo katika usimamizi wa Sheria na miongozo mbalimbali ili kuondoa changamoto hizo zinazoikabili sekta hiyo muhimu ambayo inachangia kwa asilimia kubwa kuongeza kipato cha nchi na maendeleo kwa ujumla.


Kadhalika, Jaji Mkuu alionesha kusikitishwa na kukemea tabia ya baadhi ya wadau wakishirikiana na watu wa nchi za nje kuhujumu maliasili za nchi, “Polisi wakishirikiana na watu wa uhifadhi wamekamata watu mara nyingi wengine sio raia wa Tanzania wakisafirisha pembe za ndovu, wengine wakisafirisha faru na kadhalika.”


Aidha, Mhe. Masaju amekemea vitendo vya baadhi ya maafisa wanyapori kuruhusu kuingiza mifugo kwenye hifadhi na baadaye wanaikamata na kuiuza/kutaifisha mifugo hiyo ikiwemo ng'ombe za wafugaji hao na baadaye kugawana.

Aidha, Jaji Mkuu alisema pia kwa muda mrefu zimekuwa zikitumika njia za kawaida katika kutunza mazingira ikiwamo wanyama pori, hivyo ametoa wito kwa wadau hao kuangalia matumizi ya akili Unde (AI) ili kuongezea uwezo njia za zamani zilizokuwa zinatumika.

 

“Ninaamini kwenye kikao hiki na mijadala itaonyesha namna matumizi ya akili unde yanavyoweza kuleta mapinduzi katika uhifadhi wa wanyamapori kwa kuwezesha ufuatiliaji na ugunduzi wa haraka wa vitisho kama vile ujangili na uchanganuzi wa kutabiri mabadiliko ya mazingira na athari za mfumo ikolojia. Zana zinazoendeshwa na AI, kama vile ndege zisizo na rubani zenye utambuzi wa picha na uchanganuzi wa data ya satelaiti, naamini uhifadhi utakuwa wa ufanisi zaidi kuliko mbinu za zamani pekee. Matumizi ya Akili Unde yatasaidia pia kuzuia ujangili,” alieleza Mhe. Masaju.

Aliongeza kuwa, kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa Sheria zinazolenga kuhifadhi mazingira na kipekee sheria ya wanyamapori na kusisitiza kwamba, ushiriki wa Mahakama katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori ni muhimu na haupaswi kupuuzwa.

Aidha, Jaji Mkuu alitoa rai kwamba, wakati mwingine wadau wengine muhimu kama Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Wizara ya Ardhi, Wakala wa Misitu Tanzania wahusishwe katika mafunzo hayo kwa kuwa nao ni sehemu muhimu katika uhifadhi.

Akitoa neno la ukaribisho kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TANAPA wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo naye Naibu Kamishna Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Bw. Misana Mwishawa alisema kuwa, ni jukumu la kila mdau kuhakikisha kwamba uhai wa wanyapori unaendelea kuwepo hadi vizazi vijavyo.

“Mafunzo haya ni jitihada za kuhakikisha kuwa, maliasili zetu zinaendelea kuhifadhiwa, uhifadhi ni kitu endelevu hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki,” alisema Kamishna Mwishawa.

Aliongeza kuwa, kikao hicho kinaonesha bayana kuwa ni utekelezaji kwa vitendo kuhusu uhifadhi wa Rasilimali za Taifa.

Mafunzo hayo yenye kauli mbiu isemayo Kuongeza ushirikiano kati ya Mahakama na teknolojia katika kupambana na uhalifu wa wanyamapori nchini Tanzania” yameandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa lengo likiwa ni kuboresha utekelezaji wa Sheria zinazolenga kuhifadhi mazingira yetu na kipekee sheria ya wanyamapori.




Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akifungua Mafunzo baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wadau wa Haki Jinai jana tarehe 09 Septemba, 2025 jijini Arusha.





Wadau mbalimbali wa uhifadhi wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa 
Mafunzo baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wadau wa Haki Jinai iliyokuwa ikitolewa na Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju jana tarehe 09 Septemba, 2025 jijini Arusha.





Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa TANAPA, 
Bw. Misana Mwishawa akitoa neno la ukaribisho wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo baina ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wadau wa Haki Jinai jana tarehe 09 Septemba, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mlima Meru jijini Arusha.










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni