Alhamisi, 15 Oktoba 2026

MBEYA YAENDESHA KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo, ameongoza kikao cha kusukuma mashauri ya jinai (Case Flow Management) kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya kwa lengo la kujadili namna bora ya uendeshaji mashauri ya jinai.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya mashauri ya jinai kwa ngazi ya Mahakama Kuu Mhe. Mpepo, alieleza kwamba, Mahakama Kuu ilikuwa na jumla ya mashauri 26 ya mlundikano na kwa sasa vikao vitatu vinaendelea vinatarajiwa kusikiliza jumla ya mashauri 20 ya mlundikano.

Mhe. Mpepo alifafanua kwamba, kuna mpango wa kuwa na kikao kingine kimoja kitakachofanyika wilayani Rungwe ifikapo Novemba 9, 2026 na kupitia kikao hicho jumla ya mashauri sita (06) ya mlundikano yaliyopo yatajumuishwa na mengine na hivyo kuondoa kabisa mashauri ya mlundikano kwa mwaka 2026.

Aidha, kikao hicho kilipitia kwa pamoja utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, ikiwemo mustakabali wa mashauri ya jinai ya mlundikano na yanayotarajiwa kuingia kwenye mstari wa mlundikano ambapo waliendelea kuazimia kwamba mashauri yanayokaribia kuwa ya mlundikano yapewe kipaumbele ili yasiingie kwenye mlundikano.

Kwa upande wa washiriki wa kikao hicho, walitoa pongezi kwa Ofisi ya Jaji Mfawidhi na Ofisi ya Naibu Msajili kwa kupunguza malalamiko ya mlundikano wa mashauri kwa kuendesha vikao vitatu vinavyobeba mashauri 28 ya Jinai jambo linalosaidia kupunguza mlundikano na hatimaye kumaliza kabisa mlundikano wa mashauri.

Naye, mwakilishi wa Mkuu wa Gereza Ruanda, SGT. Amani Mlawa alieleza juu ya malalamiko ya Wafungwa na Mahabusu kucheleweshewa kupatiwa hati za kuachiliwa kutoka mahakamani baada ya mashauri yao kusikilizwa na kuamuliwa kuachiwa huru.

Huku Ofisi ya uangalizi kwa Jamii ikitoa pongezi na shukurani kwa Mahakama kwa kuwapatia wafungwa wa vifungo vya nje wanaotumiwa katika shughuli mbalimbali za huduma kwa Jamii.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za wadau wa haki jinai Masjala Ndogo ya Mbeya za kuimarisha usimamizi wa mashauri ya jinai na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati mapema ipasavyo.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo (katikati) akiongoza kikao hicho, kulia nia Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer 

Moja ya mshiriki katika kikao hicho akichangia  kwenye majadiliano ya kikao hicho.

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakifuatilia kwa makini majadiliano ya kikao hicho.

Sehemu ya washiriki katika kikao hicho wakifuatilia kwa makini majadiliano ya kikao hicho.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni