Ijumaa, 9 Oktoba 2026

MAHAKAMA KUU MOROGORO YAFANYA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA MADAI

Na DIANA MOYO-Mahakama, Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Morogoro, hivi karibuni ilifanya kikao cha robo ya tatu ya mwaka 2026 na Wadau wa Haki Madai (Bench Bar Meeting).

Kikao hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ebrahimu. Kilihudhuriwa na viongozi wa Mahakama, wakiwemo Naibu Wasajili na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Wadau waliohudhuria ni Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Wenyekiti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Mawakili wa Kujitegemea na Mwakilishi wa Maadalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama. 

Katika taarifa yake, Naibu Msajili wa Mahakama, Mhe. Amir Msumi, alibainisha kuwa, kwa sasa kuna jumla ya mashauri 171 ya madai yanayoendelea. Kati ya hayo, mashauri ya ardhi ndiyo yanayoongoza yakiwa 90, huku kukiwa na mashauri mawili yaliyoko kwenye mlundikano.

Takwimu za kuanzia Januari hadi Juni 2026 zinaonyesha maendeleo chanya, ambapo mashauri 276 yaliamuliwa, ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na mashauri 222 yaliyosajiliwa katika kipindi hicho. 

Ili kuendelea kuimarisha utoaji wa haki kwa wakati, kikao kiliweka mikakati mbalimbali ikiwemo usimamizi thabiti wa maandalizi ya awali kabla ya usikilizaji, utatuzi wa haraka wa maombi na mapingamizi, pamoja na kuwasilishwa  mapema kwa kumbukumbu za mashauri kutoka Mabaraza ya Ardhi na Nyumba. 

Mbali na hayo, wadau walijadili changamoto za utekelezaji wa baadhi ya maamuzi ya Mahakama na kuazimia kuandaa kikao cha pamoja cha majadiliano na wadau mbalimbali, hasa Idara ya Ardhi ili kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa tuzo na amri mbalimbali zinahitaji huduma ya ofisi zao.

Jaji Mfawidhi alisisitiza kuwa Madalali ni Maafisa Utekelezaji wa Mahakama (Executing Officers) wanapaswa kupata ushirikiano kutoka kwa wadau ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati tarajiwa.

Alihitimisha kikao hicho wa kuwashukuru wajumbe wote kwa ushirikiano mkubwa wanaoonesha kwa Mahakama ili kutimiza lengo kuu la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Rose Ebrahi, akiongoza kikao cha Wadau wa Haki Madai.

Naibu Msajili wa Mahakama, Mhe. Amir Msumi akiwasilisha taarifa ya mashauri kwenye kikao hicho.

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni