Jumatano, 30 Septemba 2026

MAHAKAMA NJOMBE YAZINDUA MAJENGO YA MAHAKAMA ZA MWANZO LUILO NA MANDA

  •   Jaji Nongwa asisitiza Utatuzi wa Migogoro kwa njia ya Usuluhishi 

·    Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe imezindua rasmi majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa. Uzinduzi huo uliofanyika tarehe 25 Septemba, 2026 umeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi wa Wilaya ya Ludewa, hususan wakazi wa Tarafa za Masasi na Mwambao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa, aliwataka wananchi kutumia njia za usuluhishi katika kutatua migogoro yao ili kupunguza gharama na muda kwa wadaawa pamoja na Mahakama.

Mhe. Nongwa alisema, Mahakama inaendelea kusimamia sheria ipasavyo na kwamba, baada ya shauri kusajiliwa Mahakamani, Mahakimu wana mamlaka ya kuwaelekeza wadaawa kutumia njia ya usuluhishi kwa mashauri yanayoruhusiwa kisheria.

Aidha, Mhe. Nongwa alirejea hotuba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ya tarehe 17 Septemba, 2026 aliyosistiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi na Utawala ili kupunguza gharama kwa wadaawa na ucheleweshaji mashauri.

 Aliongeza kuwa, hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa mashauri Mahakamani na kuwawezesha wadaawa kupata suluhisho la migogoro yao kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Mhe. Nongwa alisema ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi na kuhakikisha huduma hizo zinatolewa katika mazingira bora.

Alisisitiza kwa kusema, “tukumbuke maendeleo katika Nchi na maeneo yake yote hupimwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kigezo cha uwepo wa huduma bora na za kisasa zilizo karibu na wananchi, huduma za Kimahakama zikiwemo. Tunafahamu Mkoa wa Njombe hususan Wilaya ya Ludewa ina mikakati mingi ya uwekezaji, hivyo majengo haya na huduma bora itakayotolewa na Mahakama itakuwa chachu ya kuendeleza uwekezaji katika Wilaya ya Ludewa na Mkoa wa Njombe kwa ujumla.”

Katika hafla hiyo, Mhe. Nongwa pia alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuiwezesha Mahakama kutekeleza mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama katika Mkoa wa Njombe.

Aidha Jaji Mfawidhi huyo aliwashukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Dkt. John Anthony Jingu pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya kwa jitihada na utashi wao katika kuhakikisha Mkoa wa Njombe unapata majengo ya kisasa ya Mahakama, ikiwemo Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Juma Nyenzi alitoa taarifa kuhusu ujenzi wa majengo hayo, ikiwemo idadi ya ofisi na miundombinu iliyowekwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma.

Bw. Nyenzi alisema kuwa, uwepo wa Majengo ya kisasa kwa Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda utaendelea kujenga imani kwa wananchi na watoa huduma wa Mahakama, huku huduma za utoaji haki zikitolewa katika mazingira bora na yanayokidhi mahitaji ya watumiaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bw. Olvanusi Thomas, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, aliwasisitiza wananchi kuepuka vitendo vya unyanyasaji na kujichukulia sheria mkononi pale wanapokutana na migogoro inayohitaji tafsiri na utekelezaji wa sheria.

Alisema, wananchi wanapaswa kutumia Mahakama na Taasisi nyingine zinazohusika katika kutatua migogoro na kupata haki kwa mujibu wa sheria.

Wananchi wa Tarafa za Masasi, hususan katika Kata za Luilo na Manda, walieleza kufurahishwa na ujenzi wa Mahakama hizo, wakisema umewapunguzia gharama na muda wa kusafiri kufuata huduma za Mahakama.

Wananchi hao walieleza kwamba, kabla ya ujenzi wa Mahakama hizo, baadhi yao walilazimika kusafiri umbali wa takribani kilometa 70 ili kufuata huduma za Mahakama.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali, akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Obadia Bwegoge, Naibu Msajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Njombe, Ludewa, Wanging’ombe na Makete pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.

Akitoa neno la shukrani, Naibu Msajili wa Mhakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Mhe. Joseph Luambano aliwashukuru wadau mbalimbali na hasa Viongozi wa Serikali ya Wilaya ya Ludewa kwa ushirikiano waliouonesha tangu mwanzo wa maandalizi ya ujenzi wa Majengo ya Mahakama, maandalizi ya uzinduzi pamoja kutenga muda wao kushiriki katika uzinduzi. Aidha aliwashukuru watumishi wote wa Mahakama kwa ushiriki wao katika kufanikisha hafla ya uzinduzi wa majengo hayo.

Wageni wengine kutoka Taasisi mbalimbali waliohudhuri ni Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Njombe, Viongozi wa Dini, wadau wengine wa Mahakama vikundi vya ngoma za asili pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ludewa.

Jaji  Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (kulia) akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Luilo na  Manda tarehe 25 Septemba, 2026. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bw. Olvanusi Thomas.

Jaji  Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe,  Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kushoto) pamoja na wenzake wakikagua jengo la Mahakama ya Mwanzo Luilo ambalo lipo Wilaya ya Ludewa. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bw. Olvanusi Thomas na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Juma Nyenzi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa  akizungumza na wananchi (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa iliyofanyika tarehe 25 Septemba, 2026.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph Luambano akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa iliyofanyika tarehe 25 Septemba, 2026.


  Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Bw. Olvanusi Thomas akizungumza na wananchi (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa iliyofanyika tarehe 25 Septemba, 2026.

Wananchi wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri katika uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa tarehe 25 Septemba, 2026.

Burudani ikiendelea kutoka Kikundi cha Ngoma ya Asili aina ya Mganda wa Kinyasa wakitumbuiza mbele ya Viongozi na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo Luilo na Manda katika Wilaya ya Ludewa iliyofanyika tarehe 25 Septemba, 2026.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Obadia Bwegoge akipanda mti wa kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Luilo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)








 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni