Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha
Wadau wa Haki Jinai Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wamejipongeza baada ya kutathmini na kubaini kuwepo kwa upungufu wa mahabusu na Watoto katika Gereza la Mahabusu Mkuza Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Pongezi hizo zilitolewa na wadau hao tarehe 17 Oktoba 2025 katika Kikao cha Kusukuma Mashauri cha Mahakama ya Wilaya Kibaha kilichofanyika kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo.
Akitoa pongezi hizo Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda Zakaria alisema wiki moja iliyopita Wadau wa Haki Jinai walitembelea Gereza la Mahabusu Mkuza ambapo walikuta Mahabusu wakiwa wachache na hakuna Watoto au Mahabusu wala wafungwa waliodhaniwa kuwa ni Watoto, hivyo kutoa viashiria kwamba Mahakama pamoja na wadau wote wa Haki Jinai wamefanya kazi yao vizuri na kwa umakini.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai aliwataka baadhi ya Mawakili wa Kujitegemea kuweka shajara zao vizuri ili kuepuka kuahirisha mashauri kutokana na shajara zao kujaa mashauri ya Mahakama nyingine.
Aliwaomba pia Polisi wanapoandaa hati za mashtaka kuzingatia makosa ili wasipeleke mashauri Mahakama za Mwanzo ambazo mamlaka yake ni Mahakama ya Wilaya.
Aliwataka Polisi waweke usawa katika kupeleka mashauri ya jinai Mahakama za Mwanzo kwakuwa Mahakama hizo ziko mbili mjini hivyo wasipeleke Mahakama moja tu.
Sambamba na kikao hicho, kulikuwa pia na Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Madai ambapo hakukuwa na mashauri ya mlundikano lakini yapo yanayokaribia kufikia mlundikano hivyo, Mawakili wametakiwa kupunguza mapingamizi ya kiufundi ili kuepuka mlundikano wa mashauri.
Wakati huo huo Afisa Adhabu Mbadala, Bw. Deogratius Njuu aliwapongeza Mahakimu wa Mkoa wa Pwani maana umekuwa Mkoa wa tatu Tanzania kwa kutumia adhabu mbadala ambayo inaokoa pesa nyingi kwa Serikali. Ikiwa ni pamoja na kupunguza pesa za chakula wawapo gerezani na mahitaji muhimu lakini pia kifungo cha nje kinasaidia taasisi za Serikali kuajiri vibarua kufanya usafi katika Ofisi za Umma na katika maeneo ya wazi na ya jumuiya kama stendi na masokoni.
Kikao hicho cha robo ya tatu ya mwaka kilihudhuriwa na Wadau wa Haki Jinai pamoja na Wadau wa Haki
Madai.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni