●
Mahakama yasema ufanisi wa utoaji haki ni muhimu katika
kukuza uchumi,
●
Yabainisha changamoto za matumizi mabaya ya Akili Unde na
nyingine zinazokwamisha utoaji haki ipasavyo
Na HALIMA MNETE- Mahakama Dodoma
Mahakama ya Tanzania
imeeleza mikakati mbalimbali inayochukua katika kuimarisha utoaji haki na kuongeza
ufanisi wa kushughulikia mashauri, huku ikibainisha changamoto zinazojitokeza
katika utekelezaji wa mikakati ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Akiwasilisha Taarifa ya Mahakama Kuhusu Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji katika Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, amesema Mahakama imeendelea kutekeleza mikakati iliyowekwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na wadau wa mnyororo wa haki.
Mhe. Nkya amesema mikakati hiyo ambayo idadi yake imefikia 10, mikakati nane inahusu Mahakama na wadau kwa pamoja, huku miwili ikiwahusu wadau pekee.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2026 Mahakama imekamilisha utekelezaji wa hukumu katika mashauri 1,290, huku kati ya Juni na Agosti, mwaka huu kukiwa na maombi 207 ya utekelezaji katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Aidha, Msajili Mkuu amesema, Mahakama imeendelea kuimarisha mawasiliano na wadau kupitia vikao vya (Bench-Bar), ambapo mwaka huu vikao 17 vimefanyika katika Mahakama Kuu, 23 katika Mahakama za Hakimu Mkazi na 115 katika Mahakama za Wilaya.
Katika upande wa usikilizaji wa mashauri, Mhe. Nkya anabainisha kuwa, Mahakama katika ngazi zake mbalimbali ilisikiliza jumla ya mashauri 101,879 kati ya 170,059 yaliyofunguliwa katika kipindi husika. Amesema, uwezo wa Mahakama kumaliza mashauri umefikia asilimia 95 ya idadi ya mashauri yanayofunguliwa.
Kwa upande wa mashauri ya madai, Mhe. Nkya ameeleza kwamba, jumla ya 69,911 yalisikilizwa kati ya 74,514 yaliyofunguliwa, huku mashauri 23,850 yakiwa bado Mahakamani na 1,913 yakitajwa kuwa mlundikano.
Mhe. Nkya pia amesema kuwa, Mahakama imeendelea kuhimiza matumizi ya njia za usuluhishi katika kutatua migogoro. Katika kipindi cha Juni hadi Agosti, mashauri 151 yalifanyiwa usuluhishi katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
“Kati ya Januari na Agosti, mwaka huu Mahakama Kuu ilimaliza mashauri 181 kwa njia ya usuluhishi, Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama Kuu kikamaliza 283, Mahakama za Hakimu Mkazi 141 na Mahakama za Wilaya 200,” ameeleza.
Msajili Mkuu huyo ameongeza kuwa, Mahakama imeweka mikakati maalum ya kushughulikia mashauri ya kimkakati ambapo Mahakama ya Rufani imepanga mashauri 300 kwa ajili ya kikao kijacho, wakati Mahakama ya Ardhi imeanza kikao maalum tangu Agosti 24 kinacholenga kumaliza mashauri 399.
Aidha, Mahakama ya Biashara imeanza kikao maalum kinacholenga kumaliza mashauri 88, huku wadau wakitakiwa kutoa ushirikiano ili mashauri hayo yakamilishwe kwa wakati.
Mhe. Nkya ameongeza kuwa, Mahakama imewezesha utekelezaji wa hukumu za mashauri 532 ya Ardhi, Biashara, Kibenki, Hifadhi ya Jamii, Kazi na Madai.
Katika upande wa matumizi ya Akili Unde, Mhe. Nkya anasema miongoni mwa changamoto alizozitaja ni matumizi yasiyofaa ya Akili Bandia (AI) na baadhi ya Mawakili kutumia katika maandalizi ya nyaraka za mashauri.
“Tayari kumekuwa na matukio kadhaa ambapo kuna hukumu ambazo hazipo zimetengenezwa kwa kutumia Akili Unde na kuwasilishwa Mahakamani kama nyaraka halisi,” amesema Mhe. Nkya na kuongeza kuwa, baadhi ya waliohusika wamechukuliwa hatua wakiwemo waliopewa onyo.
Msajili Mkuu ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na matumizi mabaya ya Kanuni 96 (7) inayoruhusu kurekebisha nyaraka za rufaa zikiwa na mapungufu, Mashauri ambayo yanatakiwa kuanza katika mamlaka nyingine kufunguliwa kwanza mahakamani, Mawakili kufungua maombi rasmi hata katika masuala ambayo wangeweza kuomba wakati shauri linaendelea mfano application for dismissal of the pending case, Baadhi ya mabenki, yanapopokea amri ya kukamata fedha (Garnishee Order Nisi).
Aidha, Mhe. Nkya ameeleza kuwa, ufanisi wa utoaji haki ni sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Maendeleo, 2050 huku akitoa wito kwa Mahakama na wadau wote wa mnyororo wa haki kuendelea kushirikiana katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya akiwasilisha Taarifa ya Mahakama Kuhusu Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau Wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji wakati wa Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika Mkutano kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati kwa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji katika Mkutano wa Wadau hao uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.
Sehemu ya Majaji na Wadau wa Mahakama waliohudhuria katika Mkutano wa Wadau wa Mashauri ya Ardhi, Kodi, Biashara, Mabenki, Ushindani wa Kibiashara na Uwekezaji uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni