Na. FRANCISCA SWAI - Mahakama, Musoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Musoma, Mhe. Edwin Kakolaki, amepogeza watumishi wa Mahakama Musoma
kwa utendaji kazi mzuri wa kuridhisha pamoja na utunzaji mzuri wa mazingira na
maeneo ya Mahakama.
Mhe. Kakolaki alitoa
pongezi hizo katika kikao cha Menejimenti kilichofanyika hivi karibuni katika
ukumbi wa Halmashauri ya Mji wilayani Tarime.
Pamoja na pongezi
hizo, Mhe. Kakolaki alisisitiza watumishi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni
katika utumishi wa umma, zinazotoa miongozo mbalimbali ya namna ya kuenenda na utendaji
kazi wa kila siku.
Alisisitiza pia kila
Mahakama Musoma kuendelea kuchukua tahadhari muhimu juu ya mvua kubwa za El-nino
zinazotarajiwa kunyesha ili kuhakikisha majengo, majalada na mali za Mahakama
zinakuwa salama.
Aidha, taarifa
mbalimbali za utendaji kazi katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka
2026/2027 ziliwasilishwa na wajumbe wanaounda kikao hicho kutoka Mahakama Kuu
Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Mahakama za Wilaya za Musoma,
Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya.
Akiongea katika kikao
hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Musoma, Mhe. Omari Kingwele, alisisitiza
watumishi wote kutunza maadili yao ya kazi na kufanya kazi kwa uadilifu na
weledi, kwani kwa kufanya hivyo wanajihakikishia usalama wa kazi zake wenyewe.
Pia alisisitiza
usikilizaji wa mashauri kwa wakati ili kuepuka mlundikano, pamoja na
kuhakikisha Mahakama Musoma inavuka mwaka bila mashauri yanayobaki kwa mwaka
husika.
Naye Mtendaji wa Mahakama
Musoma, Bw. Leonard Maufi, alielezea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika
miradi inayoendelea ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya Tarime, Serengeti na
Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo iliyoko wilayani Rorya. Aidha, alisisitiza
watumishi kuendelea kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za kazi.
Naye Mkaguzi wa Ndani,
Bw, Andala Nyakuwa, akiwasilisha taarifa yake katika kikao hicho, alisema kila
kazi au malipo yanayofanyika ndani ya Mahakama lazima yaonyeshe matokeo chanya.
Pia alisisitiza
umuhimu wa ukaguzi wenye malengo wa Mahakama za chini, utekelezaji wa kanuni
mpya katika ushughulikiwaji wa malipo ya mirathi pamoja vikao kazi ndani ya Masjala
Ndogo Musoma, kwani ndio vinavyowezesha ufanisi katika kazi.
Pamoja na taarifa
hizo za utendaji kazi, zilitolewa taarifa za kijamii zilizohusu Mfuko wa Maafa na
taarifa ya utalii wa ndani uliofanyika mwezi Agosti 2026, ambapo watumishi
walitembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire pamoja na maji moto chemka.
Akihitimisha kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwaasa wajumbe kufanyia kazi yale waliyokubaliana, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari juu ya mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha za El Nino.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Musoma, Mhe. Edwin Kakolaki,
akizungumza wakati anafungua kikao cha Menejimenti.
Naibu Msajili wa
Mahakama Musoma, Mhe. Omari Kingwele, akiongea na wajumbe wa kikao cha
Menejimenti (hawako pichani).
Mtendaji wa Mahakama Musoma,
Bw. Leonard Maufi, akiongea na wajumbe wa kikao hicho.
Mkaguzi wa Ndani
Mahakama Kuu Musoma, Bw. Adala Nyakuwa (aliyesimama) akiwasilisha mada wakati
wa kikao.
Wajumbe wa kikao cha
Menejiment wakifuatilia kwa makini taarifa zinazowasilishwa katika kikao hicho.
Watumishi wa Mahakama
Kanda ya Musoma wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara ya utalii katika
Hifadhi ya Taifa Tarangire iliyoko mkoani Arusha.
Sehemu ya
Watumishi wa Mahakama Musoma wakifurahia mandhari nzuri ya ChemkaHot Spring
iliyoko mkoani Arusha.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni