Na
HABIBA MBARUKU-Mahakama Dodoma
Jaji
Mkuu wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, pamoja na ujumbe wake leo tarehe 12
Oktoba, 2026 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma na
kujionea hatua kubwa zilizopigwa katika utoaji haki nchini, ikiwemo matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ujenzi wa miundombinu ya kisasa
inayorahisisha utendaji wa Mahakama huku ikitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.
Alipowasili
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zeija alipokelewa na Jaji Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa pamoja na Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. John Jingu pamoja na Wajumbe wa
Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.
Katika
ziara hiyo, ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea ukumbi mpya wa kisasa wa
Mahakama ya Tanzania, pamoja na Chumba Maalum cha
Usimamizi wa Taarifa za Mahakama (Judiciary
Situation Room) kinachotumika kufuatilia na kuratibu shughuli za Mahakama
nchi nzima.
Aidha,
ugeni huo ulipata nafasi ya kufanya majadiliano na kubadilishana uzoefu juu ya
matumizi ya TEHAMA, pamoja na kufahamu mifumo mbalimbali inayotumiwa na
Mahakama katika kufanikisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo ambapo Mkurugenzi
wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso, aliwasilisha
mada iliyoeleza muundo, dira, na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa
na Mahakama ya Tanzania.
Akiwasilisha Muundo wa Mahakama, Bw. Uisso amebainisha kuwa, mfumo wa Mahakama nchini
umejengwa katika ngazi kuu nne kuanzia Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya
na Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu yenye divisheni maalum ambazo ni Divisheni ya Kazi,
Ardhi, Biashara, Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, hadi Mahakama ya Rufani
ambayo ndiyo ngazi ya juu kabisa ya Mahakama.
Bw. Uisso ameeleza kuwa, Mahakama inatekeleza azma yake ya kutoa haki sawa kwa wote
mapema ipasavyo kupitia teknolojia, ikiongozwa maadili ya msingi, ambayo ni
uadilifu, kutokuwa na upendeleo, uwajibikaji, uwazi, na utaalamu kupitia
uadilifu, uwazi, na uwajibikaji, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni kuwaweka
wananchi mbele (citizen-centric) ili kujenga imani ya umma.
“Tunatazamia
kutoa haki kwa wote kupitia teknolojia, na mwelekeo wetu uko kwa wananchi,
yaani unaoweka wananchi mbele (citizen-centric). Hilo ndilo lengo letu,
kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kile wanachokitazamia kutoka kwetu,
tunajikita sana katika kujenga imani ya umma, kwa sababu kama huna imani ya
umma, basi watu hawawezi kutumia au kupata kile wanachokitazamia kutoka kwetu,” ameeleza
Bw. Uisso.
Akizungumza
kuhusu mageuzi ya Mahakama, Bw. Uisso ameeleza kuwa mageuzi ya Mahakama yalianza
takribani miaka 10 iliyopita, yaani mwaka 2015 ambapo kuanzia mwaka huo
Mahakama imemaliza mpango wa mageuzi ya sekta ya sheria, uliokuwa ukijumuisha Taasisi
zote za sekta ya sheria kwa kuongozwa na Wizara, jambo ambalo limeonesha
mafanikio kwa Mahakama.
Ameeleza
kuwa, eneo lililopewa kipaumbele katika mageuzi ni mabadiliko ya kidigitali
ambapo Mahakama ilihakikisha inafanya shughuli za ke kidigitali kwa kujenga
mifumo kama vile mfumo wa usimamizi wa mashauri, Mahakama Mtandao Pamoja na
mfumo wa kufuatilia takwimu za kiutendaji za Mahakama.
Ameongeza
kuwa, eneo lingine lililopewa kipaumbele ni mageuzi ya kisheria na kiutaratibu,
ambapo kanuni na taratibu zilianza kurahisishwa pia uanzishaji wa kanuni za
ufunguzi wa mashauri kwa njia ya mtandao kanuni za uendeshaji wa mashauri kwa
mtandao ili kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao.
Aidha,
kipaumbele cha miundombinu ya Mahakama ambapo Mahakama imefanikiwa kujenga
Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, Mahakama za Hakimu Mkazi, Pamoja na ukarabati
wa majengo ya Mahakaman nchi nzima, sambamba na kuimarisha rasilimali watu kwa
kuanzisha mafunzo ili kukuza ujuzi na kuboresha mazingira ya kazi kwa kutoa
vifaa vya kufanyia kazi, kuwezesha usafiri kwa wafanyakazi.
Sambamba
na hayo, Bw. Uisso ameyataja mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni ujenzi wa Vituo
Jumuishi vya Utoaji Haki 15 nchi nzima, ambavyo vinakusanya huduma
zinazopatikana katika ngazi zote za Mahakama chini ya pamoja.
Ameyataja
Mafanikio mengine kuwa, ni Matumizi ya TEHAMA yanayohusisha matumizi ya Mfumo
wa Kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (e-case management),
usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (virtual hearings), na mfumo
wa kurecord kumbukumbu kidijiti ili kuongeza uwazi na ufanisi pamoja na kujenga
uwezo wa rasilimali watu kupitia mafunzo endelevu kwa watumishi ili kuendana na
mabadiliko ya kiteknolojia.
Bw. Uisso amefafanua kuwa, katika miundombinu ya TEHAMA kuna intaneti ya mkongo wa
baharini yenye kasi ya gigabiti 1.28 kwa sekunde pia mtandao wa nyuzi za fiber
(fiber cable) ambao sasa umefika zaidi ya kilomita 7,000 na unafika hadi kwenye
makao makuu ya kila wilaya kwa sasa, kwa hiyo inapatikana vizuri, lakini pia
inaunganisha baadhi ya nchi jirani ikiwemo Uganda.
Akihitimisha
wasilisho lake, Bw. Uisso amesema kuwa katika muelekeo wa Dira 2050, Mahakama
ina mpango wa maendeleo wa miaka mitano, mfumo wa kimakakati wa Uchumi wa
kidigitali ambayo yatalisha sheria za kitaifa za TEHAMA ambapo ipo Sheria ya
Serikali ya Mtandao , Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, pamoja na sheria nyingine
zinazosimamia sekta hiyo, ambazo zitaielekeza Mahakama, kufaidika na mipango
hiyo, hasa mpango mkakati, pamoja na sera ya TEHAMA huku akiongeza kuwa
maboresho haya ya Mahakama yanaingiliana kwa karibu na Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara na jamii yenye haki, amani na
utawala bora.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, ameelezea mifumo
mbalimbali ya Mahakama na namna inavyofanya kazi kieletroniki ikiwa ni pamoja
na mifumo ya e-Case Management, Virtual Court pamoja na namna Chumba Maalum cha
Usimamizi wa Shughuli za Mahakama (Judicial Situation Room) kinavyofanya kazi
kama Data Hub.
Katika ziara hiyo ambayo Mhe. Dkt. Flavian Zeija, ameambatana na baadhi ya Viongozi wa Mahakama Uganda ambao ni pamoja na Maureen Kasande, Ssinabulya Joseph pamoja na Oryema Brian.
Ziara hiyo imethibitisha ushirikiano madhubuti
wa kisheria na kimahakama kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku
Uganda na Tanzania zikishirikiana kubadilishana uzoefu katika uboreshaji wa
mifumo ya utoaji haki kwa wananchi.
Mkurugenzi
wa Mipango na Uratibu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uisso (kulia), aliwasilisha
mada iliyoeleza muundo, dira na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutekelezwa
na Mahakama ya Tanzania.

























Hakuna maoni:
Chapisha Maoni