Na EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama – Singida
Mahakama ya Tanzania mkoani Singida kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa haki na ustawi wa jamii imetoa
elimu kuhusu Ukatili wa Kijinsia kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha
Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu
madhara ya ukatili huo na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kuzuia na
kutokomeza vitendo hivyo.
Elimu
hiyo ilitolewa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe. Saidi Saidi ambaye
alifafanua maana ya ukatili wa kijinsia, aina zake, sababu zinazochangia
kutokea kwake, athari zake kwa mtu binafsi, familia na taifa kwa ujumla, pamoja
na wajibu wa kila mwananchi katika kupambana na vitendo hivyo.
Akizungumza
wakati wa semina hiyo, Mhe. Saidi alisema, “ukatili wa kijinsia ni changamoto
inayokiuka haki za binadamu na kuathiri ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya Taifa.
Hivyo; ni muhimu kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla kutambua viashiria vya
ukatili huo, kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanaposhuhudia au kufanyiwa
vitendo vya ukatili, na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia na
kutokomeza vitendo hivyo.”
Aidha, alibainisha kwamba, mapambano dhidi ya
ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa wadau wote ili kujenga jamii
salama, yenye usawa na inayoheshimu haki na utu wa kila mtu.
Washiriki
walipata elimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili wa
kimwili, kingono, kisaikolojia, kiuchumi na ukatili wa kimtandao. Aidha,
walielezwa kuhusu athari za ukatili huo ambazo ni pamoja na majeraha ya mwili,
matatizo ya afya, msongo wa mawazo, kuvunjika kwa familia na kupungua kwa nguvu
kazi ya Taifa.
Katika
kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, wanafunzi walifahamishwa
kuhusu sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake na watoto nchini,
zikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Kanuni ya
Adhabu, Sheria ya Mtoto, pamoja na sheria nyingine zinazolinda haki za
binadamu.
Mbali
na Mahakama, Semina hiyo ilihusisha ushiriki wa Taasisi mbalimbali ambazo ni pamoja
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dawati la Jinsia la
Jeshi la Polisi, Ofisi ya Ustawi wa Jamii pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
(NPS), ambazo kwa pamoja zilitoa elimu na ufafanuzi wa majukumu yao katika
kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na kutoa huduma kwa waathirika.
Wanafunzi
walihimizwa kutoa taarifa mara wanaposhuhudia au kufanyiwa vitendo vya ukatili
wa kijinsia, kutafuta msaada wa kitabibu kwa wakati pamoja na kutumia vyombo
vya sheria na mamlaka husika ili kuhakikisha haki inapatikana.
Kwa ujumla, semina hiyo ililenga kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, kukuza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, washiriki walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia ndani na nje ya mazingira ya chuo.
Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakifuatilia kwa makini mada kuhusu ukatili wa kijinsia iliyokuwa ikitolewa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe. Saidi Saidi.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Utemini, Mhe. Saidi Saidi akitoa mada kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu
Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida katika programu ya elimu na uhamasishaji
kuhusu masuala ya sheria.
Mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu
Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida akiuliza swali wakati wa semina ya elimu
kuhusu ukatili wa kijinsia iliyowaleta pamoja wanafunzi pamoja na wadau wa sheria kwa
ajili ya kujadili namna ya kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia.
Wadau mbalimbali wa haki jinai na sheria wakitoa elimu kwa Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kuhusu ukatili wa kijinsia huku wakisisitiza umuhimu wa kuzuia, kuripoti na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo katika jamii.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni