- Wafanya Mafunzo na Kikao Kazi
- Jaji Mongela asisitiza utaratibu wa mafunzo ya mara kwa mara
Na JAMES KAPELE, Mahakama-Moshi
Chama
cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Kilimanjaro kimefanya kikao kazi
cha robo ya kwanza tarehe 19 Juni 2026 kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Tawi hilo
Mhe, Elibahati Petro kwa kujumuisha
wanachama kutoka katika Wilaya zote za Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Moshi kwa
kufanya mafunzo na kikao kwa lengo la kujijengea uwezo katika masuala ya
kisheria na kubuni mikakati mbalimbali ya kimaendeleo katika Tawi hilo.
Awali
akifungua mafunzo hayo, Mlezi wa Tawi hilo ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian
Mongella aliwapongeza Wanachama na Viongozi wa Tawi hilo kwa kazi kubwa
wanayofanya ya kujitolea kulijenga Tawi lao na kuwa na utaratibu wa kukutana
kufanya mafunzo ya kujijengea uwezo katika majukumu ya utoaji haki.
“Nawapongeza
sana Viongozi wetu wa Tawi pamoja na Wanachama wote kwa umoja wenu, Tawi hili
ni letu mambo tunayopanga lazima tuyatekeleze kwa pamoja, tukifanya hivyo Tawi
letu litazidi kuwa imara zaidi. Mmefanya vizuri sana kufanya kufanya kikao kwa
kuanza na mafunzo nitafurahi kama mtajenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara kujijengea
uwezo katika masuala mbalimbali ya kisheria,” alisema Jaji Mongella.
Kikao
hicho kilitanguliwa na Mafunzo yaliyohusishwa
mada mbalimbali ikiwemo utoaji wa adhabu mbadala katika mashauri ya jinai,
utekelezaji wa amri za Mahakama katika mashauri ya madai pamoja na namna bora
ya kupokea ushahidi wa kielektroniki katika Mahakama za Mwanzo.
Akifunga kikao hicho, Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo
ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi aliwapongeza Wanachama na Watoa Mada kwa kushiriki
kikao hicho na kufanya mafunzo ya kujijengea uwezo.
Mhe. Kilimi aliwasisitiza Washiriki kujenga
utamaduni wa kufanya hivyo mara kwa mara kwa kuwa, jambo hilo linawajenga
katika shughuli zao kila siku pamoja na kupata muda wa kujumuika pamoja.
Alitoa rai kwa Wanachama kupenda kushiriki katika
michezo mbalimbali ili kuimarisha afya zao pamoja na kujenga utaratibu wa
kujumuika pamoja kwa lengo la kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila
siku.
Mafunzo na kikao hicho vilihitimishwa kwa tafrija
fupi ya kuwapongeza Waheshimiwa Ally Mkama na Jasmin Athuman ambao wameteuliwa
hivi karibuni kuwa Naibu Wasajili.
Picha ya pamoja ya Wanachama wa Tawi la Chama cha
Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tawi la Kilimanjaro.
Katika picha ni sehemu ya washiriki wakiendelea na majadiliano katika mafunzo hayo. Aliyesimama ni Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Kilimanjaro, Mhe. Elibahati Petro akichangia hoja katika kikao hicho.
Wakili wa Kujitegemea Desderius Hekwe aliyealikwa kutoa mafunzo kuhusu Ushahidi wa Kielektroniki katika mafunzo hayo.
Aliyeketi kulia ni Mhe. Aden Kanje, Hakimu Mkazi aliyewasilisha Mada ya Matumizi ya Adhabu Mbadala katika mafunzo hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Moshi, Mhe. Adrian Kilimi (aliyesimama) akifunga kikao hicho.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni