- Watumishi wapatiwa mafunzo ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na namna bora ya kushughulikia malalamiko
Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe kwa
kushirikiana na Benki ya NMB-Tawi la Njombe, imeendesha mafunzo maalum kwa Watumishi
wa Mahakama kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja na namna ya kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kuwahudumia wateja.
Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni ikiwa ni
sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, yakiwa na lengo la kuongeza
uelewa, kubadilishana uzoefu na kuwajengea watumishi uwezo wa kutoa huduma bora
mapema ipasavyo na kwa weledi.
Mratibu wa mafunzo hayo, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa
Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Elisha Mwasomola aliwakaribisha
watumishi wote waliohudhuria na kuwatambulisha Maofisa kutoka Benki ya NMB
waliokuwa wamealikwa kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa Mahakama
Njombe pamoja na wengine kutoka Wilaya mbalimbali walioshiriki kwa njia ya
mtandao, hatua iliyowezesha watumishi wengi zaidi kunufaika na maarifa
yaliyotolewa.
Akitoa neno la utangulizi, Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano alisisitiza juu
ya umuhimu wa watumishi kutoa huduma bora kwa wateja wote wanaofika Mahakamani
kupata huduma mbalimbali.
Alieleza kuwa, huduma kwa wateja ni sehemu muhimu ya
utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na kwamba kila mteja anapaswa kuhudumiwa
kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha anaridhika na huduma anayoipata.
“Tunawahudumia wateja mbalimbali wanaohitaji huduma
za Mahakama. Hivyo, tunapaswa kuhakikisha tunatoa huduma kwa kiwango cha juu
ili wateja wetu waridhike. Mahakama inaelekezwa kutoa huduma bora, na msingi wa
maelekezo hayo unatokana na mkataba wa huduma tuliojiwekea na wateja wetu,”
alisema Mhe. Luambano.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa aliyekuwa
mgeni mzungumzaji katika mafunzo hayo, aliwakaribisha Wawezeshaji wa mafunzo
hayo na kusisitiza kwamba, mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kujifunza na
kubadilishana uzoefu katika kuboresha huduma kwa wateja.
Aidha, alibainisha
kuwa, kitengo cha huduma kwa wateja ni kielelezo cha taswira ya taasisi, kwani
namna mteja anavyopokelewa inaweza kuathiri mtazamo wake kuhusu ubora wa huduma
zinazotolewa na taasisi husika.
“Ningependa wote tutambue kuwa, huduma kwa mteja ni zaidi ya kujibu
maswali badala yake, inahusisha pia namna maswali hayo yanavyojibiwa kwani,
wakati mwingine mteja haulizi swali ili apate jibu sahihi pekee, bali anataka
kuona shida yake imepokelewa kwa uzito upi na ni kwa namna gani yeye amejaliwa
na mtoa huduma. Kwa sababu hiyo, kila mmoja wetu akitekeleza wajibu wake wa
kutoa huduma bora kwa wateja, imani ya wananchi kwa Mahakama itazidi kuongezeka,” alisema Mhe. Nongwa.
Aidha, Mhe. Nongwa alieleza kwamba, huduma kwa
wateja ni muhimu sana kwa kuwa inajenga imani ya wananchi (wateja) kwa taasisi,
inapunguza malalamiko na kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi na wadau wake.
Akizungumza kwa niaba ya Benki ya NMB, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi.
Regina Kavishe aliishukuru Mahakama kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika
mafunzo hayo na kueleza kuwa, huduma kwa wateja ni jukumu linalohitaji
kujituma, uvumilivu na moyo wa kujali mahitaji ya wengine. Kwa sababu hiyo,
alieleza, watumishi wanapaswa kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kutafakari
namna wanavyotekeleza majukumu yao na kutafuta njia bora za kuongeza thamani
katika huduma wanazozitoa kila siku.
Bi. Kavishe alifafanua kuwa, huduma ina sifa ya
kutokushikika, kutokutenganishika na mtoa huduma na kutohifadhika kwa ajili ya
matumizi ya baadaye. Aidha, alisisitiza kwamba, ili kutoa huduma bora mtumishi
anapaswa kumkaribisha mteja vizuri, kumsikiliza kwa makini hadi amalize kueleza
mahitaji yake, kumuelewa, kutafakari hatua zinazofaa kuchukuliwa, kutekeleza
majukumu kwa wakati na kutoa mrejesho kwa mteja.
Naye Mshauri wa Ubora wa
Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, alieleza kuwa
huduma bora kwa mteja ni kumhudumia mtu kwa namna ambayo mtumishi mwenyewe
angependa kuhudumiwa.
Bw. Luhwago alielezea kwa kina hatua zinazopaswa
kufuatwa katika kushughulikia malalamiko ya wateja. Alizitaja hatua hizo kuwa ni
pamoja na kupokea malalamiko, kumsikiliza mlalamikaji kwa makini na kumpa muda
wa kueleza tatizo lake, kuandika malalamiko, kufanya tathmini, kuwasilisha malalamiko
katika Idara/kitengo husika, kufanya uchunguzi, kutafuta suluhisho na kumpa
mteja mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa.
Bw, Luhwago alisisitiza kuwa, mchakato wa
kushughulikia malalamiko unapaswa kuzingatia misingi ya uwazi, uharaka, haki na
usiri ili kuhakikisha kila mteja anapata nafasi ya kusikilizwa na
kushughulikiwa kwa usawa.
Akizungumzia namna ya kuwahudumia wateja wagumu
(difficult customers), Bw. Luhwago alieleza kuwa, watumishi wanapaswa
kuwasikiliza wateja hao hadi mwisho, kuwatuliza wanapokuwa na hasira, kuuliza maswali
ya ufafanuzi, kufanya uchunguzi wa kina, kutafuta suluhisho linalofaa na
kuwashukuru kwa kueleza changamoto zao.
Zaidi ya hayo, Mshauri huyo wa Ubora wa Huduma kwa
Wateja wa NMB alibainisha kuwa, baadhi ya wateja wanaweza kuhitaji mbinu maalum
za mawasiliano kama vile, wanaopaza sauti, wanaolalamika mara kwa mara, walio
na hasira, wanaodai kujua kila kitu, wanaotarajia kupata huduma bila malipo na
wale wanaotumia lugha ya matusi au vitisho.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu
ya Njombe, Bw. Richard Mbambe, aliwashukuru Wawezeshaji kutoka Benki ya NMB
pamoja na watumishi wote wa Mahakama kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo
hayo na alieleza kuwa maarifa yaliyopatikana yatawasaidia watumishi kuboresha
namna ya kuwapokea na kuwahudumia wateja wa aina mbalimbali kwa weledi, utulivu
na ufanisi.
Aidha, aliwataka watumishi kuendeleza na kudumisha
ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na Benki ya NMB ili kuendelea kujifunza na
kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha
utamaduni wa utoaji wa huduma bora kwa wateja, huku yakisisitiza juu ya umuhimu
wa kusikiliza mahitaji ya wateja, kushughulikia malalamiko kwa wakati na
kuhakikisha kila mteja anahudumiwa kwa heshima, haki na weledi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa akizungumza na watumishi wa Mahakama Kanda ya Njombe (hawapo katika picha) alipokuwa akifungua mafunzo ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika hivi karibuni.
Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (kulia) pamoja na Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa NMB, Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago, wakisikiliza na kujibu maswali yaliyokuwa yanaulizwa na watumishi wa Mahakama Njombe (hawapo katika picha).
Mshauri wa Ubora wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB-Tawi la Njombe, Bw. Erick Luhwago (kushoto) na Ofisa Mikopo ya Watumishi wa Umma wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bw. Noel Urio (kulia) wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Tawi la Njombe, Bi. Regina Kavishe (hayupo katika picha).
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Njombe, Bw. Richard Mbambe akizungumza na Washiriki (hawapo katika picha) alipokuwa akifunga mafunzo hayo.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Njombe, walioshiriki mafunzo ya Huduma kwa Wateja wakiwa ndani ya ukumbi uliotumika katika mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe. Na aliyesimama ni Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Elisha Mwasomola.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (wa pili kutoka kulia), Naibu Msajili Mahakama Kuu Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyeketi kulia kwa Jaji Mfawidhi) pamoja na washiriki wengine wa Mafunzo ya Huduma kwa Mteja wakifuatilia mjadala wakati wa mafunzo hayo. Walioketi meza ya mbele ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Benki ya NMB, Tawi la Njombe.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni