· Rais Samia asisitiza amani, umoja na mshikamano kwa Watanzania
· Azitaka Kamati za Ulinzi na Usalama nchini kurejesha amani na utulivu ili maisha ya Watanzania yaendelee kama kawaida
· Marais wa Burundi na Zambia nao wawasihi Watanzania kudumisha sifa ya amani ya Tanzania
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju amemuapisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais
wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha pili.
Kadhalika, Mhe. Masaju
amemuapisha Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Makamu wa
Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hafla ya uapisho ilifanyika tarehe 03 Novemba, 2025 katika Uwanja wa Chamwino Ikulu jijini Dodoma na kushuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Marais na Viongozi kutoka Nchi mbalimbali za Afrika akiwemo Rais wa Burundi, Rais wa Zambia, Rais wa Msumbiji, Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na kadhalika.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mabalozi kutoka Nchi mbalimbali, Viongozi wa Serikali, Bunge, Mahakama, Viongozi wa Dini na Wananchi kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya
uapisho, Mhe. Dkt. Samia aliwasihi Watanzania kuendelea kulinda itikadi ya
umoja, amani na mshikamano ambapo alisema, “ndugu zangu wote tunaoitakia mema
Nchi hii ‘Tanzania’ tumesikitishwa na vitendo vya uvunjifu wa amani, upotefu wa
maisha na uharibifu wa mali za umma na mali za watu binafsi kwenye baadhi ya
maeneo hapa nchini hasa kwenye Majiji na Miji, kilichotokea hakiendani na
taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania.”
Rais Samia alisema,
Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa
undani zaidi kilichotokea na kuirudisha nchi katika hali iliyozoeleka kwa
haraka.
Aidha, Mhe. Dkt. Samia alizitaka
Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi na Usalama na Kamati za Mikoa na Wilaya kuhakikisha
kuanzia jana tarehe (03 Novemba, 2025) maisha ya wananchi yanarejea katika hali ya
kawaida mara moja.
“Amesema hapa Rais wa
Zambia na Rais wa Burundi, machafuko ndani ya nchi si mema hayana thamani na
sifa eidha kwa yeyote yule, kwahiyo ndugu zangu niwaombe sana, tuzingatia
umoja, amani na utulivu wa nchi yetu,” alisisitiza Rais Samia.
Kadhalika, Mhe. Dkt.
Samia alitoa onyo kwa wote waliochochea uvunjifu wa amani, ambapo alisema,
“nitumie fursa hii kutoa onyo kama mama kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa
amani na nawataka watambue kuwa, vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana
nguvu na uwezo wa kujihami ila mazungumzo huzaa mshikamano sasa tuchague lenye
manufaa kwetu kwani usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu zote na
gharama zozote.”
Katika hatua nyingine,
Rais Samia aliwashukuru Watanzania kwa kumpigia kura zilizompa ushindi na
kuahidi kuwa, yeye, Makamu wa Rais pamoja na Wabunge na Madiwani waliochaguliwa watalitumikia
Taifa la Tanzania kwa maarifa na nguvu zao zote ili kuleta maendeleo katika
Taifa hilo.
“Nianze kwa kumshukuru
sana Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na kutuwezesha kushiriki sherehe hizi
za kihistoria kwa Taifa letu, pili niwashukuru Watanzania wote kwa imani yao
kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa mapenzi makubwa na kutupa mimi na Makamu
wa Rais fursa hii adhimu ya kuwatumikia,” alisema Rais Samia.
Aidha, Mhe. Dkt. Samia aliipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuratibu na kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi kwa ufanisi usiotiliwa shaka.
Kadhalika, Rais Samia alikipongeza Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna walivyoendesha kampeni zao.
“Katika uchaguzi huu
tulikuwa wagombea 17 kutoka Vyama mbalimbali nchini tukiwania nafasi ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwashukuru sana wagombea wenzangu 16
ambao kwa hakika wameonesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kuendesha kampeni
ambazo tulishindana kwa hoja na kuonesha kuwa siasa sio vita,” alisema Rais
Samia.
Aliongeza kwa
kuwasisitiza Watanzania kuendelea kudumisha umoja, upendo na mshikamano
sambamba na kuheshimu sheria za nchi.
“Ndugu wananchi sifa moja
ya mwanadamu ni kutokukamilika, aliyekamilika kabisa kabisa bila kasoro yoyote
ni Mwenyezi Mungu peke yake, ndio maana katika shughuli au harakati za wanadamu
tunaunganishwa na mawasiliano, mazungumzo na maelewano au kwa maneno mengine
tunaungwanishwa na suluhu ya mambo katika jamii zetu,” alisisitiza Mhe. Dkt.
Samia.
Alisema, Serikali ya
awamu ya sita itaendelea na falsafa yake ya kuzingatia (four Rs’) ikiwemo
maridhiano na kuwataka wananchi kuchagua upendo badala ya chuki, umoja badala
ya mgawanyiko, huruma badala ya hasira, hekima badala ya kiburi.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste
Ndayishimiye amempongeza Rais Samia kwa ushindi alioupata, kumtakia heri
sambamba na kuwasihi Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Kwa upande wake Rais wa
Zambia akizungumza katika hafla ya Uapisho, Mhe. Hakainde Hichilema naye
amempongeza Rais Samia kwa ushindi aliopata na kutoa rai kwa Watanzania
kuendelea kudumisha na kuilinda amani waliyonayo kwa muda mrefu.
“Sisi sote tunatakiwa
kufanya kazi bila kuchoka kulinda amani na usalama wa nchi zetu ili kuleta
maendeleo, tuchague kufanya mazungumzo ya amani ili kushughulikia changamoto ya
aina yoyote inayoikabili nchi,” alisisitiza Rais Hichilema.
Kadhalika, Mhe. Hichilema ameahidi kuwa, Zambia itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika sekta mbalimbali ili kuendelea kukuza Uchumi wa nchi hizo mbili.
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliibuka Mshindi wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupata asilimia 97.66 katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika nchini tarehe 29 Oktoba, 2025.
.jpg)
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akila kiapo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha pili cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hafla ya uapisho ilifanyika tarehe 03 Novemba, 2025 katika Uwanja wa Chamwino Ikulu jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akimuapisha Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

.jpg)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni