Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji
Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Steven Bwana ametoa rai kwa
watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma kufanya kazi kwa
uzalendo ili kujenga Mahakama yenye sifa njema katika Taifa lenye umoja na
uzalendo wa kweli katika utumishi wa umma.
Akizungumza
katika kikao kifupi na watumishi wa Mahakama hiyo jana tarehe 04 Mei, 2026
alipotembelea Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Bwana alisema, “Nimeambiwa mnafanya
vizuri Kigoma, ni rai yangu kwenu kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, uzalendo
wa kweli kwa Taifa na bila kuangalia utapata nini kesho, maana kazi zako
zitakupa kukua, kuaminiwa na kutengeneza nafasi kubwa zaidi katika utumishi
wenu.”
Jaji
Mstaafu huyo amewaeleza watumishi hao kukumbuka kuwa shughuli zao za kila siku
ndio msingi na kichocheo cha maendeleo ya Taifa na kusisitiza kuwa, “Wastaafu
tulifanya sehemu yetu, ambapo teknolojia katika Mahakama kipindi hicho ilikuwa
kidogo sana lakini tulifanya kwa uzalendo na kujituma na shughuli za kusikiliza
mashauri na utawala zilifanyika vema.”
Aidha,
Mhe. Dkt. Bwana alisema kuwa, ni mara yake ya kwanza kufika mkoani Kigoma,
hivyo ni vema kuacha alama ya zawadi ya kitabu chake kiitwacho, ‘Maisha yangu, Utumishi
wangu” chenye Tawasifu yake, ili kiwekwe kwenye Maktaba ya Mahakama hiyo hatimaye
watumishi waweze kusoma maudhui ya kitabu hicho na kuongeza weledi wa kizalendo
katika eneo la maisha ya utumishi wa umma.
Naye
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe.
Agustine Rwizile alipata wasaa wa kumzungumzia walau kwa kifupi Jaji Mstaafu,
Mhe. Dkt. Steven Bwana kupitia kitabu chake kuwa ni moja ya Majaji wa Rufani
ambaye alihudumu kwa weledi, kujituma kwa uzalendo mkubwa wakati wa kipindi
chake, hivyo kufika kwake Kigoma ni jambo la muhimu na kuigwa na watumishi wa sasa
hasa kwa umakini wake na utumishi uliotukuka katika kuwahudumia wananchi katika
nafasi mbalimbali alizowahi kuaminiwa na Mahakama ya Tanzania.
Kwa
upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma,
Mhe. Fadhili Mbelwa, alitoa neno la shukrani kwa Jaji Mstaafu, Mhe. Dkt. Bwana aliyeambatana
na Mkewe kutembelea Mahakama Kuu Kigoma.
Aidha, Mhe. Mbelwa alimuomba Jaji huyo kupanda mti ili kuacha alama ya ujio wake wa kutembea kituo hicho, hata hivyo Jaji Mstaafu huyo aliridhia kupanda mti kama kumbukumbu ya ujio wake Mahakama Kuu Kigoma.
Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Steven Bwana (kulia) akimkabidhi Kitabu cha wasifu wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Agustine Karichuba Rwizile wakati Jaji Mstaafu huyo alipotembelea Mahakama Kuu Kigoma jana tarehe 04 Mei, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Agustine Rwizile akisoma Kitabu alichokabidhiwa na Jaji msatafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dr. Steven Bwana kwa ajili ya watumishi kusoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Agustine Rwizile (katikati) akimkaribisha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Steven Bwana (kulia) alipowasili katika viunga vya Mahakama Kuu Kigoma jana tarehe 04 Mei, 2026. Aliyesimama kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni