Ijumaa, 16 Oktoba 2026

MAHAKIMU WAPYA IRINGA WAPITISHWA KWENYE MFUMO MAALUM WA KUPIMA UTENDAJI

Na. ELEOTHERIUS PONERA- Mahakama Kuu, Iringa

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa jana tarehe 15 Oktoba, 2026, iliendesha mafunzo siku moja ya Mfumo wa Kielektroniki wa Uendeshaji na Kumbukumbu za Utendaji wa Mahakama kwa Mahakimu wapya kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Iringa.

Afisa TEHAMA, Bw John Mayagilo alieleza kuwa Mfumo huo wa e-JOPRAS (Electronic Judiciary Operation and Performance Record System), ulioundwa maalum kwa ajili ya upimaji utendaji kazi wa Maafisa wa mahakama.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo Mahakimu hao ili waweze kutumia mfumo huo kwa ufanisi katika zoezi la tathmini ya utendaji, maadili na uongozi.

Kwa mujibu wa mwongozo wa mfumo huo, e-JOPRAS ina maeneo mawili makuu ya tathmini: utendaji wa kazi za Mahakama na maadili pamoja na uongozi.

Aliongeza kuwa sehemu ya utendaji wa kazi za Mahakama inachukua asilimia 60 ya tathmini yote, na hupimwa kiotomatiki kwa kutumia data zinazotoka katika Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania (JoT-eCMS).

Vigezo vitano vinavyotumika ni pamoja na kiwango cha kumaliza kesi, kiwango cha kuondosha kesi, kupunguza kesi zilizolimbikizwa, maamuzi kutolewa kabla ya siku 90 tangu kukamilika kwa kesi, na aina ya maamuzi. Kila kigezo hubeba asilimia 12.

Bw. Mayagilo alieleza kuwa Mfumo huo pia unatoa fursa kwa mtathiminiwa kupinga au kukata rufaa. Rufaa huamuliwa na Jaji Mfawidhi kwa Mahakimu wa Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, wakati Jaji Kiongozi huamua rufaa zinazotoka kwa Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Msajili wa Mahakama Kuu, Kurugenzi ya Ukazi na Maadili na Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri.

Aliongezea kuwa mfumo wa e-JOPRAS una uwezo wa kutoa ripoti tatu: ripoti ya mtu binafsi, ripoti ya muhtasari, na ripoti ya jumla. Ripoti hizi zinaweza kufikiwa na watumiaji, watathmini na Jaji Mkuu.

Vile vile, tathmini katika mfumo huu hufanyika mara mbili kwa mwaka. Tathmini ya kwanza hufanyika Januari kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka uliopita, na ya pili hufanyika baada ya kipindi cha Januari hadi Juni.

Mzunguko wa tathmini huchukua siku 49, ambapo mtathmini (Appraiser) huchukua siku 14, mtathminiwa (Appraisee) siku saba kukubali au kupinga, mtathmini siku saba kujibu hoja, mtathminiwa siku saba kukata rufaa, na mamlaka ya rufaa siku 14. Baada ya kipindi hicho, dirisha hufungwa kiotomatiki.

Afisa TEHAMA, Bw. John Mayagil, akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

Katika picha wa kwanza kushoto ni Mhe. Deogratius Kibasa anayefata ni Mhe. Lutende Masinde, pembeni yake ni Mhe. Paschal Wenfurebe anayefuata ni Mhe. Andrew Shuma na wa mwisho ni Mhe. Fortune Mkolongo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni