Jumapili, 21 Juni 2026

JAJI RWIZILE AFUNGUA MAHAKAMA ZA MWANZO TATU KIGOMA

Na AIDAN ROBERT-Mahakama Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile ameongoza hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo Bangwe, Wilaya ya Kigoma, Manyovu iliyopo Wilaya Buhigwe na Heru Juu iliyopo Wilaya ya Kasulu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 19 Juni, 2026, Mhe. Rwizile amesisitiza kuwa, “tunachokishuhudia leo ni maono ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, aliwahi kusema, alipokuwa anahutubia Mkutano wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Tarehe 13 Mwezi Januari, 2026 Dodoma, ninamnukuu; - "Ujenzi wa majengo ya Mahakama, uwezeshaji wa rasilimali watu na fedha, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa Majaji, Mahakimu, na watumishi wa Mahakama ni nguzo muhimu zinazowezesha uhuru wa Mahakama kuwa halisi, unaoonekana na unaotekelezeka kwa ustawi wa wananchi na utawala wa sheria kwa ujumla."

Jaji Rwizile amesema, maneno hayo ya Kiongozi Mkuu wa Mhimili wa Mahakama, yanasadifu haja ya watu kupata haki katika maeneo ambayo si tu haki inakuwa imetendeka bali pia inaonekana kutendeka kwa kuzingatia unadhifu wa watoa haki, ubora wa haki yenyewe na mazingira mazuri ya mahali ambapo haki hiyo hutolewa.

“Kupitia maono hayo ya viongozi wetu wakuu wa Mahakama na Serikali, leo hii tunafurahia uzinduzi wa majengo haya tukitambua kuwa, kinachozinduliwa hapa si Majengo wala Samani au Nakshi zinazopendezesha majengo haya, Bali ni dhana thabiti ya Mahakama kama chombo pekee cha utoaji haki kwa vitendo kwa wananchi wetu,” amesema Mhe. Rwizile.

Aidha, ameongeza kuwa, Mahakama hizo tayari wameshazipangia watumishi mahsusi wa kutoa huduma zilizo bora kuendana na ubora wa majengo yenyewe, amesema, “leo hii baada ya ufunguzi, mashauri yataanza kusajiliwa hapa Bangwe na pale Heru Juu na Manyovu kadhalika wataendelea kupatiwa huduma kwa kadri ya mahitaji yao,” amebainisha Jaji Mfawidhi huyo.

“Nitoe Wito kwa Mahakimu na Watumishi wa Mahakama hizi mpya, pamoja na Wengine kwa ujumla, ninyi ndio nguzo kuu ya usimamiaji haki katika ngazi hii. Tendeni kazi kwa mujibu wa viapo vyenu kwani kiapo chetu ni kizuri kinasema bila ya Huba, Woga, Chuki wala upendeleo wa aina yoyote, mnapaswa kuendelea kulinda imani ya wananchi kwa Mahakama kwa kutoa maamuzi yasiyokuwa na upendeleo, hila au ushawishi wa aina yoyote,” amesisitiza Jaji Mfawidhi huyo.

Kadhalika, amesema kuwa, ni muhimu kutoa maamuzi yenye rejea thabiti katika sheria na misingi iliyowekwa na Mahakama za ngazi za juu, “hii inawataka muwe wa kisasa, wenye kujiongezea maarifa na kufuatilia mabadiliko katika maeneo mbalimbali ya kisheria mtakayokuwa mkiyafanyia kazi,” alisema Jaji Rwizile.

“Majengo haya mapya ni mwendelezo wa utatuzi wa changamoto za muda mrefu za kijiografia katika Mkoa wa Kigoma, hakuna shaka kwamba kipindi cha nyuma wakazi wengi walilazimika kusafiri umbali mrefu na kuingia gharama kubwa kufuata huduma katika Mahakama za Mwanzo zilizokuwa mbali na makazi yao kiasi cha kupoteza muda mwingi kwenye mashauri na sio shughuli za kiuchumi na kijamii,” alieleza Mhe. Rwizile.

Aliongeza kuwa, kupitia maboresho hayo ya ujenzi wa Mahakama mpya za Mwanzo, wananchi wataendelea kufikiwa na huduma hizo na kuokoaa muda na gharama.

“Sote tunakubalina kuwa, umbali wa kutoka Bangwe, Kigoma Mjini, Katonga, Gungu, Kibirizi, Mwanga Kusini na Mwanga Kaskazini, Katubuka na maeneo mengine jirani, haikuwa rahisi kutembea na kufuata huduma Mwandiga au Ujiji ambako Mahakama zinapatikana. Kwa sasa uwepo wa Mahakama ya Mwanzo Bangwe ni faraja na majibu ya wengi katika kufuata haki. Inakadiriwa takribani watu 62,582 watanufaika na huduma hii,” alisema Jaji Rwizile.

Kadhalika alisema kwamba, kwa Mahakama za Mwanzo Heru Juu na Manyovu; Wananchi wa Maeneo ya jirani na Mahakama hizo wataondolewa adha ya kusafiri umbali mrefu kuitafuta haki huku shughuli zao binafsi zikikwama, wanufaika wa huduma hiyo inakadiriwa kuwa watu 24,242 kwa kuzingatia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, pia huduma ya Mahakama ya Mwanzo Manyovu hapo awali ilikuwa inapatikana Tarafa ya Munanila, na baadae kutokana na uchakavu wa jengo la awali kushindwa kuwa salama kwa matumizi ya binadamu  huduma ikahamia kwa muda katika Ofisi za Serikali ya Kijiji.

Hata hivyo, Mhe. Rwizile alibainisha kuwa, kwa sasa Mahakama imesogezwa karibu na mpaka wa Tarafa mbili yaani Manyovu na Mnanila, Tarafa ambazo zina idadi kubwa ya watu, ambapo Tarafa ya Manyovu ina wastani wa watu 131,298 wakati Tarafa ya Munanila ina wastani wa watu 15,273 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

“Kumbe uwepo wa Jengo hili kwa sasa litatoa huduma Kata za Munzeze, Janda, Rusaba, Muhinda, Mwayaya, Mkatanga, Mubanga, Kinazi, Kibwigwa na Bukuba, wakati huohuo Kata za Munanila na Nyakimwe nazo zikipata huduma za Mahakama katika jengo hilo jipya,” alieleza Jaji Rwizile.

Kwa upande wake Mgeni wa Heshima katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro, alisema kuwa, uzinduzi wa majengo hayo mapya ni kielelezo tosha kuwa Mahakama imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa wananchi hawapati tu haki, bali wanaipata katika mazingira yenye staha, hadhi na usalama.

“Ujenzi na uzinduzi wa miundombinu hii ya kisasa sio jambo la bahati mbaya ni taswira halisi ya utambuzi wa kina na dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, maboresho haya makubwa ya miundombinu ni tafsiri ya maono ya kimkakati ya Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunaimarisha, tunakuza na kulinda kikamilifu Uhuru wa Mahakama ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Balozi Mhe. Sirro.

Hafla hiyo iliyofanyika katika viunga vya Mahakama ya Mwanzo Bangwe ilihudhuriwa na Viongozi wa ngazi ya Wilaya na Mkoa wa Kigoma pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka.

Wageni wengine ni Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Wilaya za Kasulu na Buhigwe, pamoja Mahakamu wafawidhi wa Wilaya za Buhigwe, Kigoma, Kasulu, Kibondo, Kakonko na Uvinza, sambamba na wadau wa Mahakama na wananchi pamoja na vikundi vya burudani.


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Mahakama za Mwanzo tatu za Bangwe, Manyovu na Heru Juu uliofanyika tarehe 19 Juni, 2026. Wanaoshuhudia kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (kulia) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro (kushoto) kwa pamoja wakifungua kitambaa cha jiwe la msingi la Jengo hilo ikiwa ni ishara ya kufunguliwa kwa Mahakama.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mahakama za Mwanzo tatu katika hafla iliyofanyikia katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa Mahakama za Mwanzo tatu katika hafla iliyofanyikia katika viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Bangwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe ikiwa ni ishara ya alama na historia katika Mahakama hiyo ya Mwanzo Bangwe mara baada ya kufunguliwa.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe ikiwa ni ishara ya alama na historia katika Mahakama hiyo ya mwanzo hiyo mara baada ya kufunguliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Mwanzo Bangwe ikiwa ni ishara ya alama na historia katika Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Nyakoro Sirro (kulia). Waliosimama ni Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni