Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma
Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir
Mruma ametoa rai kwa kila taasisi inayohusika katika mnyororo wa haki
kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi
wa umma.
Mhe. Mruma ametoa rai hiyo leo tarehe 17 Septemba, 2026 alipokuwa
akimkaribisha Mgeni Rasmi Jaji Mkuu kufungua Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Jinai kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki
Mahakamani uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania jijini Dodoma.
“Kila Taasisi inayohusika katika mnyororo wa haki ina wajibu
wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Maadili ya
utumishi wa umma” amesema Jaji Mruma.
Akifafanua nafasi ya Mahakama katika mnyororo wa haki amesema,
“Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezwa kuwa,
inaipa Mahakama nafasi ya kuwa mamlaka ya mwisho katika kuamua haki za
wananchi, huku akisisitiza kuwa, utoaji wa haki si jukumu la Mahakama pekee,
bali unahitaji ushirikiano wa taasisi zote zinazounda mnyororo wa haki.”
Kaimu Jaji Kiongozi huyo ambaye ameongeza kuwa, wajibu huo
huanza tangu hatua za awali za utekelezaji wa sheria, ikiwemo ukamataji na
upelelezi, uamuzi wa kuwasilisha mashtaka hadi shauri linapofikishwa Mahakamani
na kuamuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Mhe. Mruma amesema kwamba, mkutano huo unalenga
kufuatilia utekelezaji wa mikakati 10 iliyowekwa na Mahakama na wadau wa
mnyororo wa haki katika vikao vilivyopita.
Aidha; ametaja mikakati iliyofikiwa na vikao Mahakama na Wadau hao, miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kila taasisi
inatekeleza jukumu lake ipasavyo kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya
utumishi wa umma; kuheshimu na kulinda hadhi na ukuu wa Mahakama; pamoja na
kuimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau ili changamoto za utoaji wa haki
ziweze kushughulikiwa kwa haraka,” amesema Jaji Mruma.
"Mikakati hiyo pia inahusisha kuimarisha ufuatiliaji wa
mashauri na uwajibikaji kupitia utoaji wa taarifa sahihi na za mara kwa mara,
pamoja na matumizi ya mifumo inayoweza kuwasiliana ili kurahisisha mawasiliano
baina ya taasisi," ameeleza.
Ametaja mkakati mwingine ni kuhakikisha vikao vya
ushirikiano na mahusiano kati ya Mahakama na wadau vinafanyika angalau mara nne
kwa mwaka, kwa lengo la kujadili changamoto na kufuatilia utekelezaji wa
mikakati iliyowekwa.
Vilevile, kila taasisi inayoshiriki katika mnyororo wa haki
imetakiwa kuweka utaratibu mahsusi na madhubuti wa ndani wa kuhakikisha
mikakati hiyo inatekelezwa.
Kuhusu utatuzi wa migogoro, mkutano huo umeeleza umuhimu wa
migogoro ambayo kwa mujibu wa sheria inapaswa kutatuliwa katika ngazi
mbalimbali kwa njia ya madai au kiutawala kushughulikiwa kwanza katika ngazi
husika badala ya kufunguliwa kama mashauri ya jinai moja kwa moja.
Hatua hiyo imehusishwa na dhana ya maridhiano, ambayo
imeainishwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure
Act) kwa makosa yanayoweza kutatuliwa kwa njia hiyo.
Akielezea umuhimu wa mikakati hiyo, Mhe. Mruma amesema
“jambo la msingi si idadi ya mikakati iliyowekwa, bali ni utekelezaji wake na
matokeo yanayopatikana katika mnyororo wa haki jinai nchini.”
Mkutano huo unatoa fursa kwa Mahakama na wadau kutathmini
walikotoka, walipo na wanakokwenda katika utekelezaji wa mikakati hiyo,
sambamba na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na ushirikiano zaidi. Aidha,
utekelezaji wa mikakati hiyo umehusishwa na Dira ya Taifa ya 2050, inayotambua
haki kuwa msingi muhimu katika kujenga jamii yenye maendeleo na ustawi.
Kadhalika, Mkutano huo unatarajiwa kuendelea na majadiliano
kuhusu changamoto mbalimbali zinazokabili mnyororo wa haki na namna ya
kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wake ili kuhakikisha wananchi
wanapata haki kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria.
Sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Haki Jinai wakiwa katika picha ya pamoja. Katikati ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni