Jumamosi, 28 Machi 2026

JAJI MKUU AJUMUIKA NA RAIS SAMIA, VIONGOZI WENGINE WA SERIKALI KUAGA MWILI WA LUKUVI

  • Apata wasaa wa kutoa salamu za pole, aeleza kuwa marehemu Lukuvi aliheshimu watu na utu
  • Asema kuwa, marehemu Lukuvi alikuwa ni mtu wa kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua
  • Awasihi Viongozi wa Dini kuendelea kudumisha  umuhimu wa usalama wa jamii, umuhimu wa amani katika jamii, umoja wa kitaifa....

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 28 Machi, 2026 ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Viongozi wengine wa Serikali, familia na wageni waalikwa kushiriki ibada ya kuaga mwili wa Mhe. William Vangimembe Lukuvi aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).

Ibada hiyo imefanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na viongozi wengine wa Serikali.

Akitoa salamu za pole wakati wa ibada hiyo, Mhe. Masaju amempa pole Rais Samia na familia kwa ujumla na kusema kuwa, Marehemu Lukuvi aliheshimu watu na utu na vilevile aliwaheshimu watu wote hususani wale waliofanya kazi kwa ufanisi ipasavyo.

“Mhe. Rais kwanza nikupe pole, narejea tu hizi pole lakini nilishazisema jana, familia nawapeni pole sisi wananchi wote tuliojumuika hapa, na nikushukuru Mhe. kunipa tena fursa ya kuzungumza hapa baada ya kuwa nimezungumza jana kwa kweli sikutegemea kama ningepata fursa hii. Ndugu William Lukuvi ni mtu ambaye aliwaheshimu sana watu, alithamini utu na kutambua kwamba kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake na ndio maana alijenga mahusiano na wenzake bungeni na wananchi wa Jimbo lake la Isimani,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju amesema kuwa, Marehemu Lukuvi aliwaheshimu watu wote wakiwemo wale ambao ni waadilifu na watu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yako kwa ufanisi ipasavyo.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa, marehemu Lukuvi alikuwa ni mtu wa kupenda kujiridhisha na uhalisia wa jambo kabla ya kuchukua hatua na hasa uhalali wa jambo husika kisheria na kwamba alithamini sana utawala wa sheria.

“Nilifanya naye kazi kwa karibu nikiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati Rais Kikwete aliponiteua wakati ule, niliona alivyokuwa akinishirikisha ili ajiridhishe na hatua anayotaka kufanya, lakini hata alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Mshauri wa Masuala ya Siasa na haki za Kijamii nikapata fursa ya kufanya naye kazi tena wakati nikiwa Mshauri wa Masuala ya Sheria aliendelea kuni ‘consult’,” ameeleza Mhe. Masaju.

Kadhalika, Jaji Mkuu ameeleza kwamba, Wiliam Lukuvi alithamini pia mahusiano na kuyadumisha hata kama mtu hana cheo ambapo amesema, “ndugu Lukuvi ni moja kati ya watu wachache ambaye hata mimi baada ya kuteuliwa kuwa Jaji alidumisha mahusiano na mimi, alikuwa akiniandikia hadi meseji nilipata faraja sana,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Masaju amewapongeza Viongozi wa Dini kwa kutoa neno la faraja na kuwaomba kuwa waendelee kuhimiza umuhimu wa usalama wa jamii, umuhimu wa amani katika jamii, umuhimu wa maadili ya jamii na umoja wa kitaifa.

Mhe. Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Jumanne tarehe 31 Machi, 2026 katika Kijiji cha Idodi Iringa vijijini. 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa salamu za pole wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Mhe. William Lukuvi aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) leo tarehe 28 Machi, 2026 kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (wa pili kulia) na Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa kwanza kulia) kwenye ibada ya kuaga mwili ya William Lukuvi aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) leo tarehe 28 Machi, 2026 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. 


Mjane wa marehemu, Mama Germina Lukuvi (wa pili kushoto) akiwa pamoja na watoto wake leo katika ibada ya kuaga mwili wa mpendwa wao Hayati William Vangimembe Lukuvi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.


Picha mbalimbali za Viongozi mbalimbali walioshiriki katika ibada ya kuaga mwili wa Mhe. William  Vangimembe Lukuvi aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) leo tarehe 28 Machi, 2026 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. 

Wageni mbalimbali wakifuatilia ibada ya kuaga mwili wa marehemu William Vangimembe Lukuvi  aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) iliyofanyika leo tarehe 28 Machi, 2026 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha maombolezo alipowasili katika Viwanja vya Karimjee kwenye ibada ya kuaga mwili wa 
marehemu William Vangimembe Lukuvi  aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) iliyofanyika leo tarehe 28 Machi, 2026 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni