Jumatatu, 13 Aprili 2026

MBEYA YAZIDI KUIMARISHA UTENDAJI KAZI KWA NJIA YA TEHAMA

Na. MWINGA MPOLI – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga amekutana na wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama Mkoa wa Mbeya na kufanya nao mazungumzo kuhusu masuala muhimu ya kazi ikiwemo nidhamu, uadilifu, matumizi ya mfumo mpya wa kusajili mashauri pamoja na utunzaji wa vielelezo.

Ameyasema hayo wakati wa kikao kazi hicho kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya. Mhe Tiganga alisisitiza kuwa, maadili ya utumishi wa umma na nidhamu kazini ndiyo msingi wa kazi za Mahakama. Aliongeza kuwa, utunzaji sahihi wa nyaraka na vielelezo ni jambo la msingi katika kuhakikisha haki inatolewa kwa wananchi bila vikwazo.

“Ni vizuri kuusoma mfumo wa kusajili mashauri na kuufanyia kazi, lakini pia tuongeze nidhamu na maadili kazini. Tunapaswa kuhakikisha tunatunza kumbukumbu vizuri pamoja na vielelezo ili kutokwamisha zoezi zima la utoaji haki kwa wananchi.” alisema Mhe. Tiganga

Naye, Hakimu Mkazi Mkuu kutoka Kurungenzi ya usimamizi, ukaguzi, Maadili na ufuatiliaji wa huduma za kimahakama kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Siliti alipata fursa ya kuongea na watumishi hao kwa njia ya mtandao.

Akitoa elimu juu ya utunzaji wa kumbukumbu za Mahakama Mhe. Mohamed Siliti aliwaasa watunza kumbukumbu hao kutimiza wajibu wao na kuepuka kutumia lugha zisizo za staha na nzuri kwa wateja.

Kupitia kikao kazi hicho kiliweka maazimio na kukubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano na weledi mkubwa huku wakizingatia maadili na nidhamu kufuatia kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Aziza Temu, Mtendaji wa Mahakama Bi Mavis Miti, Maafisa Utumishi pamoja na wasaidizi wa kumbukumbu Mahakama Mkoa wa Mbeya.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga (katikati) akiongoza kikao kazi hicho cha wasaidizi wa kumbukumbu na nyaraka (kulia) ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Bi. Marvis Miti.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akitolea ufafanuzi sehemu ya mambo yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho.

Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho

Mmoja wa wajumbe akizungumza jambo katika kikao hicho Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama Kuu Mbeya Bi. Isabela Osiah

Mmoja wa wajumbe akizungumza jambo katika kikao hicho Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya wilaya Mbeya Bi. Queen Mapunda.

Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho
Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho

Sehemu ya Maafisa Utumishi Mahakama Mbeya walioshiriki kikao kazi hicho.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni