·
Jaji Mkuu awataka Wadau kuwa huru
kutoa maoni na michango ya kuboresha utoaji haki
·
Asema kipimo cha Kiongozi bora kinapatikana
kwa huduma yake katika jamii
·
Asisitiza utatuzi wa migogoro kwa
njia ya Usuluhishi
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dodoma
Mahakama ya Tanzania
pamoja na Wadau wa Sekta ya Sheria na Uchumi wamekutana kufanya Tathmini ya
Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki,
Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara lengo likiwa ni kuboresha ufanisi
katika mnyororo wa haki za kiuchumi sambamba na kuoanisha utendaji kazi na Dira
ya Taifa ya Maendeleo, 2050.
Akifungua Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya
Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara leo tarehe
16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano- Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
George Masaju amewasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kuwa huru kutoa maoni na
changamoto zilizopo zikiwemo zinazoigusa Mahakama ili kuboresha uwazi na
uwajibikaji katika utoaji haki nchini.
“Mkutano huu una mambo
mazuri tu yanayotusaidia kuboresha ufanisi katika maeneo yetu ya kazi kwa jinsi
yanavyohusiana na kuuwiana na mnyororo wa haki jinai, haki inaweza kuwa ni haki
jinai au katika muktadha wa kikao hiki cha mashauri ya kiuchumi. Kwahiyo
nawashauri kwamba muwe huru kabisa mnavyoshiriki mkutano huu. Wengi wenu
nawafahamu ninyi tu si kwamba ni viongozi lakini ni wataalamu mahiri katika
maeneo yenu, hivyo tunategemea kupata ushirikiano wenye tija kwa sababu ya
uwepo wenu,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu
amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, umuhimu wa kiongozi haupatikani kwa Kiongozi
kuwa ofisini pekee bali umuhimu wake unapatikana kwa huduma yake anayotoa
katika jamii.
Mhe. Masaju amesema, nafasi
na mchango wa Mahakama na Wadau katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba na
kisheria katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu.
“Msingi Mkuu wa Dira hii
ni Taifa Jumuishi lenye Ustawi, Haki na Linalojitegemea.Kwahiyo tunavyokaa hapa
sasa pamoja na Mikakati hii tuliyokwishajiwekea tuweke au tupendekeze mikakati
ya kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa utekelezaji
wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inamhususu kila mmoja wetu hapa. Kwa hiyo
hiki kikiwa ni kikao cha tatu tunakutana ili kutathmini utekelezaji wa mikakati
ya pamoja ya kushughulikia mashauri ya kodi, biashara, ardhi, mabenki na
ushindani wa kibiashara,” ameeleza Jaji Mkuu.
Ameongeza kuwa, pamoja na
kutathmini utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea, Mkutano huo pia ni fursa ya
kujadili masuala mengine yanayoweza kujitokeza baada ya kikao kilichopita na
yale yanayoweza kujitokeza siku za mbeleni ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji
wa mikakati iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na Wadau.
“Mnapokuwa
mmerejea katika Ofisi zenu muende mkayatekeleze haya lakini pia muwashauri
viongozi wenu umuhimu wa kuyatekeleza hayo,” amesisitiza Mhe. Masaju huku
akigusia juu ya umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi akirejea
Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo
Mahakama inahimizwa kukuza usuluhishi na kuzikumbusha Taasisi nyingine kuwa, zinapaswa
kwanza kutatua migogoro kabla ya kufikisha mashauri mahakamani.
“Naomba
niwarejeshe katika mkakati wa sita na wa kumi katika mikakati yetu inayohusu
utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. Lakini pia kwa njia za kiutawala
katika maeneo yetu ya kazi. Na hili sharti ni sharti la kikatiba linatokana na
ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Mahakama
inapotekeleza jukumu lake la kutoa maamuzi katika mashauri ya madai na jinai
inatakiwa pia kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya watu wanaohusika katika
migogoro,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Kadhalika,
Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia Mawakili
wake kuwasimamia wateja wao kwa maadili na kuwashauri kutumia mifumo ya
usuluhishi na mamlaka za udhibiti badala ya kukimbilia mahakamani. Hatua hiyo
inalenga kuepuka gharama zisizo za lazima na mapingamizi ya kisheria
(preliminary objections) lakini vilevile ni utekelezaji wa Kanuni ya 59 ya
Kanuni za Maadili ya Mawakili, 2018 Tangazo la Serikali Na. 118 la 2018 inayoelekeza
Mawakili kuwataarifu Wateja wao kuhusu uwezekano na faida za kumaliza mashauri
kwa mfumo wa usuluhishi
Akizungumzia kuhusu Uhuru
wa Mahakama na Usimamizi wa Sheria; Mhe. Masaju amesema, kwa mujibu wa Ibara ya
107B ya Katiba, Mahakama itaendelea kuwa huru na kusimamia sheria huku
akibainisha kuwa, mashauri ambayo hayakufuata taratibu za awali za kupatiwa
ufumbuzi kwanza katika mamlaka husika kabla ya kuzihusisha Mahakama yatarejeshwa
kwenye mamlaka husika.
“Na sisi huku mahakamani
tutaendelea kusimamia sheria kwa ufanisi ipasavyo. Kwa sababu hata hivyo ni
sharti letu la jukumu letu la kikatiba katika ibara ya 107B kwamba katika
kutekeleza majukumu yetu Mahakama itakuwa huru isipokuwa itazingatia tu
masharti ya Katiba na Sheria za Nchi,” ameeleza Jaji Mkuu.
Kupitia mkutano huo,
Mahakama na Wadau hao wataendelea kubainisha changamoto zilizosababisha
ucheleweshaji au zinazosababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya
kiuchumi na kuendelea kutekeleza ipasavyo mikakati iliyowekwa na mingine
itakayokubalika katika Mkutano huo.
Mkutano huo umehudhuriwa
na Amidi wa Mahakama Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Jaji Amir Mruma, Majaji Wafawidhi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma
Maghimbi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, Mahakama Kuu
Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki
Nkya, Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na baadhi ya Naibu
Wasajili kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na
Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.
Wadau wengine
waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe na wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Tume ya Taifa ya
Mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum
ya Kiuchumi (TISEZA), Msajili wa Baraza la Ushindani.
Wengine ni kutoka Chama
cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Umoja wa Mabenki (TBA), Chama cha Madalali na
Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Baraza la Ushindani, Benki ya Taifa ya Biashara
(NBC).
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiongoza Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni