Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora
imeendesha mafunzo maalum kwa Majaji na Mahakimu yanayolenga kuimarisha uelewa wa dhana na taratibu za kupokelewa kwa ushahidi wa kielektroniki
pamoja Maadili na Mienendo
(Nidhamu) ya Kimahakama.
Mafunzo hayo yaliendeshwa hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi aliyewasilisha mada kuhusu ushahidi wa kielektroniki, pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Simiyu, Mhe. Wilbert Martin Chuma aliyefundisha kuhusu maadili na nidhamu ya
kimahakama kwa njia ya mtandao.
Akitoa mada yake, Mhe. Dkt. Mambi alieleza kwa kina dhana
ya ushahidi wa kielektroniki, aina zake na masharti ya kisheria
yanayozingatiwa ili ushahidi huo upokelewe mahakamani. Alisisitiza umuhimu wa
kuzingatia sheria husika, taratibu, pamoja na misingi ya uhalisia, uaminifu na uadilifu wa
ushahidi huo.
“Katika zama hizi za teknolojia, Mahakama haziwezi kukwepa
ushahidi wa kielektroniki. Hata hivyo, ni wajibu wa Mahakama kuhakikisha kuwa, ushahidi huo
umepatikana na kuhifadhiwa kwa njia halali na kwamba haujabadilishwa,”
alisema Jaji Dkt. Mambi.
Aliongeza kuwa Mahakimu na Majaji
wanapaswa kuwa makini katika kupima uzito wa ushahidi wa aina hiyo, hususan
ujumbe wa simu, barua pepe, rekodi za miamala ya kielektroniki na vielelezo
vinavyotokana na mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu, Mhe. Wilbert Martin Chuma
alipowasilisha mada ya Maadili na Mienendo ya Kimahakama kwa njia ya Mtandao, alisisitiza kuwa
maadili ni nguzo kuu ya uaminifu wa Mhimili wa Mahakama akieleza kuwa, huo ni wajibu wa kikatiba
kisheria, kitaaluma na kimaadili akitolea mifano mbalimbali ya ibara za katiba,
vifungu vya sheria na kanuni za maadili.
“Heshima na imani ya wananchi kwa Mahakama inaanzia kwenye mienendo yetu sisi Majaji na Mahakimu. Nidhamu ya
kimahakama ni wajibu wa
kikatiba, kisheria
na kitaaluma,” alieleza.
Alifafanua kuhusu misingi ya uhuru wa kimahakama kwa kufanya kazi bila kupendelea, huba, hofu wala chuki na kuzingatia uadilifu,
kujiepusha na mgongano wa maslahi pamoja na wajibu wa kuilinda hadhi ya Mahakama ndani na nje ya mazingira ya kazi.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha Majaji wa Kanda hiyo wakiwemo Mhe. Dkt. Zainabu Mango na Mhe. Frank Mirindo pamoja na Naibu
Msajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi na Mahakimu
wa ngazi mbalimbali kutoka katika Kanda husika.
Washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu, na kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria na maadili ya kimahakama katika mazingira ya sasa yanayokua kwa kasi ya matumizi ya teknolojia.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni