Jumanne, 3 Februari 2026

KIWANGO CHA UONDOSHAJI, UMALIZAJI MASHAURI KANDA YA DAR ES SALAAM CHAONGEZEKA

Na MAGRETH KINABO- Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania   Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amesema, kanda hiyo mwaka uliopita ilipokea jumla ya mashauri 35,259 ambapo mashauri 38,277 yaliamuliwa, na mashauri 4,649 yalibaki.

Akizungumza akiwa mgeni rasmi kwenye Siku ya Sheria iliyofanyika eneo la Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Mhe. Maghimbi amesema mashauri hayo ni kutoka Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

“Kasi ya kusikiliza mashauri imeongezeka kufikia uondoshaji [clearance rate] wa 109 na umalizaji [disposal rate] wa asilimia 89, hii ni hatua kubwa kwa kuwa Mahakama zetu ndani ya Kanda zimeweza kusikiliza mashauri kwa uwiano wa idadi ya mashauri yaliyofunguliwa na yaliyosikilizwa (clearance rate) na kwa kila mashauri 100 yaliyofunguliwa asilimia 89 yamesikilizwa (disposal rate). Vilevile idadi ya mashauri yaliyobaki ilipofika Desemba 2025 imepungua kufikia 4,649 ikilinganishwa na Desemba 2024 yalibaki mashauri 7,579,” alisema Jaji Maghimbi.

Sambamba na hilo, ameongeza kwamba mlundikano wa mashauri umepungua, kutoka mashauri 205 kwa mwaka 2024 hadi mashauri 86 Desemba 2025, ikiwa ni sawa na asilimia 2 ya mashauri yaliyobaki, hivyo ni matarajio ya Mahakama kuwa ifikapo Desemba 2026 hakutakuwa na mlundikano wa mashauri.

Aidha, Mhe. Mghimbi amefafanua   kuwa mafanikio hayo yametokana na ufanisi katika utoaji haki, uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa mashauri, matumizi ya Mahakama za mtandao, vikao vya kuondoa mashauri, kuzuia mlundikano na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa mnyororo wa haki.

Akizungumzia kuhusu mashauri ya kiuchumi Mhe. Maghimbi amesema maendeleo na usikilizwaji wa mashauri ya kimkakati katika kanda hiyo yanaendelea kushughulikiwa, mashauri hayo yanahusu biashara, ardhi, uwekezaji na masuala ya mikataba.

Uamuzi wa mashauri haya umechangia kurejesha fedha katika mzunguko wa uchumi, kulinda haki za wawekezaji na wananchi, na kuimarisha mazingira ya biashara.

Katika kanda ya Dare es Salaam, tarehe 1 Oktoba, 2025, usikilizaji wa mashauri ya kimkakati (biashara, kodi, benki, ardhi, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na uwekezaji) yaliwekewa mkakati maalumu wa usikilizwaji na kutolewa maamuzi.

Mhe. Maghimbi ameongeza kuwa migogoro hiyo ikiwa na wastani wa thamani ya TZS 46,189,670,723,371.70 (Shilingi za Tanzania trilioni arobaini na sita, bilioni mia moja themanini na tisa, milioni mia sita sabini, mia saba ishirini na tatu elfu, mia tatu sabini na moja na senti sabini) na USD 816,772,434.64 (Dola za Marekani milioni mia nane na kumi na sita, elfu mia saba sabini na mbili, mia nne thelathini na nne na senti sitini na nne) ambapo hadi kufikia Desemba 15,2025 mashauri 257 yalikuwa yamekamilika, kufanikisha shughuli za kiuchumi na kuchangia ustawi wa Taifa.

Ameongeza kuwa wakati Mahakama inaanza utekelezaji wa Dira mpya ya 2025-2050, imejidhatiti katika maeneo makuu manne (4) ambayo ni usimamizi wa rasilimali, kuhakikisha kodi za wananchi zinatumika kwa tija, haki sawa kwa wote na kwa wakati, kupambana na mlundikano wa mashauri ili rasilimali zilizofungwa kwenye migogoro zifanye kazi ya maendeleo.

Mkakati mwingine ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa haki na kupunguza gharama kwa mwananchi.

Naye, Wakili Mkuu Mfawidhi wa Mkoa Dar es Salaam kutoka Ofisi  ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Mwema Pumzi amesema ili Mahakama iweze kutoa mchango muhimu katika ustawi na maendeleo ya Taifa ni lazima iwe na sifa mbalimbali, baadhi ya sifa hizo ni uhuru wa Mahakimu na Majaji kutoka kwenye ushawishi, msukumo au vitisho kutoka Mhimili mwingine, vyama vya siasa au nguvu zozote za nje.

Vilevile Bi. Pumzi ameongeza kuwa, Weledi ni Mfumo mzuri wa Mahakama unaowezesha kupunguza msongamano wa mashauri (case backlogs) na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Akizungumza kuhusu uadilifu wa Mahakimu na Majaji Bi. Pumzi amesema kuwa  ni lazima wawe ni watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu na wahakikishe kunakuwa na imani ya umma katika mfumo wa sheria.

Hivyo, Mahakama kama mlezi wa Katiba, mlinzi wa haki za binadamu na utawala wa sheria, ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza ustawi na maendeleo ya Taifa, Mahakama iliyo huru na yenye kuheshimika na kuaminika huhakikisha utekelezaji thabiti wa mikataba, ulindaji wa haki za mali na kudhibiti matendo ya matumizi mabaya ya madaraka, ambayo hatimaye hukuza imani ya wawekezaji na hivyo kuwezesha ukuaji imara na endelevu wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Wakili kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Mzizima, Ipilinga Panya amesema kuwa, kwa sasa TLS inahudumia wananchi mbalimbali wanaohitaji huduma za Msaada wa Kisheria kwa wenye uhitaji na kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili wanapata haki bila vikwazo katika ofisi zake zilizopo kwenye chapter 21 Tanzania nzima.

Ameongeza kuwa kwa mwaka 2025 TLS iliweza kupokea jumla ya watu 421 (270 Wanaume, 151 Wanawake) waliohitaji huduma ya msaada wa kisheria katika ofisi zake ambapo, wateja 209 walishauriwa, 102 walipewa mawakili kwa ajili ya uwakilishi katika Mahakama na wateja 110 walipewa elimu ya kisheria katika masuala mbali mbali ya kisheria, mbali na wateja waliofika moja kwa moja katika ofisi za TLS, wanachama wa TLS ambao ni mawakili wameendelea kupokea na kusimamia zaidi ya mashauri 200 ya jinai yaani doc brief wanayopewa na Mahakama kwa ajili ya uwakilishi wa watuhumiwa wasio na uwakilishi.

 Vilevile, TLS imekuwa ikishiriki katika matukio mbali mbali ikiwamo Wiki ya Sheria na Maonesho ya Saba Saba ambapo ilifikia wananchi 1,769 (Wanaume 895 Wanawake 874) ambao walifika katika mabanda ya TLS kwa ajili ya kupatiwa elimu na huduma za msaada wa kisheria, na ilifikia wananchi 144,824 kwa kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameipongeza Mahakama kwa kupunguza malalamiko ambapo hivi sasa hakuna malalamiko.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini kwa mwaka 2026 yalibebwa na kaulimbiu isemayo “Mchango wa Mahakama katika  Ustawi na Maendeleo ya Taifa”.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akisoma hotuba ya   Siku ya Sheria kwenye viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 2 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,Mhe, Mary Moyo akisoma matukio ya siku hiyo.

Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Kinondoni, Ipilingi Panya akisoma hotuba.

Wakili Mkuu Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Mwema Pumzi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisoma hotuba.

Wageni waalikwa   na baadhi ya watumishi wa Mahakama wakiwa katika sherehe hiyo.

Shule ya Msingi Bunge ikitumbuiza katika siku hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akikagua gwaride maalum la Siku ya Sheria kwenye viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 2 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni