Jumatatu, 19 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU GEITA YAWAPONGEZA WALIOSHIRIKI MICHEZO YA SHIMIWI

Na INNOCENT MWANDOJE-Mahakama, Geita

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, imewapongeza watumishi walioshiriki katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kufanya vizuri na kuwawakilisha vyema.

Pongezi hizo zimetolewa kwenye hafla maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kutambua juhudi, ushiriki na mafanikio ya watumishi hao katika mashindano hayo ya michezo. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mafunzo uliopo katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Geita.

Miongoni mwa watumishi hao ni Bi. Zainabu Abdallah, baada ya kuibuka bingwa wa mbio fupi za mita mia mbili, Bi. Philipina Katunzi baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika mchezo wa kuvuta kamba upande wa wanawake na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Jacob Shayo, mmoja wa wawakilishi kutoka Geita.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Griffin Mwakapeje, aliwapongeza watumishi hao kwa juhudi walizozionesha wakati wa mashindano na kwa kuiwakilisha Mahakama Kuu Geita kwa heshima na mafanikio.

Mhe. Mwakapeje alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushiriki, kujituma na moyo wa kuiwakilisha Taasisi katika mashindano ya michezo ya watumishi wa Serikali. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo kwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuongeza ufanisi na kujiandaa vizuri zaidi kwa mashindano yajayo.

“Hongereni sana kwa kufanya vizuri katika mashindan ya SHIMIWI. Tunaomba muendelee kufanya mazoezi ili kuongeza ufanisi zaidi,” alisema Mhe. Mwakapeje.

Aliongeza kuwa michezo ina nafasi muhimu katika kuimarisha afya za watumishi, kujenga mshikamano, kuongeza ushirikiano na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya watumishi ndani ya Taasisi.

Aidha, alisema kuwa ushiriki katika michezo hutoa fursa ya kuonesha vipaji, kukuza nidhamu na kujenga ari ya kufanya kazi kwa pamoja katika kufikia malengo ya Taasisi.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa watumishi kuendelea kuitumia michezo kama sehemu ya kujenga umoja na kuimarisha mahusiano kazini, huku wakidumisha bidii na kujituma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya utoaji huduma za haki kwa wananchi.

Kwa upande wao, wawakilishi wa watumishi walioshiriki katika mashindano ya SHIMIWI waliishukuru Mahakama Kuu Geita, kwa kutambua mchango wao na kuandaa hafla maalumu ya kuwapongeza.

Walisema kuwa kutambuliwa kwa juhudi zao ni jambo linalowapa motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi katika michezo na kulitangaza vyema jina la Mahakama Kuu Geita katika mashindano yajayo.

Aidha, waliwahakikishia viongozi wa Mahakama kuwa wataendelea kufanya mazoezi kwa bidii, kuimarisha ushirikiano miongoni mwao na kuongeza maandalizi ili kuboresha kiwango chao cha ushindani na kupata mafanikio makubwa zaidi katika mashindano yajayo ya SHIMIWI.

Wawakilishi hao pia walieleza kuwa michezo ni fursa muhimu ya kujenga urafiki, mshikamano na ushirikiano baina ya watumishi, mambo ambayo yanaweza kuchangia kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Hafla hiyo ya pongezi imekuwa ishara ya kuthamini juhudi na mafanikio ya watumishi hao, huku ikitoa hamasa kwao kuendelea kujituma, kudumisha nidhamu na kuimarisha ushirikiano katika michezo na katika utendaji wa kazi.

Watumishi walioiwakilisha Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita wakikata keki ya pamoja iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwapongeza mara baada ya kuiwakilisha vyema Mahakama Kuu Geita.

Picha ya pamoja ya watumishi walioiwakilisha Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita katika mashindano ya SHIMIWI kwa mwaka 2026.

Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita Mhe. Griffin Mwakapeje, akimvalisha medali ya dhahabu, Bi. Zainabu Abdallah, baada ya kuibuka bingwa wa mbio fupi za mita mia mbili.

Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Geita Mhe. Griffin Mwakapeje, akimpongeza Bi. Philipina Katunzi baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika mchezo wa kuvuta kamba upande wa wanawake.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Mhe. Jacob Shayo, mmoja wa walioiwakilisha Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita katika mashindano ya SHIMIWI 2026 akitoa maneno ya shukurani kwa viongozi pamoja na watumishi wote kwa mapokezi mazuri walipowasili kituoni baada ya mashindano kumalizika.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni