Ijumaa, 19 Juni 2026

JAJI MFAWIDHI MPYA DODOMA AKABIDHIWA OFISI

Na ARAPHA RUSHEKE- Mahakama Kuu Dodoma.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dodoma imeingia katika awamu mpya ya uongozi jana tarehe 18 Juni, 2026, baada ya Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Joachim Tiganga, kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Makabidhiano hayo yalijikita katika kukabidhi majukumu ya kiutawala, nyaraka mbalimbali za ofisi, na taarifa muhimu za utendaji kazi, zote zikiwa na lengo la kuhakikisha mwendelezo wa utoaji wa huduma za kimahakama na usimamizi wa shughuli za Mahakama katika Masjala Ndogo hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Mhe. Dkt. Masabo alimpongeza Jaji Tiganga kwa kukabidhiwa majukumu hayo na kumtakia mafanikio katika utekelezaji wake. 

“Nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Tiganga, tunaungana nawe kumshkuru mwenyezi Mungu kwa kibali ambacho amekupatia ili uje uhudumu hapa uwatumikie watu wake. Namshukuru pia Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, kwa imani kubwa ambayo ameionesha kwako na kuona ni muda sahihi kuweza kufanya kazi katika kituo hiki cha Dodoma,” alisema.

Naye Mhe Tiganga aliwashukuru Viongozi na Watumishi wote wa Mahakama Kuu Dodoma kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa Wananchi.

Makabidhiano hayo yanaashiria mwanzo wa awamu mpya ya uongozi katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, huku yakisisitiza dhamira ya kuendeleza ufanisi, uwazi na ubora katika utoaji wa huduma za Mahakama kwa Wananchi kwa kuzingatia salamu ya Mahakama isemayo Uadilifu,Weredi na Uwajibikaji.


Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (wa kwanza kulia) akikabidhi ofisi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dodoma Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC).


 

Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa kumpokea Jaji Mfawidhi mpya mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu Masjala ndogo Dodoma.

 


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyepo katikati waliokaa), kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga na kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Biswalo Mganga, ikiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama Kuu Dodoma waliohudhuria hafla hiyo ya makabidhiano.


 

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyepo katikati waliokaa), kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga na kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Biswalo Mganga, ikiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma waliohudhuria hafla hiyo ya makabidhiano.


 

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (aliyepo katikati) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (kulia) wakisaini nyaraka za makabidhiano. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Biswalo Mganga, anayeshughudia zoezi hilo.


Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma waliohudhuria hafla hiyo ya makabidhiano.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni