Jumamosi, 26 Septemba 2026

MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAPYA YAFUNGWA DODOMA

Na ARAPHA RUSHEKE-MAHAKAMA.

Mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Kada ya wanasheria pamoja na ugavi katika utumishi wa umma, yaliyokuwa yanafanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma, yamehitimishwa leo tarehe 25 Septemba, 2026.

Mafunzo hayo yalifungwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Irene Musokwa. Washiriki wameonesha kuridhishwa na maarifa na ujuzi walioupata katika kipindi chote cha mafunzo.

Katika kipindi cha mafunzo, washiriki walipata fursa ya kujifunza mada mbalimbali kutoka kwa wakufunzi, huku wakishiriki kikamilifu katika mijadala, maswali na kubadilishana uzoefu.

Mijadala hiyo ilitoa nafasi kwa washiriki kuongeza uelewa na kupata maarifa yanayoweza kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mhe. Musokwa aliwahimiza washiriki hao kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa weledi, uadilifu na kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wa umma.

“Nawahimiza kutumia maarifa mliyoyapata kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wa umma,” alisema Mhe. Musokwa.

Kwa niaba ya washiriki, Afisa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Bw. Samweli Banzi, alitoa shukrani kwa uongozi na wawezeshaji kwa kuwawezesha kupata mafunzo hayo, akieleza kuwa yamewapatia maarifa mapya, uelewa mpana na fursa ya kujifunza kupitia uzoefu wa wakufunzi pamoja na majadiliano yaliyofanyika.

Aidha, washiriki walikabidhiwa vyeti, ikiwa ni sehemu ya kutambua ushiriki wao katika mafunzo hayo.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza tarehe 21 Septemba, 2026 yaliandaliwa na kuratibiwa na Chuo cha Uongozi Mahakama Lushoto (IJA), huku wakufunzi kutoka sehemu mbalimbali wakichangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mafunzo hayo, kupitia uwasilishaji wa mada mbalimbali na majadiliano.

Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Irene Musokwa, akiwa ukumbini wakati wa kufunga mafunzo hayo ya washiriki yaliyodumu kwa muda wa siku tano.

Mwezeshaji ambaye ni Mhadhiri kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Bi. Rose Sanga, akifundisha mada ya itifaki kwa washiriki.

Mwezeshaji  ambaye ni Mkurugenzi wa Sheria kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Charles Mulamula, akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.

Mratibu wa Mafunzo hayo na Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Husna Rweikiza (aliyesimama) akiongea jambo wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Irene Musokwa (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo. Aliyeketi kushoto kwake ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Thurstone Kombe na aliyeketi kulia kwake ni Mratibu wa Mafunzi hayo na  Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Chuo cha Mahakama Lushoto, Mhe Husna Rweikiza.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Jamaica.

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni