Ijumaa, 9 Oktoba 2026

DKT. MAMBI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA MANYARA

Na CHRISTOPHER MSAGATI - Mahakama, Manyara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella ofisini kwake jana tarehe 08 Oktoba, 2026 kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali ambayo yanahusu ushirikiano wa kikazi kati ya Mahakama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Dkt. Mambi alimshukuru Mhe. Shigella kwa kumkaribisha ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo, kufahamiana na kujadiliana juu ya utendaji kazi na ushirikiano unaopaswa kuwepo baina ya Ofisi hizo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alimuomba Mkuu wa Mkoa huyo aweze kusaidia katika suala la upatikanaji wa viwanja kila Kata za Mkoa wa Manyara kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

“Kwa kuwa huduma za Mahakama zinaendelea kukua kila siku, tunaomba utusaidie katika michakato mzima wa kupata viwanja pamoja na hati za umiliki katika Kata ambazo hamna huduma za Mahakama ili tuweze kujenga Mahakama hizo na kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Kwa upande wake, Mhe. Shigella alimuahidi Mhe. Dkt. Mambi kutekeleza jukumu hilo kwa kuwasiliana na mamlaka zilizopo chini yake ili viwanja hivyo vipatikane ili kukidhi adhima ya Mahakama ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

“Ninatambua kuwa, Mkoa wetu wa Manyara una changamoto ya uhalifu na hususan mashauri ya kijinsia, na migogoro ya ardhi na kwa sababu hiyo ni kweli kila mahali panahitaji kufikiwa na huduma hizi za Mahakama. Kwa sababu hiyo Mhe Jaji nitajitahidi kuwasiliana na viongozi wa Mamlaka nyingine ili tufanikiwe katika upatikanaji wa viwanja na hati hizo,” alisema Mhe. Shigella.

Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hawa wawili kukutana na kufanya mazungumzo tangu ambapo Mhe Shigella alipohamishiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Manyara ambapo awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita mnamo Mwezi Septemba, 2026 akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga aliyehamishiwa Mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mambi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava, Naibu Msajili anayefanya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Mariam Lusewa na Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama alioambatana nao kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella (katikati).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia) akizungumza na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella mara baada ya kumtembelea ofisini jana tarehe 08 Oktoba, 2026.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Charles Mnzava akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella.

Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemed (kushoto) akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella. Wengine ni Mhe. Ashery Stanley (katikati) na Mhe. Kuruthumu Mkundawatu (kulia) ambao skwa pamoja ni Mahakimu Wakazi na Wasaidizi wa Sheria wa Jaji.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella mara baada ya kumtembelea katika ofisini kwake.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Mariam Lusewa akifuatilia mazungumzo kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigella.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha & James Busanya - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni