Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya
Timu ya
mpira wa miguu ya Mahakama Sports Mbeya imemaliza vyema mchezo wake kwa kuibuka
kidedea kwa ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya Timu ya soka ya Hospitali ya Rufaa Kanda
ya Mbeya, mchezo huo wa gozi la Ng’ombe ulitandikwa katika Uwanja maarufu wa
Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na kuvuta hisia za mashabiki wengi wapenda
kandanda.
Mchezo huo
uliokuwa na ushindani mkali ulianza kwa kasi, huku kila Timu ukionesha dhamira
ya kutawala dimba. Mahakama Sports Mbeya ilifanikiwa kupata bao la kwanza
katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Mchezaji wake Ally Sandali, aliyefungua
ukurasa wa mabao na kuiweka timu yake kifua mbele.
Baada
ya mapumziko, timu ya Mahakama Sports Mbeya iliingia uwanjani kwa morali kubwa
na mchezo uliendelea kwa kasi huku timu zote zikisukuma mashambulizi kutafuta
mabao, ila kutokana na moto mkubwa uliowashwa na Mahakama Sports Mbeya
iliongeza bao la pili kupitia mchezaji wake mahiri Pierregety Kalaghe na
kuimarisha uongozi kwa timu hiyo kwa goli 2 nunge.
Kufuatia
mchezo mzuri Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ilifanikiwa kupata bao moja
la kufutia machozi ambalo lilifungwa kwa ufundi mkubwa na kufanya ubao usomeke
mbili kwa moja, hata hivyo hadi kipyenga cha dakika 90 kinasikika mchezo
umalizika kwa Mahakama Sports Mbeya kuibuka kidedea kwa ushindi wa goli mbili
kwa moja.
Akizungumza
mara baada ya mchezo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya,
Mhe. Fahamu Mtulya, ambaye pia alishiriki katika mchezo huo, kama maestro supa sabu, aliwapongeza
wachezaji kwa kuonesha kiwango kizuri na kuitetea vyema timu yao.
“Hongera
kwa wachezaji ambao wametuheshimisha katika mchezo huu na kuibuka na ushindi
mnono wa goli mbili. Kwa hakika mmecheza vizuri na ninawashauri kujibidiisha
katika mazoezi,” alisema Mhe. Mtulya.
Aidha,
Mhe. Mtulya aliwashukuru watumishi waliojitokeza uwanjani kuipa nguvu timu yao,
huku akitumia fursa hiyo kuhamasisha watumishi kuendelea kujumuika katika
programu za mazoezi zinazofanyika katika viunga vya Mahakama Kuu Mbeya kila
Jumanne na Ijumaa.
Mchezo
huo pia ulihudhuriwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw.
Festo Chonya, pamoja na viongozi na watumishi wengine wa Mahakama wa ngazi
mbalimbali jijini Mbeya.
Ushindi
huo, umeongeza hamasa miongoni mwa watumishi na mashabiki wa Mahakama Sports
Mbeya, huku mchezo huo ukiendelea kuonesha umuhimu wa michezo katika kuimarisha
afya, mshikamano, ushirikiano na mahusiano mema miongoni mwa watumishi.
Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Sports Mbeya (jezi nyeupe) ikimenyana vikali na Timu ya mpra wa miguu ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kutafuta ushindi ndani ya dakika 90 za mchezo katika Uwanja maarufu wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, a.k.a
maestro supa sabu akiwa mchezoni katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine Jijiji
Mbeya.
Sehemu ya Wachezaji wa akiba wa timu ya mpira wa miguu ya Mahakama sports Mbeya wakiwa kwenye benchi la timu hiyo.
Wachezaji wa Mahakama Sports Mbeya wakisikiliza maelekezo ya Mwalimu Bw. Himili Mwaigombe (aliyenyoosha mikono), wakati wa mapumziko baada ya kipindi cha kwanza kumalizika.
Wachezaji
wa timu ya mpira wa miguu ya Mahakama sports Mbeya wakiwa kwenye mazoezi ya
Mwisho “Warm up” kabla ya mchezo huo kuanza.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, (kushoto) maestro
supa sabu akijiandaa kuingia uwanjani wakati wa mchezo huo. Kulia ni Mtendaji
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya.
Wachezaji
wa timu ya mpira wa miguu ya Mahakama sports Mbeya wakiwa kwenye picha ya
Pamoja kabla ya Mchezo huo kuanza
Wachezaji
wa timu ya mpira wa miguu ya Mahakama sports Mbeya wakiwa kwenye mazoezi ya
Mwisho “Warm up” kabla ya mchezo huo kuanza.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni